Leon Bahati
WAZIRI Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye amejibu shutuma mbalimbali ambazo zimeelekezwa kwake na Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi huku akisema kauli za hivi karibuni za Umoja wa Vijana wa Chama hicho (UVCCM) ni matusi, kejeli na hatari kwa taifa.Sumaye (pichani) aliwaambia waandishi wa habari jana, Dar es Salaam kwamba CCM bado ni chama kinachotegemewa kuleta maendeleo kwa Watanzania siku zijazo lakini kauli za makada wake hao ni kali na zinaashiria kuwa hakina budi kusafishwa ili kirudi kwenye mstari.
"Future (mustakabali wa baadaye) ya CCM ni nzuri, ila kuna mambo lazima yafanyike. Udhaifu lazima tuuondoe," alisema Sumaye ambaye ni mwanachama mwanzilishi wa CCM na kuongeza:
"Chama kinapaswa kujivua magamba, nami nafikiri hii ndiyo njia sahihi ya kukijenga upya ili kiendane na misingi yake."
Hivi karibuni Baraza Kuu la UVCCM Taifa likitanguliwa na lile la Mkoa wa Pwani, walitoa kauli kali za kuwatisha viongozi wanaokikosoa chama hicho nje ya vikao, wakisema lengo lake ni kuharibu mustakabali wa CCM.
Umoja huo uliapa kuwa utafanya kampeni za kuhakikisha viongozi hao, uliodai kuwa wana malengo ya kupata Urais mwaka 2015, hawapati nafasi yoyote ya uongozi.
Sumaye ambaye alijiunga na Umoja wa Vijana wa Tanu wakati huo ukijulikana kama Tanu Youth League (TYL) mwaka 1969 alisema: "Kama UVCCM ingefanya kazi kwa vitisho na ubabe namna hiyo tangu awali, sidhani kama tungelikuwa na CCM tunayoiona leo."
Shutuma dhidi yake
Sumaye alijibu shutuma za vijana hao wa CCM na kuzitolea majibu, moja baada ya nyingine huku akisema kuwa lengo lake si kushindana wala kupimana nguvu, bali kueleza hali halisi ili wananchi wajue kinachoendelea.
Alisema chimbuko la kutupiwa kwake lawama kali ni ushauri wake wa kutaka CCM, ijibu tuhuma zinazotolewa na Chadema kwenye maandamano na mikutano yake ya hadhara.
"Baada ya kuona kazi za kisiasa wanazofanya Chadema za maandamano na mikutano ya hadhara na sisi CCM bado tuko kimya na badala yake tumeachia kazi zote Serikali, nikashauri kwa nia njema kabisa kuwa CCM nayo ifanye kazi ya siasa, kujibu hoja za chama hicho (Chadema).
"Kusema CCM ifanye, ni kiswahili safi tu, maana nazungumzia chama. CCM ifanye haiimanishi mimi simo kama walivyotafsiri baadhi ya wananchama na viongozi wa chama. Sijasema Serikali isifanye kazi yake. Kwa kweli Serikali inafanya kazi yake kama tulivyoshuhudia Waziri (wa Nchi Ofisi ya Rais Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira akitoa msimamo wa Serikali.
"Malumbano ya kisiasa hujibiwa kisiasa, CCM walitakiwa kuwajibu Chadema na si kazi ya Serikali kufanya kazi ya kisiasa. CCM kinafahamu kazi ya kisiasa na kimekuwa kikifanya hivyo tangu zamani. Viongozi wetu wamekuwa wakifanya hivyo katika ngazi zote. Ni shughuli ya chama na haihitaji maamuzi ya vikao.
"Mimi ni mmoja wa walioshambuliwa sana na niko hapa kujiwakilisha mwenye, sijakutana na wengine, hawajanituma na wala siwasemei hao," alisema.
"Nimeshutumiwa kuwa namshutumu mwenyekiti wa chama. Nilijibu nikadhani mambo yamekwisha kumbe ndiyo kwanza yameanza. Nimeshutumiwa na UVCCM Pwani kuwa (mimi) Sumaye na (Edward) Lowassa wana mpango wa kukivuruga chama ili wafikie malengo yao ya 2015. Kama Lowassa na Sumaye wanautaka urais 2015, kwa nini washirikiane? Je, 2015 kutakuwa na marais wawili?" Alihoji Sumaye akisisitiza:
"Unapotaka urais kupitia chama fulani, hivi unakidhoofisha au unakiimarisha? Busara ya kawaida inakataa kuwa unadhoofisha chama chako ili ukitumia kupata urais."
Alizungumzia madai ya UVCCM kuwa anapaswa kujua kuwa kwa kumtukana Rais Kikwete na Serikali yake hawatafanikiwa malengo yao. Alisema: "Hii ni shutuma ya ajabu. Mimi sijawahi wala siwezi kuthubutu kumtukana Rais wangu. Sijalelewa hivyo na wala sijajifunza hiyo tabia mbaya."
"UVCCM wanadai sisi (Sumaye na baadhi ya viongozi) tumeshiba na sasa tumevimbiwa... Tuwaache nao wale kama sisi. Haya ni matusi na kejeli na inasikitisha sana."
Alisema kauli hizo zinaashiria kwamba UVCCM wana watu wao ambao wanawapigania ili nao wale ama kufaidika. Alisema kama vijana wana mtu wanayempigania ili nao wapate zamu yao ya kula basi hata amani, usalama na mshikamano wa Tanzania upo shakani.
"Itakuwa ni kudra ya Mwenyezi Mungu kumpata kiongozi bora kwa sababu tutakuwa tunampima si kwa uwezo wake wa kuongoza, bali wa kushibisha matumbo ya baadhi."
Sumaye pia alishutumu vikali kauli ya UVCCM Mkoa wa Pwani kuwa viongozi wanaokisema CCM nje ya vikao wameacha utaratibu mzuri wakidhani wanakikomoa na kufikiri kuwa ni lazima Rais atoke Kaskazini akisema huo ni ubaguzi ambao unaweza kukigawa chama na hata taifa.
"Tusitazame watu kwa wanakotokea au dini na rangi zao. Hata bungeni kuna kauli za kibaguzi, tumezikemea bila kujali eneo," alionya Sumaye.
Kuhusu shutuma zilizotolewa na Makamba pamoja na Lukuvi kwamba alizungumza nje ya vikao huku wakihoji yuko chama gani kwa kusema CCM ijibu mapigo na kwamba yote yaliyomfika amejitakia kwa sababu ya utovu wake wa nidhamu, alisema alisikitishwa na kauli hiyo aliyoisoma kwenye gazeti moja la Kiswahili (siyo Mwananchi) na kuhoji … "Imekuwaje wao wakatumia chombo hicho cha habari kama kikao cha chama?"
Lakini, Sumaye alisema alipowasiliana na Lukuvi alidai kuwa hajawahi kutamka maneno hayo.
Kugombea Urais
Sumaye alisema hana uhusiano mbaya na UVCCM na kwamba kuhusu kugombea urais hajaamua kuwa atagombea au la.
Alisisitiza: "Wananchi ndiyo wenye uwezo wa kila jambo katika nchi, ndiyo wanaopiga kura na ndiyo wanaoamua nani awe kiongozi na nani asiwe."
Alipinga vikali kauli ya UVCCM kuwa wanaweza kuendesha kampeni kumzuia mtu kuchaguliwa kuwa Rais wa Tanzania akisema makundi yenye dhamana hiyo ni wananchi, chama na dola.
Uhuru wa kuongea
Sumaye alisema kuwa kitendo cha kumshutumu kuwa kauli hakuna maana kwa sababu mtu yeyote, awe mwanachama au kiongozi ndani ya chama ana uhuru wa kuongea.
"Kiongozi asipokuwa na uhuru wa kutoa yale anayofikiria kuwa sahihi basi hana sababu ya kuwa kiongozi. Ni kweli kuna maoni mengine ambayo yanaweza kuwa na athari kwa chama na hasa kama yanakwenda kinyume na sera, itikadi na kanuni."
"Ni juu ya kiongozi husika kupima yale ayasemayo. Ni lazima tukubali kwenye chama chenye demokrasia kama chetu, uhuru wa kutoa maoni lazima nao uwepo... Kundi moja ambalo limeendelea kupata shida (ndani ya CCM) ni la wastaafu."
Lazima tukiri kuwa wastaafu wana ujuzi ambao watu wanapenda kuutumia na hivyo kulazimika kusema.
Kumsema rais, chama
Sumaye alisema katika demokrasia kusemana au kusemewa ni jambo ambalo haliepukiki labda iwe ni kwenye utawala wa kiimla.
"Demokrasia maana yake ni chetu kwa ajili yetu. Penda tusipende chochote ambacho watu wamekiweka wao kwa ajili yao na ni chao lazima watakisema au kukisemea."
Kwa sababu hiyo alisema iwe chama, Serikali au rais anayeongoza kwa misingi ya demokkrasia lazima asemwe au asemewe… "Mfumo au taasisi ambayo haisemwi wala kusemewa ni ya kiimla. (Baba wa Taifa) Mwalimu Nyerere aliwahi kusema waacheni waseme, Mungu amewapa midomo ya kusema, wewe utawazuiaje?
Kero ndani ya CCM
Sumaye alisema kauli za mtu yeyote anayezungumzia jambo zito kuhusu chama na kuambiwa kuwa anautaka urais inaweza kuwaziba wengi midomo akasema kinachoonekana ndani ya CCM hivi sasa ni kwamba: "Tunakosa muda wa kujielekeza katika mambo ya msingi tunaanza siasa za
kupakana matope."
Sumaye ambaye alikuwa Mbunge wa Hanang, alisema alitumia fursa hiyo kujibu shutuma dhidi yake na hatarajii kuibua malumbano na kwamba hataongea tena kuhusu hilo na waandishi wa habari.
Msimamo wa UVCCM
Jumatatu iliyopita, Kaimu Mwenyekiti wa UVCCM, Benno Malisa alitoa maazimio ya kikao cha Baraza Kuu la UVCCM Taifa akisema wamekusudia kuhakikisha kwamba vigogo ambao wamekuwa wakizungumza nje ya utaratibu wa vikao wanatupwa nje ya ulingo wa siasa za chama hicho tawala.
Kauli hiyo Ilionekana kuwalenga baadhi ya makada wa CCM wakiwamo, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe, Lowassa na Sumaye ambao wamekuwa wakishutumiwa kwa kuzungumza mambo ya chama hicho nje ya vikao.
CHANZO:Mwananchi
No comments:
Post a Comment