ANGALIA LIVE NEWS

Friday, March 25, 2011

Uvumilivu, unyenyekevu sifa zinazowashinda wengi

HAKIKA nina furaha sana moyoni mwangu kupata kibali cha kukutana tena siku hii ya leo. Rafiki zangu, naamini mtakuwa wazima wa afya njema na mpo tayari kupata kile nilichowaandalia wiki hii.

Rafiki zangu, je tayari umeshanunua kitabu changu cha Let’s Talk About Love? Kama bado, nenda ukanunue sasa. Ni kitabu kizuri sana kilichokusanya mada za mapenzi pamoja na Love Messages kali kwa ajili ya kumtumia mpenzi wako.


Kabla ya kuingia katika sehemu ya mwisho ya mada yetu iliyoanza wiki iliyopita, nitawapa stori kidogo juu ya mada hiyo. Ukweli ni kwamba mada hii ilichangiwa na wasomaji wengi sana. Kati yao, wapo waliouliza maswali wakitaka ufafanuzi wa mambo fulani yanayowatatiza.

Ni wengi sana, siyo rahisi kuandika maelezo ya wote, lakini kwa uchache nitachapa baadhi ya meseji ambazo naamini zitakufundisha kitu fulani kipya. Hebu tuone.

MSOMAJI WA KWANZA:
Nashukuru kwa mada nzuri kaka Shaluwa. Hongera sana, kwani umekuwa ukisaidia ndoa nyingi kuwa imara. Uvumilivu unawashinda wengi sana katika ndoa zao; baadhi wanadhani ni kama utumwa fulani hivi, jambo ambalo siyo la kweli.

Kumvumilia mwenzi wako ndiyo msingi wa ndoa, ndiyo maana ndoa inapofungwa mahali popote pale, suala la uvumilivu hutajwa kama kiungo cha ndoa hiyo. Nashukuru sana kaka Shaluwa.
Anneth, Tabora.

MSOMAJI WA PILI:
Kwa miaka yote 22 niliyopo kwenye ndoa yangu na mke wangu, uvumilivu tu ndiyo naweza kusema umetudumisha. Mimi nina miaka 49 sasa, mke wangu ana miaka 43, lakini tunavyoishi utadhani tumeoana mwezi uliopita.

Mdogo wangu Joseph, mimi nakupa pongezi na uendelee na moyo huo huo kusaidia jamii, maana ni kweli kwamba unajenga ndoa za wengi. Nakupongeza sana Jose.
Julius Kimario, Iringa.

MSOMAJI WA TATU:
Mimi ni msichana mwenye umri wa miaka 27, sijaolewa lakini nina mchumba. Niseme ukweli kwamba, nimejitahidi sana kumvumilia huyu mwanaume kwa kila kitu, lakini sasa naona anataka kuvuka mikapa.

Huyu bwana analalamika sana, siku hizi ameanza mchezo wa kuniomba ‘mlango wa pili’, yaani analalamika sana, anasema eti amesikia rafiki zake wakisema kwamba, wapenzi wakijaribu mchezo huo, eti hawataachana.

Naumia zaidi maana huyu mwanaume nipo naye kwa miaka mitatu sasa, matarajio yetu ni ndoa, lakini ndiyo hivyo tena, tangu ameibuka na hayo mambo yake amenikatisha tamaa sana. Naomba unisaidie kaka yangu, maana nahofia hata umri wangu nao unasonga sana!
Mwathirika, Arusha.

SHALUWA ANAJIBU:
Meseji yako nimeipata vizuri ingawa imekuwa ya kuunga-unga kutokana na urefu wake. Kwanza kabisa, ondoa hiyo dhana kichwani mwako kwamba, eti una miaka 27, unahofia kupata mume! Hiyo ni fikra mbaya sana.

Ndoa ni agano, halafu mume mwema anatoka kwa Mungu mwenyewe. Huo ndiyo ukweli. Huna sababu ya kukimbilia kwenye ndoa ambayo itakusababishia matatizo hapo baadaye. Mwanaume wa kweli ambaye ana nia ya dhati ya kukuoa na anapenda maisha yako, hawezi kutaka kufanya mchezo mchafu kama huo.

Kifupi kauli yake hiyo ni kielelezo tosha kwamba anakudharau na anakuona kama ‘kipumzikio’ chake na si mwanamke wa maisha yake ya ndoa. Hapo unapaswa kutulia na kufanya maamuzi sahihi kwa ajili ya maisha yako.

Juu ya yote hayo, huyo mwanaume hana mapenzi ya kweli kwako, isitoshe huo mchezo inaonekana ameshakuwa mzoefu wa muda mrefu, hivyo anataka kukuharibu na wewe kama alivyofanya kwa wengine.

Hakuna ukweli wowote, kwamba eti kufanya upuuzi huo kuna uhusiano wowote na kuzidisha penzi. Hilo jambo halipo. Bila shaka ukifanyia kazi maelezo haya, utaamua cha kufanya.

Rafiki zangu, hayo ndiyo baadhi ya mambo niliyokutana nayo wiki iliyopita, ni mada iliyokuwa na changamoto sana. Sasa tumalizie somo letu; kipengele cha mwisho ni unyenyekevu baada ya kuanza na uvumilivu wiki iliyopita.

VIPI KUHUSU UNYENYEKEVU?
Hapa panajieleza penyewe; lazima umnyenyekee mpenzi wako, usijidanganye kwamba kumnyenyekea mpenzi wako ni utumwa, hizo ni fikra mgando. Sasa kama usipomnyenyekea laazizi wako, ambaye mwenyewe ulikubali kuwa naye na kufunga naye ndoa unataka umnyenyekee nani?

Mumeo/mkeo ndiyo wa kumnyenyekea siku zote za uhai wako. Lazima uwe na kauli ya upole iliyojaa ukarimu. Ndoa kubembelezana bwana, mpenzio akija na mawazo yake, mtu amemuudhi kazini, kwako ndiyo mahali haswa anapopaswa kunyenyekewa na kupewa raha.

Wewe ndiye unapaswa kumsahaulisha kabisa mambo yote yaliyotokea kazini.  Mpokee kwa upole, mwambie pole, mkaribishe chumbani kisha mvue nguo zake na umpeleke bafuni mwenyewe. Anza kumwogesha bila kuzungumza naye maneno mengi. Tumia dodoki au kitambaa laini kumsafisha ngozi ya mwili wake.

Baada ya hapo mkaushe kwa taulo laini kisha mrudishe chumbani, mtolee nguo za usiku kisha mpeleke mezani kwa chakula. Baada ya hapo sasa mkiwa sebuleni mnaangalia runinga mwulize kwa upole huku macho yakiwa yanazungumzia mapenzi:

“Darling vipi? Mbona leo naona siyo kawaida yako? Umechoka-choka...kuna nini mpenzi wangu jamani?” Amini nakuambia kwa kauli kama hiyo hata kama alikuwa na tatizo kubwa atakujibu: “Ah! Kuna mtu aliniudhi kidogo ofisini, lakini baada ya kufika hapa nyumbani najisikia amani sasa.”

Dada zangu, uhai wa ndoa yako, upo mikononi mwako mwenyewe. Nashukuru kwa kunisoma, naomba niishie hapa kwa leo. Kama una tatizo linakusumbua, wasiliana nami kwa njia ya simu nikusaidie.
HADI WIKI IJAYO.

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi ambaye anaandikia magazeti ya Global Publishers, ameandika vitabu vya True Love, Secret Love na Let’s Talk About Love.

No comments: