ANGALIA LIVE NEWS

Monday, March 7, 2011

Phiri: Sare na Yanga imetupa ubingwa

 Mechi yao yaingiza Milioni 243/-
Kocha Patrick Phiri
Sare ya juzi ya watani wa jadi imeuweka ubingwa wa ligi kuu ya bara msimu huu mikononi mwa Simba, kwa mujibu wa kocha wa klabu hiyo, Patrick Phiri. Lakini kocha wa Yanga, Sam Timbe amesema hajakata tamaa kwa sababu bado ana nafasi ya kuwavua mahasimu wao taji wanaloshikilia.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya mechi baina yao iliyoisha kwa sare ya 1-1 kwenye Uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam, Phiri alisema licha ya kutarajia ushindi katika mechi hiyo iliyochezwa juzi lakini pointi moja aliyoipata kwake ni faida kubwa na anaamini hana kizingiti katika mechi zilizobaki.

Phiri alisema kuwa anawapongeza wachezaji wake kwa kupambana kutafuta goli la kusawazisha baada ya wapinzani wao kutangulia kupata goli na ameahidi wataendelea na kasi hiyo katika mechi nyingine ambazo zitawaweka sawa kwa ajili ya mechi yao ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe itakayochezwa Machi 20 mjini Lubumbashi.
"Matokeo haya si mabaya, bado ubingwa uko mikononi mwetu kwa sababu hatuko katika nafasi mbaya kama walivyo wapinzani wetu, tutajituma ili tutimize malengo yetu," alisema Phiri.
Aliongeza kuwa katika mchezo huo wachezaji wake walicheza vizuri zaidi na kuwapa wakati mgumu wapinzani wao lakini bahati ya kufunga haikuwa kwao.
"Nimejifunza baadhi ya vitu, nitavifanyia kazi ili kuwa kwenye nafasi nzuri zaidi katika safari yetu ya kutetea ubingwa, hakuna kulala, kila timu inataka kupata mafanikio," aliongeza.
Phiri alisema pia kutokana na kiwango ambacho timu yake inacheza bado ndio timu bora msimu huu ambapo juzi mabeki pamoja na kipa chaguo la kwanza la timu hiyo, Juma Kaseja, walidhihirisha.
Naye Timbe ambaye hakuwa anafahamu kwamba Yanga imecheza mechi moja zaidi ya Simba alisema kuwa ligi hiyo yenye timu chache ni ngumu na bingwa atajulikana katika mchezo wa mwisho.
Timbe alisema kuwa ni mapema kutaja timu itakayotwaa ubingwa kwa sababu katika mechi tano zilizobakia lolote linaweza kutokea.
"Mechi ilikuwa ngumu sana lakini bado hakuna anayeweza kujua bingwa atakuwa nani, ligi bado inaendelea, ni kama mbio za marathoni, hadi mwisho ndio bingwa atajulikana," alisema Timbe na kuongeza kwamba kwake mechi dhidi ya Simba ni sawa dhidi ya timu nyingine za ligi hiyo.
Kutokana na matokeo hayo ya juzi, Yanga imeendelea kuongoza katika msimamo wa ligi baada ya kuwa na pointi 39 na Simba itakayoshuka tena dimbani keshokutwa kucheza mechi yake ya kiporo dhidi ya Ruvu Shooting kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro ni ya pili kutokana na pointi 38 ilizonazo na Azam FC inayowapa 'homa' ikiwa ni ya tatu.
Simba inaondoka leo saa sita mchana kulekea Morogoro kwa ajili ya kujiandaa na mechi ya Ruvu Shooting.
Wakati huo huo, timu za Yanga na Simba kila moja imepata Sh. Milioni 51.1 ikiwa ni mgawo wa mapato yaliyopatikana katika mechi yao ya juzi ambayo iliingiza Sh. Milioni 243 zilitokana na jumla ya mashabikiri 46,539 waliooingia uwanjani kwa tiketi, taarifa ya Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura ilisema jana.
CHANZO: NIPASHE

No comments: