ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, April 19, 2011

Shabani Kado aikana Simba


Kipa wa timu ya taifa ya vijana wa umri chini ya miaka 23, Shabani Kado, akielekea kwenye gari mara baada ya kuwasili kwa timu hiyo kwenye uwanja wa ndege wa Julius Nyerere wakitokea Uganda jana. Nyjma yake ni waandishi wa habari wakimfuata.(Picha: Omar Fung 
Kipa tegemeo wa timu ya taifa ya vijana wa umri wa chini ya miaka 23, Shabani Kado, amekana kuwa katika mipango ya kujiunga na klabu ya Simba ya Dar es Salaam akisema ataendelea kuidakia timu yake ya Mtibwa Sugar ya Manungu mkoani Morogoro.
Kado, ambaye pia ni kipa tegemeo wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, amekuwa akihusishwa na mipango kutua Simba ili kumrithi Juma Kaseja, ambaye uvumi wa vyombo vya habari umekuwa ukidai kwamba yuko mbioni kutemwa na klabu hiyo ya Msimbazi.

Akizungumza na gazeti hili jana, Kado, alisema kuwa hakuna kiongozi yoyote wa Simba au Yanga aliyefanya naye mazungumzo kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari na kusisitiza kwamba ataendelea kuvaa jezi za Mtibwa Sugar katika msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Kado alisema kuwa tayari alishafanya mazungumzo na viongozi wake wa Mtibwa Sugar na kuongeza mkataba na anaamini kwamba kuwepo kwake kwenye timu hiyo ndio mafanikio yatazidi kupatikana.
Aliongeza kwamba yeye ana mkataba na timu hiyo ya Manungu mpaka mwezi Februari mwakani na kila kinachotakiwa kwenye mkataba wake kinatekelezwa.
"Ni maneno ya watu, hakuna mtu niliyemwambia kwamba ninataka kuhakikishiwa namba endapo nitajiunga na Simba, nilishaafikiana tayari na viongozi wangu kwa hiyo mimi ni mchezaji wa Mtibwa Sugar mpaka mwezi Febriari mwakani," alisema kipa huyo.
Aliongeza kuwa anafahamu 'presha' zilizoko katika timu hizo kongwe hivyo anahitaji kupata muda wa kufikiri kabla ya kujiunga na klabu mojawapo endapo watamuhitaji.
Umahiri wa kipa huyo ulionekana wakati alipokuwa anagombewa na kocha wake wa timu ya vijana, Jamhuri Kihwelu 'Julio' na kocha wa Stars, Mdenmark, Jan Poulsen, ambaye alisema kwamba timu ya ya wakubwa ndiyo inayopaswa kupewa kipaumbele cha kukaa na wachezaji inaowahitaji.
Kado aling'ara wakati yosso wa Tanzania walipowaondoa wenzao wa Cameroon kwa kupangua penati moja na nyingine ikigonga mwamba na kuwafanya watinge hatua ya 16-Bora ya mashindano ya kusaka tiketi ya kucheza fainali za Olimpiki zitakazofanyika London, Uingereza mwakani.
Licha ya klabu kuanza zoezi hilo, bado Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) halijafungua rasmi pazia la usajili kwa ajili ya msimu ujao.
CHANZO: NIPASHE

No comments: