ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, March 27, 2011

`Super Sub` Samatta aibeba Stars Afrika

Mshambuliaji Mbwana Samatta jana alitoka benchini na kuifungia Taifa Stars bao la ushindi wa 2-1 wa dakika za majeruhi dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, baada ya wenyeji kwenda mapumziko wakiwa nyuma kwa goli moja, kwenye Uwanja wa Taifa.
Ushindi huo uliorudisha matumaini ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika za mwakani umeiwezesha Stars kufikisha pointi nne sawa na Afrika ya Kati na ni Morocco tu yenye pointi nne pia ambayo inaweza kuzivuka kama itaifunga Algeria ugenini leo.

Samatta ambaye ameibuka kuwa mfungaji hatari kwenye ligi kuu ya Vodacom tangu kujiunga na kambi ya Simba mwishoni mwa mwaka jana, alifunga baada ya kuunganisha kwa kichwa mpira wa kona uliopigwa na Nurdin Bakari.
Kona hiyo ilipatikana wakati baadhi ya wapenzi wenye moyo mdogo wakiwa wameshaanza kutoka uwanjani kutokana na kumalizika kwa muda wa kawaida wa mchezo na jitihada za Afrika ya Kati kupoteza muda kwa kujiangusha uwanjani kadri ilivyoweza.
Mshindi wa kundi pekee ndiye atakuwa amejihakikishia nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika za Guinea ya Ikweta na Gabon za mwakani.
Kiungo Shaaban Nditi aliifungia Taifa Stars bao la kusawaziswha dakika nne tangu kuanza kwa kipindi cha pili baada ya kuunganisha krosi ya Mrisho Ngassa ambaye jana aling'ara katika wingi ya kushoto.
Afrika ya Kati ilipata bao la uongoza ndani ya sekunde 120 za kwanza lililofungwa na Salif Keita baada ya kuuwahi mpira uliotemwa na Shaaban Kado langoni mwa Stars.
Stars ingeweza kwenda mapumziko ikiwa sare na wageni kama Athumani Machupa asingepoteza nafasi nzuri ya kufunga katika dakika ya 17 alipoitoka beki ya Afrika ya Kati lakini shuti alilopiga lilitolewa na kuwa kona.
Nurdin Bakari ambaye alikuwa na nyota ya magoli katika michuano ya Kombe la Chalenji alipoteza nafasi nyingine nzuri ya Stars mwanzoni mwa kipindi cha pili.
Mbali na kumuingiza Samatta kuchukua nafasi ya kiungo Henry Joseph, kocha wa Stars Jan Poulsen alifanya mabadiliko mengine mawili yaliyoongeza uhai wa mashambulizi katika kikosi kilichocheza hovyo kipindi cha kwanza.
Aliwapumzisha pia beki wa pembeni Idrissa Rajabu wa Sofapaka ya Kenya na nafasi yake kuchukuliwa na Stephano Mwasika wa Yanga ambaye hupenda kushambulia zaidi, na John Bocco kuchukua nafasi ya Machupa.
Poilsen alisikitikia nafasi nyingi ambazo Stars ilipoteza kutokana na tatizo la umaliziaji, "hasa katika kipindi cha kwanza."
Kocha wa Afrika ya Kati Accori Julius alisema timu yake ilikuja kutafuta sare, na akasikitika kukataliwa kwa bao la kuotea ambalo alidai ni halali.
Stars ambayo imebakiwa na mchezo mmoja nyumbani dhidi ya Algeria Septemba, itarudiana na Afrika ya Kati Juni kabla ya kumaliza na Morocco ugenini Oktoba.
Timu zilikuwa:
Stars:Shaaban Kado, Shadrack Nsajigwa, Idrissa Rajabu (Stephano Mwasika), Aggrey Moris, Nadir Haroub, Nurdin Bakari, Shaaban Nditi, Mohammed Banka, Henry Joseph (Mbwana Samatta), Athumani Machupa (John Boko), Mrisho Ngassa.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments: