ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, March 9, 2011

Serikali yagoma kuwataja vigogo dawa za kulevya

9th March 2011

Waziri William Lukuvi
Serikali imesema haitaitangaza hadharani orodha ya “vigogo” wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya kwa vile kufanya hivyo bila ushahidi wa kutosha ni kinyume cha Katiba ya nchi.
Kauli hiyo ilitolewa na jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alipokuwa akitoa taarifa ya hali ya dawa za kulevya ya mwaka 2009 kwa waandishi wa habari.
Alisema Katiba inaizuia serikali kumtendea mwananchi kama mhalifu pasipo na ushahidi kwa sababu tu jina lake limetajwa na mtu au watu kuwa anahusika na biashara ya dawa za kulevya.

“Ni kweli tuna majina ya vigogo wa biashara hii. Lakini ieleweke kuwa vigogo ni wale wanaoiendesha biashara ya dawa hizi. Na katika kundi hili, kuna watu wa kutoka katika makundi mbalimbali ya kijamii, ambamo ndani yake wanaweza wakawemo wafanyabiashara na wanasiasa,” alisema.
Alisema nchi inaendeshwa kwa misingi ya sheria na kwa hiyo ni pale utakapopatikana ushahidi wa vielelezo na ikathibitika kuwa kweli kigogo au vigogo wana kesi ya kujibu ndipo watapelekwa mahakamani.
Mkuu wa Kitengo cha Kuzuia Dawa za Kulevya cha Jeshi la Polisi nchini, Kamishna Mwandamizi Msaidizi wa Polisi, Godfrey Nzowa, alitolea ufafanuzi taarifa zilizoandikwa kwenye baadhi ya vyombo vya habari nchini zilizoeleza kupotea kwa baadhi ya dawa za kulevya zilizokamatwa Tunduma mkoani Mbeya.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), Kamishna Robert Manumba, aliwataka Watanzania kuelewa kuwa eneo la Afrika Mashariki hivi sasa linakabiliwa na uhalifu, ambao unaihangaisha dunia nzima.
CHANZO: NIPASHE

No comments: