ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, April 20, 2011

Jamii Forum yakanusha kutumiwa na Chadema

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Pius Msekwa
Mtandao wa Kijamii wa Jamii Forums, umekanusha madai yaliyotolewa na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Pius Msekwa, kuwa umeanzishwa na vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kwamba unatumiwa na chama hicho katika harakati zake za  kisiasa hapa nchini.



Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jamii Forums, unafanya kazi kwa kujitegemea na kwamba haumilikiwi na chama chochote cha kisiasa wala kufadhiliwa na Chadema kama alivyodai Msekwa.
Taarifa hiyo ilisema Msekwa alitoa madai hayo wiki iliyopita wakati akitambulisha Sekretarieti mpya ya CCM mjini Dodoma ambapo alitumia muda wake kushutumu mtandao huo.
Mtandao huo ulisema kwa sasa una wanachama 40,000 waliojiandikisha na kwamba unafanya kazi kama chanzo huru cha habari bila kutumiwa na mtu wala chama chochote cha siasa.
Shutuma hizo za Msekwa zilitolewa Aprili 14, mwaka huu mjini Dodoma ambapo pia mwanasiasa huyo alisema mtandao huo ulichangia kukikosesha kura CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
Taarifa hiyo iliongeza kwamba shutuma zinazotolewa dhidi yao kwamba unatumika kuivuruga CCM na serikali yake sio za kweli na kwamba zinalenga kuukwamisha mtandao huo katika harakati zake za kuielimisha jamii na kuipasha habari.
Mtandao huo ulisema CCM unawaandama kutokana na wao kuwa mstari wa mbele katika kupiga vita vitendo vya rushwa ambavyo hivi karibuni vimekichafua chama hicho na serikali yake.
Shutuma hizo zimewasababishia usumbufu kutoka kwa wanachama wao walioenea kona zote za nchi na nje ya nchi na kwamba hatua hiyo ya CCM ni ishara kuwa kimeanza kuuogopa mtandao huo.
CHANZO: NIPASHE

No comments: