ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, April 6, 2011

Mambo ya kuzingatia katika penzi jipya

MARAFIKI zangu, ni imani yangu kwamba ni wazima wa afya njema na mnaendelea na majukumu yenu ya kila siku kama kawaida. Kwa upande wangu nipo salama kabisa.

Ikiwa una matatizo ya uhusiano au unahitaji kupanua zaidi uelewa wako katika ulimwengu huu wa mapenzi, kitabu changu kipya cha Let’s Talk About Love ni dawa tosha kwako, nenda kakinunue sasa, kinapatikana mitaani.


Baada ya hayo, sasa tugeukie katika mada yetu ya leo, kama inavyosomeka hapo juu. Leo nazungumzia juu ya mambo muhimu ambayo yanapaswa kuzingatiwa na wapenzi wanaoingia katika penzi jipya. Yes… Namaanisha kwamba, mambo ambayo unayopaswa kuyafanya na yale usiyopaswa kuyafanya!

Inawezekana ulikuwa unamsaka mwenzi wako kwa muda mrefu,lakini baada ya kumpata na kutokujua unaweza kufanya mambo ambayo badala ya kuboresha uhusiano wako, ukajikuta ukiharibu  kila kitu!
Kama umeshampata mpenzi mpya, kitu kikubwa kinachotakiwa kuwa mbele ya fikra zako ni mambo gani muhimu ambayo unapaswa kumfanyia ili aweze kuamini kuwa unampenda?

Jambo la kwanza ambalo unapaswa kuzingatia ni kumhakikishia kwa mdomo na hisia kuwa unampenda, hata hivyo kumpenda huko kusiiishie kinywani pekee, bali hata matendo yako yanatakiwa yadhihirishe kile unachozungumza.

Ili aweze kuamini kuwa ni kweli unampenda kwa mapenzi ya kweli, kingine unachopaswa kufanya ni kuwa naye karibu kila wakati kwa njia ya mawasialiano. Unapaswa kuwasiliana naye pale unapokuwa kazini au hata yeye anapokuwa katika shughuli zake.

Ukifanya hivyo, ataamini kuwa unampenda ndiyo maana kila wakati unamkumbuka. Unaweza ukampigia simu mchana ukamwambia; “Nakupenda sana mpenzi wangu, nashindwa kufanya kazi kutokana na ‘kukumisi’ kwa muda mrefu, angalau sasa nimeisikia sauti yako, naweza kufanya kazi kwa ufanisi,” ni maneno machache lakini yaliyobeba maana kubwa sana katika uhusiano wenu.

Baadhi ya marafiki zangu, huwa wana haraka ya kukimbilia kufanya ngono, acha nikuambie ukweli, kufanya ngono siyo mapenzi. Siku hizi hata wanawake wamekuwa wajanja sana,ukiwasumbua kuhusu kufanya tendo hilo mapema, wanajua kuwa huna mapenzi ya dhati kwao, hivyo wanakosa imani na wewe na kutoa nafasi ndogo ya kuendelea na uhusiano huo.

Usiwe na haraka rafiki yangu, kama kweli unampenda hutakiwi kuwa na haraka, subiri kwanza mpaka uhusiano wenu utakapokomaa ndiyo uanze kuzungumzia suala la mapenzi.

Katika hali ya kawaida, msichana anaweza akaamini kuwa ulimtamani ili ufanye naye mapenzi badala la kumwingiza katika mapenzi ya moja kwa moja yatakayowaingiza katika ndoa takatifu, usikubali mpenzi wako akawa na hisia mbaya na wewe mapema, ni vizuri zaidi kama utajitahidi kumfanyia mambo ambayo yatamfanya akuamini kuwa ni mkweli na mwenye mapenzi ya dhati kwake na huna lengo la kumchezea.

Siyo vibaya kama mtatenga siku moja kwa wiki kukutana na kuzungumza mambo mbalimbali ya maendeleo katika penzi lenu ambalo kimsingi bado ni changa!
Toka naye ‘out’, kisha zungumza kwa furaha, mnaweza mkacheza michezo mbalimbali mkiwa ufukweni kama vile kukimbizana, kuogelea na mengine mingi, lakini kamwe msihusishe na mambo ya ngono mapema.

Kuanza uhusiano siyo kazi kubwa, kazi ni kuujenga uhusiano huo na kuwafanya kila mmmoja wenu asiwe na raha pale asipomuona mwenza wake kwa wakati mmoja.

Lakini kazi nyingine kubwa ambayo itakuwa mbele yako ni jinsi ya kuweza kudumisha uhusiano huo kwa mpenzi wako na kuonesha nia yako ya dhati kwake kiasi cha kukufanya uweze kuvuka kuta za moyo wake na kuingia ndani zaidi.

Kiukweli kabisa, jambo hili linawashinda wengi na kujikuta wakiwapoteza wapenzi wao kwa kuwa huwa wanasumbuliwa na tamaa za haraka za kufurahisha miili yao badala ya mioyo ya wapenzi wao.

Hakikisha  kwamba, mwanzo wa mapenzi ni muda muafaka  kwako kumuonesha mapenzi ya kweli mwenza wako, kumfariji na kumsaidia kwa hali na mali pindi akikumbwa  na matatizo, ni kati ya mambo muhimu yatayomfanya aamini kuwa ni kweli una mapenzi ya dhati na siyo tamaa ya ngono kwake.

Jitahidi uwe mshauri wake mkuu, kama ana tabia ambazo unadhani siyo njema, ni vizuri ukamshauri na kumweleza kwa kina madhara ya jambo ambalo anataka kufanya, ili aepukane nalo. Kama utakuwa na hoja za kutosha anaweza akabadilisha maamuzi mabaya ambayo alitarajia kuyafanya hapo kabla.

Jitahidi pia kumtumia zawadi za aina mbalimbali, kadi, nguo za ndani na vitu vingine vyenye mvuto wa kimapenzi, nakuhakikishia ikiwa utamfanyia hayo, lazima uhusiano wenu utadumu. Mfanye kuwa mshauri wako mkuu katika mambo yako ya msingi.

Pia, kabla hujafanya jambo lolote, mwite kisha zungumza naye kuhusu mawazo na mipango yako huku ukihitaji naye akuambie anachofikiria  katika mtima wake kabla ya wewe kufanya mambo hayo.
Kwa vyovyote vile, ataona kuwa unatambua thamani yake kama mwanandoa wako mtarajiwa, ndiyo maana unamwita na kumshirikisha kabla ya kufanya kitu chochote, hasa kinachohusu maendeleo ya maisha.

Rafiki zangu, naamini kuwa mnaweza kudumu na wapenzi wenu kwa muda mrefu mpaka mkafikia hatua ya ndoa kama  wote mtakuwa na nia njema.

Lakini haya yote ni baada nyie kuvuka vizingiti kadhaa ambavyo kwa njia moja ama nyingine mtaviepuka ili kuendelea kuwa bora zaidi katika uhusiano wenu.

Kwa leo naomba kuweka kituo kikubwa hapa, hadi wiki ijayo katika mada nyingine nzuri ambayo bila shaka itakuacha na mafunzo makubwa. USIKOSE!

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi ambaye anaandikia magazeti ya Global Publishers, kwa sasa ameandika vitabu vya True Love, Secret Love na Let’s Talk About Love vilivyopo mitaani. Unaweza kumtembelea katika mtandao wake; www.shaluwanew.blogspot.com

No comments: