ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, March 23, 2011

Mufti Simba: Chadema wanavuruga amani nchini

Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Issa bin Shabani Simba
Edom Mwasamya na Aziza Masoud
SHEIKH Mkuu wa Tanzania, Mufti Issa bin Shabani Simba amelaani maandamano yanayofanywa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), akisema yanalenga kuvuruga amani ya nchi.

Akizungumza katika mkutano wa Masheikh na Maimamu jijini Dar es Salaam jana, Mufti Simba alisema lengo la maandamano hayo yanayoendelea ni kuharibu amani ya nchi... “Wanasiasa wanataka kuivuruga nchi kwa visingizio kuwa wanataka kulinda amani, hivyo Waislamu tumeamua kuvunja ukimya uliodumu kwa muda mrefu na kuamua kukemea vitendo hivyo.”
Mjadala wa uhalali wa mikutano na maandamano ya Chadema uliibuliwa na Rais Jakaya Kikwete alipolieleza taifa katika hotuba yake ya Februari mwaka huu kuwa chama hicho cha upinzani kina lengo la kuleta machafuko nchini.

Kauli hiyo ya Rais Kikwete, iliungwa mkono na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira ambaye alikionya Chadema akisema kisije kuilaumu Serikali itakapokosa uvumulivu na kuanza kutumia dola kukishughulikia.

Simba alisema kuwa mafunzo ya dini ya Kiislamu yanawapa jukumu la kutunza amani popote walipo, hivyo wameamua kukemea vitendo hivyo kwa kuwa vinahatarisha usalama wa amani iliyopo. Alisisitiza kuwa uchaguzi ulifanyika kwa amani na walioshindwa hawana budi kusubiri kipindi kijacho badala ya kuchochea vurugu kwa kufanya maandamano nchi nzima kwa kisingizio cha kutafuta amani.

Wakati huo huo; Mufti Simba ameyashutumu mataifa ya magharibi akisema mashambulizi yake dhidi ya Kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi yana lengo la kupiga vita Uislamu.

“Hakuna kiongozi aliyesaidia Uislamu duniani kama Gaddafi, sasa wameleta chokochoko ya kuwashawishi watu kuandamana na baadaye unaibuka Umoja wa Mataifa wanavamia na kudai wanawatetea wananchi,” alisema Simba.

Alisema maandamano yaliyofanywa na wananchi wa Libya yamesababishwa na shinikizo la nchi za magharibi kwani kulikuwa hakuna sababu ya watu hao kudai kwamba hawamtaki kiongozi huyo akisema amefanya mazuri mengi kwa taifa hilo.
Alisema Waislamu wote wa Tanzania wanalaani kitendo kilichofanywa na Marekani na washirika wake na kusema Masheikh, kupitia mihadhara wataendelea kukemea kitendo kilichofanywa na nchi hizo.

“Kwa niaba ya Waislamu wote wa Tanzania nalaani kitendo hicho. Siyo cha kistaarabu, hasa ikizingatiwa kuwa mashambulizi yanayofanywa na majeshi hayo yameua watu wengi kuliko wale aliowaua Ghaddaf,” alisema.
Alisema ni wazi kabisa kuwa uvamizi uliofanywa na nchi hizo hauna baraka za Umoja wa Mataifa, bali ni matakwa ya mataifa hayo ambayo yamelenga kuhakikisha Uislamu haupati nafasi duniani.

Alisema kama kweli lengo la nchi hizo lilikuwa ni kulinda usalama wa Libya na raia wake, wangetumia njia za kidemokrasia katika kutatua tatizo hilo na wala si kwa kuivamia.

CHANZO:MWANANCHI

1 comment:

Anonymous said...

aaahhhh waliofanya mapinduzi afrika magharibi walikuwa wayahudi ?ccm imeshamnunua atishie wananchi kila mtu duniani anataka hali bora ya maisha