.jpg)
Mshambuliaji tegemeo wa timu ya soka ya vijana ya umri chini ya miaka 23 ya Tanzania, Thomas Ulimwengu anatarajiwa kuondoka jijini hapa leo Jumanne na kuelekea Cameroon kuungana na yosso wenzake kwa ajili ya kucheza mechi ya kutafuta tiketi ya kucheza fainali za Olimpiki zitakazofanyika mwakani nchini Uingereza.
Ulimwengu yupo jijini hapa katika klabu ya TP Mazembe akifanyiwa majaribio ya kucheza soka la kulipwa baada ya kuwavutia makocha wa timu hiyo.
Akizungumza na gazeti hili jana, Ulimwengu alisema kuwa anaendelea vizuri na majaribio yake na anaamini kwa kiasi kikubwa ameonyesha uwezo.
Ulimwengu alisema kuwa amefanya kila alichokuwa anaambiwa na kwa ufanisi mkubwa na amekuwa mwepesi kutokana na kupata uzoefu alipokuwa kwenye timu ya vijana ya umri chini ya miaka 17 na timu ya taifa, Taifa Stars.
"Niko vizuri na naendelea na mazoezi kama walivyonipangia, nashukuru nimepata ruhusa ya kwenda kuitumikia timu ya taifa, naamini tutafanya vizuri huko Cameroon," alisema Ulimwengu ambaye alikuwa analelewa na kituo cha Tanzania Soccer Academy kabla ya kwenda Sweden katika kituo kingine cha ABC chini ya wakala wake, Damas Ndumbaro.
Ulimwengu alikuja jijini hapa mapema mwezi huu na majaribio yake yalipangwa kukamilika Aprili Mosi lakini Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lilieleza kwamba lilikuwa na mpango wa kumuombea ruhusa chipukizi huyo kujiunga na wenzake na baadaye kurejea Lubumbashi kuendelea na mazoezi.
Timu hiyo ya vijana inayofundishwa na Jamhuri Kihwelu, 'Julio', itavaana na Cameroon katika jiji la Yaounde Machi 27 na baada ya wiki mbili watarejeana Dar es Salaam.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment