ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, April 12, 2011

Taifa Stars kuwavaa Bafana Bafana Dar

12th April 2011
Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars

Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, itacheza mechi ya kimataifa ya kirafiki na timu ya taifa ya Afrika Kusini 'Bafana Bafana' mnamo Mei 14 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, timu hiyo inatarajiwa kuivaa Msumbiji Aprili 23 ambapo kipa Juma Kaseja ameachwa katika kikosi kitakachokwenda Maputo lakini atakuwemo baadaye mwezi Juni katika maandalizi ya kuivaa timu ya taifa ya Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Stars inatarajia kwenda ugenini kuivaa Msumbiji Aprili 23 ikiwa ni mechi maalum kwa ajili ya ufunguzi wa uwanja mpya wa kisasa uliojengwa nchini humo.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Kocha wa Stars, Mdenmark Jan Poulsen, alisema kuwa mechi zote hizo mbili zinachezwa kwa ajili ya kuiandaa timu yake na mechi ya marudiano dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati ambao ni wa kusaka tiketi ya kushiriki fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika utakaochezwa Juni 4.
Alisema kuwa baada ya kurejea kutoka Msumbiji, Stars itaingia tena kambini Mei 2 ili kujiandaa na mechi dhidi ya Bafana Bafana.
"Pia tunatarajia kucheza mechi nyingine mbili za kirafiki za kimataifa kati ya Mei 22 na 28, ratiba inaonyesha kwamba Stars itakuwa ikiingia kambini mara kwa mara kwa ajili ya kuwaweka imara wachezaji kwa sababu muda huu hawatakuwa na mechi za ligi," alisema.
Aliwataja wachezaji watakaoivaa Msumbiji kuwa ni Shabani Kado, Shabani Dihile, Shadrack Nsajigwa, Aggrey Morris, Nadir Haroub,'Cannavaro', Amir Maftah, Juma Nyosso, Kigi Makasi, Nurdin Bakari, Shabani Nditi, Jabir Aziz, Ramadhani Chombo,' Redondo' na Mwinyi Kazimoto.
Wengine ambao ni washambuliaji ni Salum Machaku, Mrisho Ngassa, Mohamed Banka, John Bocco na Mbwana Samatta.
Aliongeza kuwa wachezaji wanaocheza nje ambao wataungana na wenzao kuivaa Jamhuri ya Afrika ya Kati mwezi Juni ni Juma Kaseja, Idirssa Rajab, Henry Joseph, Abdi Kassim, Danny Mrwanda, Nizar Khalfan na Athumani Machuppa.
Poulsen ambaye ni mkufunzi wa makocha anayetambuliwa na Shirikisho la Soka la Duniani (FIFA), pia anatarajia kwenda Gambia kuongoza semina ya makocha kwa muda wa siku tano kuanzia Mei 2.
CHANZO: NIPASHE

No comments: