ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, March 22, 2011

Tibaijuka aomba ulinzi kwa Rais

  Ni urejeshaji viwanja vilivyoporwa
  Tanroads Mara wampuuza Pinda
Rais Jakaya Kikwete, akisalimiana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, alipowasili katika wizara hiyo aliyoitembelea jana. Kulia ni Naibu Waziri wa wizara hiyo, Goodluck Ole Medeye.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, amemuomba Rais Jakaya Kikwete kumkingia kifua katika kurejesha viwanja vilivyoporwa.
Profesa Tibaijuka alitoa ombi hilo alipokuwa akisoma taarifa ya wizara yake kuhusu utekelezaji wa maagizo ya Rais Kikwete alipotembelea wizara hiyo baada ya kuzungumza na viongozi na watendaji wa Wizara ya Ujenzi katika ofisi za Wakala wa Ujenzi jijini Dar es Salaam jana.

Rais Kikwete alitembelea wizara hiyo kwa lengo la kuangalia utekelezaji wa maagizo yake aliyoyatoa wakati wa ziara yake aliyoifanya wizarani hapo Januari mwaka 2006.
“Mheshimiwa Rais, katika kutekeleza hilo (kurejesha viwanja vilivyoporwa) naomba unikingie kifua,” alisema Profesa Tibaijuka na kujibiwa na Rais Kikwete: “We chapa kazi tu, usionee. Penye haki fanya. Ukisimamia maadili watu watakuona jeuri tu.”
Alisema miongoni mwa mambo, ambayo wizara yake inashughulikia hivi sasa, ni pamoja na kurejesha viwanja vilivyoporwa, vikiwamo vile vya wazi. Rais Kikwete alisema viwanja vya wazi, kama vile vya Jangwani, wakati wa enzi za utoto wake, vilikuwa vikitumika kwa michezo, lakini hivi sasa baadhi ya watu wameanza kuvitumia kwa ujenzi.
“Kuna mtu amejenga nyumba zake pale (Jangwani), sijui ndio nyie (wizara)?” alihoji Rais Kikwete.
Waziri Tibaijuka alisema asilimia 90 ya ardhi nchini haijapimwa na kumilikishwa, hali ambayo imekuwa ikizua migogoro.
Alisema miongoni mwa maagizo ya Rais Kikwete, yaliyotekelezwa na wizara yake ni pamoja na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma. Profesa Tibaijuka alisema katika kutekeleza agizo hilo, wizara imewafukuza watumishi wanane, kati yao mmoja amefikishwa mahakamani kwa tuhuma za utovu wa maadili kazini.
Alisema wizara imeandaa mpango kabambe wa kujenga miji mipya katika maeneo ya Kawe, Buguruni na Kigamboni katika jiji la Dar es Salaam ili kupunguza msongamano wa watu wanaokimbilia kupata mahitaji katika eneo moja peke yake, kama Kariakoo.
Maeneo yatakayojengwa miji hiyo, ni Buguruni, ambako watatumia wakazi wa Wilaya ya Ilala; Kawe (wakazi wa Wilaya ya Kinondoni); na Kigamboni (wakazi wa Wilaya ya Temeke).
Waziri Tibaijuka kupitia maofisa waandamizi wa wizara hiyo, alisema mpango mji wa uendelezaji wa mji mpya wa Kigamboni, umegharimu Sh. bilioni 2.5.
Alisema mradi mzima wa ujenzi wa mji mpya wa Kigamboni utagharimu Sh. trilioni 11.6 na kwamba, hivi sasa zinahitajika Sh. trilioni 1.6 ili kuanza utekelezaji wake.
Profesa Tibaijuka alisema awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi huo, kutakuwa na daraja la urefu wa mita 60 kwenda juu litakalojengwa karibu na ofisi na makazi ya Rais, Ikulu.
Hata hivyo, suala hilo lilipingwa vikali na Rais Kikwete kwa kusema: “Chukueni tahadhari. Hamuwezi mkajenga daraja juu karibu na ofisi ya Rais. Maana mtu anaweza kukaa juu na mzinga wake akashambulia makazi ya Rais. Hata ukienda Marekani huwezi kukuta kitu kimejengwa juu ya White House, Uingereza na nchi yoyote duniani ni hivyo hivyo.”

AITAKA UJENZI KUTOTUMIA UBABE
Mapema akizungumza na uongozi na watendaji wa Wizara ya Ujenzi, Rais Kikwete aliitaka wizara hiyo kuacha kutumia ubabe katika kubomoa nyumba za wananchi kwa kutumia Sheria ya Hifadhi ya Barabara.
Alisema serikali haipaswi kutafuta unafuu katika kutekeleza suala hilo kwa gharama ya wananchi.
“Serikali ina fedha za kutosha kulipa fidia wananchi, hivyo kabla ya kubomoa nyumba zao inapaswa kwanza irejee historia ya barabara inazotaka kuzibomoa,” alisema Rais Kikwete.
Alisema waliojenga nyumba katika kipindi, ambacho barabara zilikuwa za kawaida, wanastahili kulipwa fidia isipokuwa wale waliojenga baada ya barabara hizo kuendelezwa baadaye na serikali. “Kitendo mnachokifanya ni kinyume cha sheria. Lazima wakati mwingine muwe na huruma kwani kumpa mtu saa 48 kubomoa nyumba yake si kitendo cha kibinadamu, ikiwezekana muwape muda wa kujiandaa kuhama kati ya miaka miwili hata mitatu,” alisema.
Alisema kuna baadhi ya maeneo, ambayo barabara zake ni nyembamba kutokana na mazingira na kutoa mfano wa maeneo ya milimani kama Lushoto, mkoani Tanga.
Alisema watu waliojenga maeneo hayo kama watabomolewa nyumba zao hawatapata pa kwenda kwani eneo kubwa ni la milima, hivyo kama watahamishwa watakosa pa kwenda na barabara zitakazojengwa zitakosa watu wa kuzitumia. Aliitaka Wizara ya Ujenzi kuhakikisha barabara zinazojengwa nchini kuwa za viwango vinavyotakiwa, vitakavyowezesha barabara hizo kudumu kwa miaka 15 bila ya kuwa na dosari.
Naye Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, alisema kwa sasa fedha zilizoko kwa ujenzi wa barabara nchini hazitoshi na kwamba wakandarasi 35 wameshatoa notisi kwa serikali ya kusimamisha ujenzi.

TANROADS MARA WAMPUUZA PINDA
Wakati Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akitangaza kusitishwa kwa zoezi la bomoa bomoa lilotangazwa na Magufuli, nchini kote, Wakala wa barabara Tanzania (Tanroads) mkoani Mara umesema haujapokea maelekezo ya serikali na kwamba utaendelea na bomoabomoa.
Tanroads Mkoa wa Mara imetoa kauli hiyo kufuatia baadhi wa wananchi wa mkoa wa Mara ambao walikubali kubomoa nyumba zao zilizokuwa zimewekewa alama ya X kutaka fidia ama kujengewa nyumba hizo kutokana na tamko la Pinda kuwa zoezi hilo limesitishwa na kwamba suala hilo litawasilishwa katika Baraza la Mawaziri. Meneja wa Tanroads Mkoa wa Mara, Emmanuel Korosso, alisisitiza kuwa hakuna fidia yoyote itakayolipwa kwa watu waliobomolewa ama kubomoa wenyewe nyumba zao zilizokuwa katika hifadhi ya barabara na kwamba Tanroads wataendelea kusimamia sheria.
“Tunasema hakuna mtu wa kulipwa fidia kwani kama Tanroads Mara hatujapata maelekezo yoyote kutoka makao makuu ya Tanroads, Wizara ya Ujenzi ama ofisi yoyote ya serikali inayotuzuia kutekeleza sheria hiyo.
“Mimi nimesoma tu katika vyombo vya habari kuhusu agizo la Waziri Mkuu hivyo hainifanyi niache kutekeleza wajibu wangu,” alisema Korosso. Alisema tayari kuna baadhi ya barabara zilizotangazwa na kupata wakandasi na si rahisi kusitisha mikataba kwa kushindwa kusimamia sheria hiyo kwa kuwataka wananchi kuondoa nyumba ama vibanda walivyojenga ndani ya hifadhi ya barabara.
“Kwa mfano hii mikataba tuliongia na baadhi ya kampuni kwa ajili ya ujenzi ama upanuzi wa barabara sasa na sisi tusitishe kwa vile wananchi wameambiwa wasitoke ndani ya hifadhi ya barabara, ndugu yangu sijapata maelekezo yoyote kuhusu hilo, bali ninachojua mimi kwa sasa nasimamia sheria,” alisisitiza.
Tayari zaidi ya nyumba na vibanda 1,000 mkoani Mara na wilaya jirani ya Magu zimewekewa alama za X.
Pinda alishawatumia waraka wakuu wote wa mikoa kuaeleza uamuzi wa kusitishwa kwa bomoa bomoa. Mkuu wa Mkoa wa Mara, Enos Mfuru, hakupatikana kuzungumzia suala hilo kwa kuwa yuko nje ya nchi kikazi.
Katibu Tawala wa Mkoa, Clement Lujaji, alisema alikuwa Dar es Salaam kikazi, lakini wakati anaondoka Musoma waraka huo haukuwahi kupokelewa na kumtaka mwandishi kuwasiliana na msaidizi wake, Mwanga Exaud.
Hata hivyo, Exaud alisema Mkoa wa Mara haujapokea waraka huo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu.
CHANZO: NIPASHE

No comments: