
Na Walusanga Ndaki
Aliyekuwa mdogo wa Malkia Elizabeth wa Pili wa Uingereza
Hospitali ya Muhimbili iliwahi kupewa jina lake
KWA wanaokumbuka vizuri, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili iliwahi kuitwa Princess Margaret Hospital tangu mwaka 1956 hadi baada ya uhuru mwaka 1961 ilipobadilishwa na kuitwa Hospitali ya Muhimbili.
Aliyekuwa mdogo wa Malkia Elizabeth wa Pili wa Uingereza
Hospitali ya Muhimbili iliwahi kupewa jina lake
KWA wanaokumbuka vizuri, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili iliwahi kuitwa Princess Margaret Hospital tangu mwaka 1956 hadi baada ya uhuru mwaka 1961 ilipobadilishwa na kuitwa Hospitali ya Muhimbili.
Ilipewa jina hilo kumtukuza mwanamke huyo aliyekuwa mdogo wake
Malkia Elizabeth wa Pili wa sasa wa Uingereza kwani wakati huo Tanzania ilikuwa chini ya ukoloni wa Uingereza.
Kabla ya hapo, hospitali hiyo ilikuwa ikijulikana kwa jina la Sewa Haji.
Princess Margaret aliyekuwa na cheo cha kifalme cha Countess of Snowdon, aliyezaliwa Agosti 21, 1930 akijulikana kama Margaret Rose, alifariki Februari 9, 2002.
‘Mage’ (pichani) na Elizabeth walikuwa mabinti wa Mfalme George wa Sita na mkewe Malkia Elizabeth. Malkia Elizabeth wa Pili wa sasa alirithishwa jina la mama yake.
Maisha yake yalibadilika ghafla mwaka 1936 wakati baba yao mkubwa, Mfalme Edward wa Nane, alipoliacha taji na kuamua kumuoa mwanamke wa Kimarekani, Wallis Simpson, jambo lililosababisha baba yake (Margaret) kuwa Mfalme wa Uingereza.
Hivyo yeye na dada yake (Elizabeth) wakaingia kikamilifu katika ukoo wa kifalme, Mage akiwa Malkia mtarajiwa iwapo dada yake huyo angefariki au kupatwa na janga lolote.
Baada ya Vita Kuu ya Pili mwaka 1945, aliolewa na jamaa aliyeitwa Peter Townsend, mtu ambaye familia ya kifalme na Kanisa la Uingereza hawakumpenda, hivyo akaolewa tena na mpiga picha Antony Armstrong-Jones, ambaye naye walitengana 1978.
Kikazi alijihusisha na mambo mengi ya kijamii yaliyotokana na heshima ya kuwa katika jamii ya kifalme.
Mwaka 1952, baba yao, Mfalme George wa Sita, alifariki na nafasi yake kuchukuliwa na Elizabeth wa Pili ambaye tangu wakati huo ameendelea kuwa Malkia wa taifa hilo mashuhuri duniani.
Maisha yake ya ndoa kila mara yaliitatiza familia hiyo ya kifalme kutokana na kuolewa na kuachika mara kwa mara. Mbali na kuwa na uhusiano wa kimapenzi na wanaume wengi.
Pia, maisha ya Margaret yaliandamwa na magonjwa yaliyomfanya ashindwe hata kutembea. Mwanamke huyo alianza kuvuta sigara akiwa na umri wa miaka 15 hadi uzeeni.
Januari 5, 1985 sehemu ya pafu lake la kushoto iliondolewa, jambo ambalo pia liliwahi kumtokea baba yake miaka 30 hapo nyuma.
Mnamo 1991 aliacha kuvuta sigara, lakini akaendelea kulewa kwa nguvu ambapo mwaka 1993 alilazwa hospitalini kutokana na kichomi (pneumonia). Mwaka 1998 akakumbwa na kiharusi na mwaka uliofuata akababuka miguu katika ajali iliyompata akiwa bafuni, jambo ambalo lilimfanya ashindwe hata kutembea mpaka awe ameshikiliwa na wakati mwingine alitumia kiti cha magurudumu.
Kati ya Januari na Machi 2001, alikumbwa na matukio kadhaa ya kiharusi yaliyomwacha nusu ya kushoto ya mwili wake ikiwa imepooza. Mara ya mwisho kuonekana hadharani ulikuwa wakati wa kuadhimisha mwaka wa 101wa kuzaliwa kwa mama yake Agosti 2001 na kwenye hafla ya kutimiza mwaka wa 100 tangu kuzaliwa kwa shangazi yake, Princes Alice iliyofanyika Desemba mwaka huo.
Mage alifariki dunia katika Hospitali ya Mfalme Edward wa Saba siku ya Februari 9, 2002 akiwa na umri wa miaka 71; hii ni baada ya kukumbwa tena na kiharusi.
Maiti yake ilichomwa moto Februari 15, mwaka huo, siku ya kutimia miaka 50 tangu kuzikwa kwa baba yake. Hiyo ndiyo siku ambayo Mama wa Malkia (Elizabeth) naye alionekana hadharani kabla ya kufariki wiki sita baadaye.
Majivu ya Mage yalizikwa baadaye kando ya makaburi ya wazazi wake– Mfalme George wa Sita na Malkia Elizabeth– miezi miwili baadaye katika Kanisa la Mt. George.
CHANZO:GLOBAL PUBLISHERS
No comments:
Post a Comment