ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, April 19, 2011

Serikali yasitisha safari za Loliondo kwa muda

Mussa Juma, Samunge na Filbert Rweyemamu, Arusha
SERIKALI mkoani Arusha imesitisha kwa muda safari za kwenda Samunge kwa Mchungaji Ambilikile Mwasapila kuanzia kesho hadi Aprili 25 mwaka huu.

Uamuzi huo ulitangazwa jana kwa nyakati tofauti na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Isdore Shirima na Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Elias Wali.

Shirima aliwaambia waandishi wa habari mjini Arusha kuwa hatua hiyo imefikiwa kutokana na utaratibu aliojiwekea mchungaji huyo kwamba hatatoa tiba siku za Ijumaa Kuu na Jumapili ya Pasaka.


“Mchungaji Ambilikile Mwasapila amesema hatatoa huduma ya dawa kituoni Samunge katika siku ya Ijumaa Kuu na siku ya Pasaka," alisema Shirima na kuongeza:

"Katika mazingira hayo, siku ya mwisho kuruhusu watu kutoka vituo vikuu kwenda Samunge itakuwa kesho Jumanne, Aprili 20. Watu wataruhusiwa tena kutoka vituoni hapo Aprili 25, mwaka huu."

Shirima alisema mbali na kusitishwa kwa safari hizo kwa muda, watu wanapaswa kuzingatia utaratibu wa kwenda Samunge kwa vibali ili kuondoa msongamano usiokuwa wa lazima.

Kwa upande wake, Lali aliliambia gazeti hili kuwa urefu wa foleni ya magari Samunge sasa umefikia zaidi ya kilometa 10 kutoka kwa Mchungaji Mwasapila.
 
"Mkuu wa Mkoa wa Arusha leo pia ametoa taarifa kama hii ya kuomba watu wasije kwanza ili kupisha magari yaliyopo yapewe huduma," alisema Lali.
 
Babu aomba magari yadhibitiwe
Katika hatua nyingine, Mchungaji Mwasapila ameiomba Serikali idhibiti uingiaji zaidi wa magari yanayopeleka wagonjwa kupata tiba katika Kijiji cha Samunge kutokana na foleni kuwa kubwa na kutishia maisha ya wagonjwa.
 
Akizungumza na Mwananchi jana, kwa niaba ya mchungaji huyo, Msaidizi wake, Fred Nsajile alisema kama magari yasipodhibitiwa hasa yanayotoka Kanda ya Ziwa, vifo vinaweza kutokea.

"Mchungaji anaomba ule utaratibu wa awali ufuatwe hasa kwa watu wa Bunda kwani foleni imekuwa kubwa sana na imefikia porini ambako hakuna huduma muhimu," alisema Nsajile.
 
60 wananusurika ajalini wakielekea kwa Babu
Zaidi ya watu 60 wamenusurika kufa jana alfajiri baada ya basi walilokuwa wamepanda kutoka Kondoa, mkoani Dodoma kuanguka kabla ya kufika Samunge.
 
Basi hilo lililokuwa linaendeshwa na Idrisa Ramadhani lilianguka majira ya saa 10 alfajiri likiwa linashuka katika mlima uliopo eneo la Mdito.

Baadhi ya abiria ambao wamejeruhiwa wamelazwa katika kituo cha afya cha Samunge na hakuna aliyefariki.

Wageni zaidi waongezeka Samunge
Raia wa nchini Uganda jana walianza kuingia kwa wingi Samunge, sambamba na wale wa Kenya ambao hadi jana mchana walikuwa wamefikia 2,568.

Raia wengine waliokwishafika Samunge ni wa nchi za Lebanon, Sweden, Uingereza, Zimbabwe, Rwanda, Uholanzi na Falme za Kiarabu (UAE).


CHANZO::MWANANCHI

No comments: