Monday, March 28, 2011

Soma alama, ni aibu, mateso kulazimisha penzi lililokufa-GPL

Mwanzoni kabisa wakati naanza kuandika mfululizo wa makala haya, nilitoa mfano wa Ester na Sam. Jinsi ugomvi wao baada ya kuachana, ulivyochukua nafasi kubwa kiasi cha kusababisha hata wasiohusika wajue.

Kimsingi mada hii ina lengo la kukutaka uwe wa kwanza kulinda heshima yako. Usipojiheshimu hakuna hata mtu mmoja atakayekuheshimu. Usipojidhibiti, mapenzi yanaweza kukupa ugonjwa.


Sizungumzii magonjwa yanayotibika hospitali au kwa Babu Loliondo, namaanisha maradhi ya kukosa utulivu wa kichwa na moyo. Lazima uwe wa kwanza kuhakikisha huugui ‘umapepe wa mapenzi’.

Zingatia kuwa kila mtu anapenda kwa maana ya yule ambaye nafsi yake imemdondokea. Lakini haijawahi kusemwa kwamba mapenzi ni utumwa.
Inawezekana ukawa hujapata mantiki ya hoja yangu hapo. Labda nikufafanulie kuwa tatizo linalowakabili watu wengi ni kushindwa kusoma alama za nyakati.

Namaanisha kutokufahamu kipimo cha mapenzi na wakati wake. Inawezekana alikupenda na unampenda lakini mabadiliko yake yakupe picha ili ujue cha kufanya.

Unangoja akuoneshe mpenzi mwingine ndiyo ujue kuwa zama zako zimefika tamati? Akufukuze kama mbwa na matusi juu? Usingoje aibu, heri nusu shari kuliko shari kamili.

Mwanafasihi wa Kimanzichana, Abbas Hamis Kinzasa ‘20%’ katika wimbo “Ya Nini Malumbano” anaimba: “Najiweka pembeni kuepusha msongamano.” Hebu na wewe kaa pembeni kwa hiari yako.

Thamani yako ni kubwa mara sabini kama utakuwa mwelewa na kujiondoa kuliko taadhira ya kutupiwa virago. Kuna penzi hai na lililokufa, weka akilini na uheshimu.

Wiki iliyopita kuna mambo ambayo nilikutaka uyafanye unapoona mwenzi wako amebadilika. Ukishindwa yote hayo, hapo hutakuwa na lakufanya zaidi ya kuinua mikono. Uking’ang’ania, ni sawa na kukumbatia penzi lililokufa. Utateseka, utaaibika.

1. MSIKILIZE 2. JIDHIBITI 3. MKUBALIE ANACHOKITAKA 4. CHUNGUZA  KINACHOMKASIRISHA 5. USICHOCHEE MOTO 6.  USILALAMIKE

Pointi zote hizo, nilizitolea maelezo wiki iliyopita, endelea

7. KUBALI MAKOSA
Kama umegundua kuwa wewe ndiyo chanzo cha mwenzi wako kukasirika, kubali makosa na mwonyeshe kwamba unajuta kwa uliyoyafanya. Hutapungua chochote endapo utakiri makosa. Kukiri ni alama ya ukomavu wa hisia, mwenzi wako atakuheshimu.

8. MTAZAME USONI
Wataalamu wa saikolojia za mapenzi wanaeleza kuwa kutazamana usoni (hasa machoni) huwaweka jirani kihisia wapendanao. Kama mwenzio amekasirika sana, mtazame usoni kwa uso angavu usio na hata chembe ya hasira wala kinyongo. Mtazame kwa makini na mwonyeshe kwamba unamsikiliza kwa makini. Hii itakusaidia kuziteka hisia zake na kubadilisha hisia chungu alizonazo kuwa hisia za kimahaba.

9. JIAMINI
Tuliza hisia zako na jiamini kwamba japokuwa mwenzio amekasirika una nafasi ya kumfurahisha na kumfanya asahau yote yaliyomuudhi. Amini kwamba hasira ni sehemu ya maisha na kwamba kila mtu hukasirika.

10. MTULIZE KWA MAHABA
Tendo la ndoa linaaminika kuwa na uwezo mkubwa wa kuwafanya wapendanao kubadilishana hisia. Ikiwa mwenzio amekuudhi, hiyo siyo sababu ya kukufanya umbanie haki yake. Baada ya hasira kutulia, mtulize kwa kumpa mahaba mazito, hii itawaunganisha upya na kuwafanya nyote msahau yaliyotokea na kuanza ukurasa mpya.

ANGALIZO
Kwa nini uambiwe “toka”, “sikutaki” na mengine yenye kukuaibisha na kutesa moyo wako? Unapaswa kusoma alama. Ujue kipimo cha mapenzi yenu ili uwe na pakushikia.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake