ANGALIA LIVE NEWS

Monday, April 4, 2011

Simba yafa kiume kwa Mazembe


Amir Maftah (kulia) wa Simba akiwachambua Kipa wa TP Mazembe Kidiasa (kushoto) na Beki wake Benza Bedi, wakati timu zao zilipopambana michuano ya raundi ya pili ya fainali ya Klabu Bingwa ya Afrika, kwenye mechi iliyofanyika uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam jana.

Mabingwa TP Mazembe walidumisha matumaini yao ya kutetea kwa mara ya tatu mfululizo taji lao la Ligi ya Klabu Bingwa Afrika wakati walipoiengua Simba ya Tanzania katika mechi ngumu iliyoisha kwa wageni kuibuka na ushindi wa 3-2 kwenye Uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam jana.
Kwa ushindi huo, TP Mazembe, ambayo mwaka jana ilicheza fainali ya Kombe la Klabu la FIFA, imesonga mbele kwa jumla ya magoli 6-3, baada ya kuwa iliwafunga Wekundu wa Msimbazi 3-1 katika mechi yao ya awali ya hatua ya kwanza mjini Lubumbashi wiki mbili zilizopita.
Simba walikomboa mara mbili na kufanya ubao wa matokeo usomeke 2-2 lakini TP Mazembe walikuwa bora zaidi na kuwamaliza wenyeji kwa goli la tatu katika dakika ya 73.
Mazembe walianza kwa nguvu zaidi na katika dakika ya 16 walipata goli walilokuwa wakilihitaji ili kuingiza mguu mmoja kwenye hatua ya pili ya michuano lililofungwa na Given Singuluma kwa shuti la kustukiza baada ya kuuwahi mpira wa kona.
Baada ya kipa mwenye vituko Robert Kidiaba kuokoa hatari kadhaa langoni mwake, Simba walipata goli kufuatia Pamphile Mihayo kujifunga wakati akijaribu kuokoa krosi ya Shija Mkina katika dakika ya 57.

Dakika saba baadaye, Mazembe walifunga goli la pili kupitia kwa Alain Kaluyituka aliyemzidi ujanja beki Juma Nyosso na kupiga shuti lililomzidi kipa Juma Kaseja.
Yosso aliye katika kiwango cha juu wa Simba, Mbwana Samata ambaye alikuwa akisumbua ngome ya mabingwa, aliipatia timu yake goli la pili kwa kichwa katika dakika ya 65 kufuatia mpira wa kona uliopigwa na Amir Maftah.
Kaluyituka alizima ndoto zozote za Simba za kurejea maajabu ya mwaka 2003 ya kuwatoa mabingwa watetezi wakati walipofanya hivyo kwa Zamalek ya Misri, kwa kufunga goli lake la pili jana na la tatu kwa Mazembe kwa kutumia udhaifu wa walinzi wa Simba kushindwa kujipanga.
Simba ilikuwa na nafasi ya kufunga mapema zaidi katika dakika ya 12 wakati Samatta alipowachana mabeki wa Mazembe lakini baada ya kusubiri bila ya mafanikio msaada kwa mchezaji wa kumpasia, mshambuliaji huyo aliyejikuta ametelekezwa katikati ya "msitu" wa mabeki alilazimika kupiga shuti lililombabatiza kipa Kidiaba.
Kidiaba aliyejichukulia umaarufu Afrika na duniani kwa staili yake ya kushangilia kwa kudunda-dunda kwa makalio huku akiwa amekaa chini, alifanya kazi ya ziada kuupangulia juu ya lango mpira wa shuti la Mgosi katika dakika ya 34 kufuatia kazi nzuri ya Samatta tena.
Kipigo hicho hakikuonyesha kumstua kocha wa Simba, Patrick Phiri ambaye siku zote za mpambano wao amekuwa akiwaita Mazembe "walimu na Simba ni wanafunzi" akisema ameridhishwa na kiwango cha wachezaji wake na akaipongeza Mazembe akisema ni timu ya kiwango cha juu, ambayo imeimarishwa zaidi na mechi za kimataifa ilizocheza mwaka jana katika Kombe la Klabu la FIFA.
Ukubwa wa mechi ulivutia mashabiki wengi waliofurika katika uwanja huo huku jezi nyekundu na nyeupe zikitawala licha ya kwamba mashabiki wa mahasimu wa Simba katika ligi ya nyumbani Yanga pia walikuwepo.
Hapakuwa na manjonjo ya kushangilia kwa mashabiki wa Simba walioondoka vichwa chini huku, mashabiki wachache wa Mazembe wakitawala ugenini.
Vikosi jana vilikuwa; Simba: Juma Kaseja, Salum Kanoni, Juma Jabu, Kelvin Yondan, Juma Nyosso, Jerry Santo, Mussa Hassan Mgosi, Patrick Ochan, Emmanuel Okwi, Mbwana Samatta na Amir Maftah
TP Mazembe: Robert Kidiaba, Jean Kasusula, Eric Nkulukuta, Given Singuluma, Patou Kabangu, Benza Bedi, Alain Kaluyituka, Stopila Sunzu, Rainford Kalaba, Pamphile Mihayo, Narcisse Ekanga.
CHANZO: NIPASHE

No comments: