
Inaelezwa kuwa wivu ni muhimu kwenye mapenzi huku wataalam wa masuala ya uhusiano wakitafsiri kama mguso wa ndani unaopima kiwango cha juu cha kujali na kujitolea alichofikia mtu kwa mwenzake. Kwa maana nyingine mapenzi ni wivu na wivu ni mapenzi.
Hata hivyo, ushirikiano wa wivu na mapenzi hutegemea pande mbili zenye sura tofauti ambazo kwa kujifunza tunaweza kuzifananisha na mboga inayohitaji chumvi ili iwe na ladha. Hii ina maana kwamba chumvi (wivu) peke yake hailiki lakini pia mboga (penzi) iliyozidi chumvi haipendezi kwa chakula.
Watu wengi siku hizi wanakosea sana kujikita kwenye wivu, jambo linalowafikisha mahali pa kuyafanya mapenzi yao yazidiwe sana na chumvi na hivyo kutopendeza kwa chakula. Hebu tujifunze kwa ufupi madhara saba ya wivu.
KUSINGIZIA
Mtu mwenye wivu mkali huwa na tabia za kusingizia. Unaweza kukuta mpenzi wake amechelewa kurudi nyumbani kwa sababu ya foleni au majukumu kazini lakini akirejea anahisiwa alipitia nyumba ndogo. Hisia hizi huvunja moyo sana na kwa kiwango kikubwa huondoa upendo na pengine humfanya mtuhumiwa kutoona umuhimu wa kujiheshimu, heshima ambayo haithaminiwi.
KUJIHADAA
Kuwa na wivu sana kunaweza kukufanya ukatafsiri tofauti matendo mengi ya mpenzi wako. Kwa mfano, mpenzi wako anaweza kukujibu vibaya kwa kasoro za ubinadamu lakini wewe ukatafsiri amefanya hivyo kwa sababu amepata mwingine. Kujihadaa au kujidanganya kwenye mawazo yako utajifikisha mahali pa kujiona hufai na hivyo kuamua aidha kuachana na mpenzi wako au na wewe kufanya vituko ambavyo mwishowe vitakufikisha pabaya.
KUJIDHOOFISHA
Mapenzi siku zote yanahitaji uhodari wa kutenda, kuamua, kuvumilia, kukabiliana na changamoto na wakati mwingine maono ya mbali. Mtu mwenye wivu mkali hawezi kuwa mvumilivu, muda wote hujiona mnyonge asiyejua hatima yake kimapenzi itakuwaje. Mambo mengi atakayokuwa anawaza kifamilia yatakuwa chini ya kiwango na pengine ya muda mfupi na hivyo kujikuta akipoteza sifa ya kuwa mpenzi bora.
KUTOTOSHEKA
Historia inaonesha kuwa watu wenye hisia za kusalitiwa na wivu wa kupita kiasi huwa hawatosheki. Wakipewa kila siku nyama, huwaza kupata zaidi ya hapo na sababu wanazojipatia ni: “Kama mume wangu amefanikiwa kuleta nyama kila siku, asingekuwa na nyumba ndogo ningekula kuku.” “Mke wangu anashindwa kunipa haki yangu kwa sababu anatoka nje ya ndoa.” Mwenye wivu siku zote hatatosheka na anachopewa.
KUJENGA UADUI
Mwenye wivu wa kupindukia hawezi kuishi na jamii kwa amani, anakuwa na maadui wengi sana mtaani kwake na kazini kisa wivu. “Yule uliyekuwa unaongea naye ni nani? Siku nikimkuta hapa nitampiga!” Wivu huongeza maadui kwenye jamii unayoishi jambo ambalo halipendezi.
KUJITIA KITANZI
Ukichunguza kwa makini, wapenzi wenye wivu na hisia za kusalitiwa mara nyingi wao ndiyo hufumaniwa. Hii inatokana na ukweli kwamba kuishi muda mwingi na wivu kutakufikisha mahali ambako utasema, ngoja na mimi nianze! Kuanza kwenye lengo la kulipa kisasi huwapeleka wahusika kwenye mafumanizi na kuambulia aibu mbele ya jamii.
KUJIHUZUNISHA
Kuishi maisha yaliyotawaliwa na wivu mkali ni kujihuzunisha kusikokuwa na sababu. Ulimwengu wa leo ni wa mawasiliano na umoja zaidi. Wanawake na wanaume kushirikiana kazini na nyumbani kwa lengo la kujenga taifa ni jambo muhimu sana. Hivyo, kuwa na mke ambaye hutaki ashirikiane na wanaume kisa wivu ni kujihuzunisha bure. Wivu ukizidi una madhara kwa afya na ustawi wako na familia yako.
No comments:
Post a Comment