ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, April 27, 2011

Waziri mwingine atua Samunge

Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Eng. Christopher Chizza (kushoto) akizungumza na Mchungaji Ambilikile Mwasapila (kulia) katika kijiji cha Samunge, Loliondo, mkoani Arusha baada ya kunywa dawa jana. Picha na Mussa Juma
Mussa Juma, Samunge
NAIBU Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chizza na familia yake, jana walikuwa miongoni mwa watu waliopata kikombe cha tiba ya magonjwa sugu kwa Mchungaji Ambilikile Mwasapila katika Kijiji cha Samunge, Loliondo.
Chizza aliwasili Samunge akiwa na mkewe na wanafamilia wengine na kupokewa na Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Elias Wawa Lali. Mbali ya kupata kikombe, alitumia fursa hiyo pia kumpa pole mchungaji huyo ambaye amefiwa na mtoto wake.
Akizungumza mara baada ya kupata kikombe cha tiba, Chizza alisema ni wajibu wa Serikali kuboresha miundombinu ya kufika Samunge kutokana na watu wengi wa ndani na nje ya nchi kwenda Samunge."Bado barabara siyo nzuri na mazingira ya Samunge ni machafu. Ni wajibu wa Serikali kuboresha miundombinu na utaratibu wa kutunza mazingira," alisema Chizza.

Waziri huyo ambaye alifika Samunge kwa gari alisema, ameamua kutumia mapumziko ya Pasaka kwenda Samunge kupata tiba baada ya kusoma habari za Mchungaji Mwasapila na kupata taarifa za watu kupona magonjwa mbalimbali.

Robo tatu ya magari Samunge yatokea Kenya
Raia wa Kenya, juzi na jana walitinga kwa wingi hapa Samunge na kufanya karibu robo tatu ya magari yaliyokuwapo hapa kutoka nchi hiyo jirani. Mengi ya magari hayo ni mabasi madogo, maarufu kama matatu (daladala).
Wakenya hao waliingia kuanzia juzi usiku na kutawala Viwanja vya Samunge, huku magari machache ya Watanzania yakianza kuingia jana asubuhi.Licha ya Wakenya, raia wa Rwanda na Uganda jana wali
tinga Samunge na kupata kikombe na sasa idadi ya wageni kutoka nje ya nchi waliofika Samunge, imefikia zaidi ya 13,700.

Wagonjwa kuweka matanga kwa Babu
Baadhi ya wagonjwa leo wanaanza matanga nyumbani kwa Mchungaji Mwasapila ambaye amefiwa na mtoto wake, Jackson (43).Wakizungumza na Mwananchi jana, baadhi ya wagonjwa waliopo Samunge, walisema wataendelea kuwapo Samunge hadi Ijumaa Mchungaji Mwasapila atakaporejea.
"Kama unavyoona siyo rahisi leo kupata kikombe. sisi tutakuwa hapa nyumbani kwa Mwasapila hadi arudi msibani na tutaweka matanga," alisema John Lyimo aliyekuwa anatokea Same, mkoani Kilimanjaro.
Mkazi mwingine wa Musoma, Joram Mahiza ambaye alikuwa na familia yake, pia alisema hatarajii kurejea Musoma hadi Ijumaa atakapopata kikombe: "Sisi tutamsubiri tu hapa tutakuwa na jamaa zake hapa msibani."
Lali alitangaza juzi kusitishwa kwa safari na huduma hiyo ya tiba hadi Ijumaa Mchungaji Mwasapila atakaporejea kutoka Babati. Alitarajiwa kuondoka Samunge jana jioni

CHANZO:MWANANCHI

No comments: