Ni Umoja wa Vijana waliokutana Pwani
Wawatuhumu kudhoofisha serikali, CCM
Wadai wanasumbuliwa na urais wa 2015.jpg)
Walioko serikalini kwa mustakabali wa taifa kwani wameonekana dhahiri kuchoka na hawana tija yoyote kutokana na kumwachia yeye (Rais Kikwete) afanye kazi zote.
Kauli hiyo nzito ilitolewa jana mjini Bagamoyo na Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Pwani, Abdalah, Ulega, wakati wa kikao cha Baraza Kuu la Umoja huo Mkoa wa Pwani.
Mkutano huo ulihudhuriwa na baadhi ya wabunge wa CCM, wenyeviti na makatibu wa umoja huo kutoka mikoa mbalimbali nchini.
Pia, alikuwepo Kamanda wa UVCCM Mkoa wa Pwani ambaye pia ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, na Mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM Taifa akiwakilisha mkoa wa Pwani, Ridhiwani Kikwete.
Akianza na Sumaye, Ulega alisema Waziri Mkuu huyo mstaafu anashangaza kwa kuiambia CCM ijibu mashambulizi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kana kwamba yeye si mwanachama wa CCM.
Alisema licha ya kuwa Sumaye ni mwanachama wa siku nyingi wa CCM, pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho hivyo ana wajibu wa kukisaidia chama badala ya kukinyooshea kidole.
“Kila kitu anabebeshwa Kikwete, hivi atafanya kazi ngapi, kwani Sumaye yeye yuko chama gani hadi aseme CCM ijibu mapigo ya Chadema, inaonekana kuna watu wakubwa serikalini na kwenye chama ambao wamechoka, tunawashauri wajiondoe wenyewe ama Kikwete awatoe kafara kwa ajili ya mustakabali wa chama,” alisema huku akishangiliwa na vijana waliokuwa kwenye mkutano huo.
Alisema Sumaye kwa wadhifa aliopata kuwa nao ndani ya serikali kama ana mambo mazuri ya kuishauri serikali ana nafasi ya kuonana na mwenyekiti wa chama hicho na kumshauri badala ya kuzungumza bila mpangilio.
Ulega alisema Sumaye na Lowassa wana mpango wa kukivuruga na kukidhoofisha chama hicho ili wafikie malengo yao katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
“Hawa nawaambia ukweli wajue kuwa sote tuko kwenye jahazi moja ambalo ni CCM, sasa kama wanataka kulitoboa hili jahazi wajue tutazama sote na hakuna atakayepona,” alisema Ulega na kuongeza:
“Sisi vijana hatuwezi kukubali kuona jahazi linatobolewa, ndiyo maana tunamwomba Kikwete awatose wao kwanza kabla hawajatimiza malengo yao.”
Akizungumzia kauli ya Lowassa ya kutaka serikali iongeze mishahara kwa watumishi wake, Ulega alisema kama angekuwa na nia njema angezungumzia suala hilo kwenye vikao husika kwenye chama na serikalini kwa kuwa bado ni Mbunge wa CCM.
Ulega alisema hatua ya kutamka maneno hayo hadharani ni nia ya dhati ya kukidhalilisha chama na serikali kuwa imeshindwa kazi.
“Lowassa alikuwa Waziri Mkuu miaka michache iliyopita, ina maana hajui hali halisi ya uchumi wa nchi, inamaana ameshindwa kabisa kuonana na Rais Kikwete faragha na kumshauri hayo aliyoyasema badala ya kuzungumza kwenye vyombo vya habari….Si bure hawa naona kuna mambo wanatafuta kwa malengo yao binafsi ya mwaka 2015,” alisema bila kufafamua.
“Lakini wanapaswa kujua kuwa mgombea wa CCM atakayesimamishwa na chama hiki mwaka 2015, ushindi wake utategemea zaidi mafanikio ya kiutendaji wa Rais Kikwete.
“Wanapaswa kujua kuwa kwa kumtukana Kikwete na serikali yake hawatafanikiwa kufikia malengo yao,” alisema Ulega.
Alisema kuna viongozi wakubwa serikalini ambao hawapaswi kuwepo kwenye nafasi walizonazo kwani wanashindwa kumsaidia Rais Kikwete katika kutekeleza majukumu yake.
Hata hivyo, hakuwa tayari kutaja jina la kiongozi yeyote wala wizara au idara mahususi ambazo zimekwama kumsaidia Rais Kikwete.
Ulega alisema lawama na shutuma zote zimekuwa zikielekezwa kwa Rais Kikwete, lakini watendaji hao wanashindwa kujibu na kufafanua malalamiko hayo wakimsubiri Rais Kikwete ndiye atoe matamko.
“Hivi Kikwete atazungumzia mambo mangapi jamani, mfano huu mfumko wa bei hakuna mtu wa kulitolea ufafanuzi hadi Rais ndiye azungumze? Watu wanakaa kimya, lakini wakiibuka wanaibuka na masuala ya kumbomoa Rais Kikwete na chama chetu,” alisema.
Hivi karibuni Lowassa amekuwa akizungumzia hadharani mambo mbalimbali, mapema mwaka huu baada ya vurugu za mkoani Arusha ambako polisi waliua watu watatu kwa kuwapiga risasi wakizuia maandamano ya Chadema, alitaka CCM na Chadema wakae wazungumze na kuepusha kuingiza nchi katika machafuko kama ya Ivory Coast.
Kadhalika, akiwa amekwisha kuchaguliwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na Usalama, Lowassa alifanya mkutano na waandishi wa habari katika Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (KIA) akitokea Dar es Salaam, na kuitaka kuundwa kwa kamati kupitia mishahara ya watumishi wa umma kwa kuwa gharama za maisha zimepanda sana.
Kwa upande wake, Sumaye alisema CCM haina sababu ya kutishwa na maandamano ya Chadema, bali ni kujibu hoja zinazotolewa na chama hicho kuhusu gharama za maisha, mgawo wa umeme na malipo ya Sh. bilioni 94 kwa kampuni ya kufua umeme ya Dowans Tanzania Limited.
Sumaye na Lowassa walipotafutwa jana kuzungumzia tuhuma dhidi yao zilizotolewa na Ulega, hawakupatikana.
Simu ya Lowassa ilikuwa inaita bila kupokelewa wakati simu ya sumaye ilikuwa imefungwa.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake