ANGALIA LIVE NEWS

Friday, March 25, 2011

‘Wajanja’ wazalisha pombe kali bandia

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Cyrill Chami
Daniel Mjema, Moshi
HALI si shwari mkoani Kilimanjaro baada ya kuwapo kwa madai ya kuzagaa kwa pombe kali zilizo chini ya kiwango hali iliyomlazimu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Cyrill Chami kuagiza kuchukuliwa kwa sampuli zake.

Mkazi mmoja wa Moshi, Beda Massawe alidai kuwa mtandao unaochakachua pombe hizo ni mpana kama ulivyo ule wa gaidi wa kimataifa, Osama Bin Laden anayesakwa kwa udi na uvumba na mataifa ya nchi za Magharibi.

Kutokana na agizo hilo la Dk Chami alilolitoa juzi, tayari maofisa kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS), jana walifanya operesheni ya kushtukiza mkoani Kilimanjaro na kuchukua sampuli ya pombe zinazolalamikiwa kwa ajili ya kuzipima.

Wananchi waliohojiwa na timu hiyo ya wataalamu kutoka TBS, wamedai kuwa pombe hizo feki, zimekuwa zikizalishwa kwa siri na viwanda bubu mkoani humo na kujazwa kwenye chupa halisi za vinywaji hivyo.

Hatua hiyo ya TBS imekuja wakati madaktari wakitahadharisha kuongezeka kwa magonjwa ya ini na macho kupungua nguvu ya kuona kunakosababishwa na kunywa pombe hizo kali za bandia.

“Nimeshawaagiza TBS wachukue hatua za haraka kuja Kilimanjaro kuchunguza jambo hilo la hatari kwa afya ya wananchi na kwa kweli baada ya vipimo vya maabara tutachukua hatua kali na madhubuti,” alisema Dk Chami.

Akizungumza na Waandishi wa habari jana baada ya kuchukua sampuli za pombe hizo, Ofisa Mwandamizi anayeshughulikia Uthibiti wa Ubora wa TBS, Lazaro Msasalaga alisema majibu ya uchunguzi huo yatatolewa haraka iwezekanavyo.

“Wateja wakinywa pombe hizi kali zikiwa zimechanganywa na methanol wanapata shida ya kuona. Lakini athari kubwa zaidi ya pombe hizi zisizo na ubora ni kwenye figo na ini,” alisema Msasalaga.

Pombe ambazo sampuli zake zilichukuliwa ni Gordon’s, John Walker na Grants zinazozalishwa nje ya nchi na kuingizwa nchini lakini, inadaiwa ‘wajanja’ hapa nchini wamezichakachua.

Meneja uhusiano wa TBS, Roida Andusamilie aliwaomba wananchi wenye taarifa sahihi za mahali vilipo viwanda bubu vinavyodaiwa kutengeneza pombe hizo kutoa ushirikiano kwa mamlaka hiyo ili wahusika watiwe mbaroni.

Mfanyabiashara mashuhuri wa mjini Moshi anayemiliki klabu ya usiku na mgahawa wa Chrisburger, Chriss Shayo alishangazwa na mtandao unaochakachua pombe hizo kufanikiwa kubandika stika za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
 
Shayo alidai kuwa kubandikwa kwa stika hizo za TRA kwenye chupa hizo zenye pombe feki, kunawafanya wananchi waamini kuwa zimepitia mamlaka halali wakati pombe hizo ni mwitu zilizozalishwa uchochoroni na kujazwa kwenye chupa.

“Tatizo unapokwenda kuzinunua huwezi kugundua kama ni feki kwa sababu ziko kwenye chupa original (halisi) lakini, unapokuja kuifungua na kumuuzia mteja, ndipo analalamika kuwa siyo yenyewe na tunalazimika kumwaga,” alisema Shayo.
 
Hata hivyo, Meneja wa TRA Mkoa wa Kilimanjaro, Patience Minga alipohojiwa na Mwananchi jana kuhusu stika hizo, alidai kuwa wafanyabiashara hao huzinunua makao makuu ya TRA baada ya kujisajili kuwa waagizaji wa pombe kali na wine.

Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika Mashariki wa kampuni ya Tecno Group ya Italy, Chriss Martin aliwaambia maofisa hao wa TBS kuwa pombe hizo zilizochakachuliwa, zimekuwa na ladha ya mafuta ya taa na muonjo tofauti na pombe halisi.

“Hii ni syndicate (mtandao) mkubwa na tunashukuru TBS mmekuja maana hili si tatizo la leo, lina muda mrefu sana hapa Moshi na ni vyema mkatumia vyombo vyenu kuwabaini hawa wahujumu uchumi,” alisema Martin.

Meneja wa Baa ya Changbay Annex, Hellen Shayo aliwaambia maofisa hao kuwa kati ya chupa tano za pombe hizo kali wanazonunua, moja au mbili hubainika kuwa si halisi jambo ambalo limekuwa likiwatia hasara.


CHANZO:MWANANCHI

No comments: