ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, March 26, 2011

Viroja usafiri wa meli Ziwa Victoria

Sheilla Sezzy, Mwanza
 NI majira ya saa 2.30 usiku nipo katikati ya jiji la Mwanza. King’ora kinalia katika Bandari ya Mwanza, Kaskazini na hapo naona magari, pikipiki na watembea kwa miguu wakiwa katika mwendo unaoashiria haraka, kuelekea bandarini.
Sishangazwi na hali hii kwani kwa sisi wakazi wa jiji hili la Mwanza tumeshakijua king’ora cha meli hii ya mv Victoria ambacho mlio wake husikika sehemu kubwa ya jiji hili, hasa pale inapokaribia kung’oa nanga tayari kuanza safari ya kuelekea Bukoba, mkoani Kagera.

Hivyo kwa haraka nami nikiwa karibu na bandari niliingia eneo hilo, kisha nikaruhusiwa kupanda melini baada ya wakaguzi wa tiketi kuridhika kwamba nilikuwa na tiketi halali kwa ajili ya kwenda Bukoba. Niliingia sehemu wanayoketi abiria wa daraja la tatu, nikatulia huku nikiwa nimeukunyata mkoba wangu ambao ulikuwa na vitu vichache. Ilipotimu majira ya saa 2.58 hivi usiku, king’ora cha pili kililia na hapo taratibu meli ikaanza kung’oa nanga na kuanza safari.


Usafiri wa meli Usafiri wa meli kati ya Mikoa ya Mwanza na Kagera umekuwa ndiyo unaotegemewa zaidi hivyo kuwa na historia ndefu. Lakini kadri miaka inavyozidi kusonga, utamaduni huu unafifia. Meli si rafiki tena wa wasafiri wa Mwanza – Bukoba. Hii ni kutokana na kuwapo kwa mabasi ambayo yanatoa huduma ya usafiri wa kila siku kati ya mikoa hii miwili.  Idadi kubwa ya wasafiri wa meli enzi hizo, walitoa fursa kwa wafanyabiasha kununua tiketi kwa wingi katika ofisi za lililokuwa Shirika la Reli Tanzania (TRC), kisha kuziuza kwa bei ya kuruka.

Wananchi waliumizwa kwani ilikuwa ikifika wakati tiketi hizo ziliuzwa maradufu ya bei halali. Biashara hiyo haikuishia kwenye tiketi tu, ndani ya meli, wanyabiashara walipata mwanya wa kuuza vitu mbalimbali vikiwemo vyakula licha ya kwamba melini kuna mgahawa ambao hutumika kutoa huduma hiyo. Kwa ujumla, usafiri wa meli ulikuwa ni wa aina yake kiasi kwamba umaarufu wake uliongezeka siku hadi siku, katika mikoa karibu yote ya kanda ya ziwa.

 Mv Victoria Mv Victoria ni meli kongwe ambayo imefanya safari zake katika Ziwa Victoria kwa zaidi ya miaka 40 sasa. Meli hii ina uwezo wa kubeba abiria 1,200 na  magari sita yenye uzito wa tani tano kila moja. Hata hivyo, hivi sasa inachuka magari ya tani 1.5 kutokana na ‘winch’ au ‘crane’ ya kunyanyulia magari kwa ajili ya kuyapakia kwenye meli hiyo kupungua uwezo wake wa kufanya kazi. Mbali na magari pamoja na abiria, meli hiyo ina uwezo wa kubeba tani 200 za mizigo mbalimbali. Mara nyingi bidhaa mbalimbali hupakiwa jijini Mwanza kwenda Kagera kwa ajili ya kuwawezesha wakazi wa huko kupata mahitaji yao muhimu lakini pia Mkoa wa Kagera husafirisha ndizi kwa wingi kwenda jijini Mwanza.

 Madaraja kwa abiria Ndani ya meli kuna madaraja tofauti ya wasafiri. Daraja la juu kabisa ni la kwanza. Katika daraja hili, abiria hupata vyumba vya kulala. Vyumba hivi idadi yake ni 19 na kila chumba kina vitanda viwili.

 Kwa maana hiyo, kati ya wasafiri 1,200 ni abiria 38 tu wanaoweza kupata nafasi katika daraja hili. Kwa viwango vya sasa vya nauli, msafiri wa daraja la kwanza ni Sh30,600. Daraja la pili pia linatoa nafasi kwa abiria wake kulala na wengine kukaa. Katika daraja la pili, abiria wanaoweza kulala ni 60 katika vyumba 10 ambavyo kila kimoja kina vitanda sita. Nauli ya daraja la pili kulala kwa sasa ni Sh20,600.

Katika sehemu ya kukaa ya daraja hili la pili, abiria wanapata fursa ya kukaa kwenye viti vya sofa. Hapa kuna abiria 130 na nauli yake kati ya Bukoba na Mwanza ni Sh17,100 kwa sasa.  Daraja la mwisho kabisa ni daraja la tatu. Hili ndilo kimbilio la wengi. Katika daraja la tatu kuna idadi kubwa ya abiria tofauti na madaraja mengine. Pia nauli yake ni tofauti. Daraja hili linabeba abiria 972. Katika vyumba viwili vya daraja la tatu kuna mabenchi ambayo yametengwa katika sehemu ndogo ndogo zinazoruhusu kukaliwa na mtu mmoja mmoja. Daraja la tatu hakuna vitanda vya kulala. Nauli ya ‘kukesha’ katika sehemu hii ni Sh12,000.

  Ndani ya daraja la tatu   Kuna maisha tofauti ndani ya meli. Kama tunavyojua katika maisha ya kawaida, ni vigumu mtu kuuzuia usingizi. Hali hii huwaweka katika wakati mgumu abiria wanao safiri katika daraja la tatu. Hufika wakati wakataka kupumzika kutoka na uchovu wa safari na pengine mambo mengine kadha wa kadha. Wengi wa abiria hawa hulazimika kulala chini ya viti na wengine juu katika sehemu za kuwekea mizigo.

Kutoka na hali hii wapo abiria ambao huamua kuingia melini wakiwa na mikeka na hata vipande vya magodoro. Abiria wa aina hii mara nyingi huwahi kuingia melini ili kuwahi nafasi ya kulala, iwe ni chini ya kiti ama katika sehemu za kuwekea mizigo baada ya kuwa wametanguliza mikeka yao au vipande vya magodoro. Katika hali hii, baadhi ya abiria hupata fursa ya  kufahamiana na wenzao na kuanzisha uhusiano wa kimazungumzo hivyo kuufanya usiku wa safari kuwa mfupi kwao.

 Biashara melini Tofauti na baishara za vyakula na vinywaji, zipo ‘biashara’ nyingine ambazo hufanyika melini. Moja ya biashara hizo ni uuzaji wa vyumba vya kulala ambao hufanywa na wafanyakazi wa meli. Wanaouziwa vyumba au vitanda hivi wako katika makundi mawili.  Kwanza ni wale ambao huingia melini kinyemela wakiwa wamekosa tiketi na pili ni wale ambao huzidiwa na usingizi hivyo kuamua kutafuta mahali pa kupumzika. Kitanda kimoja melini kinauzwa kati ya Sh8,000 na Sh10,000.

Biashara nyingine ni ile ya vipande vya magodoro. Biashara hii pia hufanywa na wafanyakazi wa ndani meli wakiwalenga abiria wa daraja la pili kukaa na lile la tatu.  Abiria hukodi kipande cha godoro na kukitumia usiku huo kwa kutandika chini ya kiti, kisha hukirejesha asubuhi kwa mhusika. Bei ya biashara hii ni makubaliano.

 Senene wamo Biashara ya senene pia imeshamiri ndani ya meli. Mkazi mmoja wa Bukoba, Said Juma anasema amefanya biashara hiyo kwa miaka mitatu na amepata mafanikio makubwa. Anasema atakuwa mmoja kati ya watu ambao wataathirika kama meli hiyo haitafanya kazi kwa kuwa wateja wake wengi ni wasafiri. Huanza kuuza senene mara tu meli inapong’oa nanga katika Bandari ya Bukoba na husafiri nayo hadi katika mji mdogo wa Kemondo ambako hutia nanga kupakia abiria, pamoja na mizigo hususan ndizi.

Hapo huwa ndiyo mwisho wa safari yake lakini anakuwa ameitumia vyema safari hii ya takriban saa moja kufanya biashara yake. Baada ya hapo huteremka na kurejea mjini Bukoba kwa gari, safari ambayo humchukua dakika 20 tu.
 Hali ya usafi   Hali usafi katika meli inategemea wingi wa abiria. Wanapokuwa wengi hali huwa si nzuri tofauti na wanapokuwa wachache. Kila daraja lina maliwato yake. Hata hivyo, abiria wa daraja la tatu hulazimika kwenda kutimiza haja zao katika maliwato za daraja la pili kutokana na hali mbaya iliyopo katika vyoo vya daraja la tatu.

Hatma ya usafiri wa meli  Meneja Masoko wa Shirika linaloendesha huduma za meli hiyo, Herry Kajenge anasema uwepo wa mabasi yanayotoa huduma za usafishaji kati ya Mwanza na Kagera siyo kikwazo kwao kwani bado kuna abiria wengi wanaosafiri kwa meli. Licha ya kukiri kuwepo kwa ushindani kutokana na kuwepo kwa mabasi hayo, anasema bado meli yao inapata abiria wengi kuliko mabasi.

Anasema idadi ya abiria wa meli wanafikia 500 na kwamba mabasi yaliyopo yanasafirisha abiria 450. “Hii bado ni idadi nzuri pamoja na ushindani huo. Tunawafuatilia kwa karibu washindani wetu kitu ambacho tumegundua ni kwamba hawakidhi viwango na hata hiyo idadi ya watu waliyonayo siyo wote ambao wanawapata na kuwasafirisha,” alisema Kajenge.

Anasema kuna baadhi ya wafanyakazi wao ambao wanakiuka taratibu ndani meli ikiwa ni pamoja na kufanya biashara ya vitanda na vyumba akisema wamekuwa wakifuatilia na kuchukua hatua

No comments: