Baba aua wanawe wawili kwa kisu
Mama naye ajeruhiwa, alazwaMwalimu wa Shule ya Sekondari Mondo, Wilaya ya Kondoa, mkoani Dodoma, Kassim Bindo (25), anatuhumiwa kuua kikatili watoto wawili wa kaka yake na kumjeruhi mama yao jijini Dar es Salaam.
Mtuhumiwa huyo ambaye anatafutwa na Polisi Mkoa wa Ilala, anadaiwa kuwaua watoto hao wa kike kwa kuwachoma kisu tumboni pamoja na kumchoma kifuani mama yao.
Bindo, ambaye ni mkazi wa Kipunguni ‘B’ Machimbo, Wilaya Ilala, jijini Dar es Salaam, anatuhumiwa kuwaua Mwanamkasi Shabani (4) na Asha Shabani mwenye umri wa siku 40.
Anatuhumiwa kufanya kitendo hicho katika eneo hilo, saa 5:30 usiku wa kuamkia jana wakati watoto hao na mama yao wakiwa wamelala nyumbani kwa babu yao, Bakari Bindo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Faustine Shilogile, alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kuongeza kuwa mtuhumiwa alitoroka muda mfupi baada ya kufanya mauaji hayo.
Kamanda Shilogile alisema Polisi wanaendelea kumsaka Kassim kutokana na mauaji hayo.
Baba mzazi wa mtuhumiwa, Bakari Bindo, aliiambia NIPASHE kuwa watoto hao walifariki dunia papo hapo, wakati mama yao, Kuruthumu Shabani (28), alijeruhiwa kwa kuchomwa kisu kifuani.
Kwa mujibu wa Bindo, mwanawe, Kassim, aliwahi kulazwa miaka ya nyuma katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wodi ya wagonjwa wa akili na kuruhusiwa baada ya wiki mbili na nusu.
Alisema kuwa miili ya marehemu hao imehifadhiwa MNH na kwamba mazishi yatafanyika leo.
Bindo alisema kuwa mazishi hayo yalipangwa kufanyika jana, lakini yaliahirishwa kutokana na baba mzazi wa watoto hao, Shabani Bakari, kuchelewa kurejea jana kutoka Morogoro anakofanya kazi.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment