ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, April 27, 2011

Rais Kikwete, Maalim Seif wang'ara Z'bar

Rais Jakaya Kikwete (kulia) akizungumza na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein wakati wa maadhimisho ya Muungano
Viongozi mbalimbali wakiwa wamesimama wakati gwaride la heshima likipita kwa mwendo wa haraka wakati wa maadhimisho ya Muungano Mjini Zanzibar. Picha na Ramadhan Othman-Ikulu Zanzibar na Muhidin Sufiani -Ofisi Ya Makamu Wa Rais

Elias Msuya na Salma Said, Zanzibar
MAMIA ya watu jana waliupamba Uwanja wa Amani, Zanzibar katika sherehe za maadhimisho ya miaka 47 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Watu hao walionekana kuvutiwa zaidi na mgeni rasmi, Rais Jakaya Kikwete na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad.Umati huo wa watu, wengi wao wakiwa katika sare tofauti tofauti, ulilipuka shangwe za kelele na vifijo wakati viongozi hao wawili walipoingia kwenye uwanja huo kwa nyakati tofauti.
Rais Kikwete aliingia uwanjani hapo majira ya saa nne asubuhi akiwa kwenye gari la wazi na kuwapungia mkono mamia ya wananchi na baadaye kukagua gwaride.Baada ya hapo gwaride lilipita mbele ya Jukwaa Kuu kwa mwendo wa kasi na kisha mwendo wa pole.
 Ulipowadia wakati wa halaiki iliyowashirikisha wanafunzi 500, mvua kubwa ilianza kunyesha na kuvuruga kabisa sherehe hizo.Kwa mujibu wa ratiba ya sherehe hizo, kipindi kilichokuwa kikifuatia ni ngoma za asili, lakini mvua ilipozidi washereheshaji walitangaza kukatisha na viongozi wakaanza kuondoka.
Kaulimbiu ya sherehe hiyo ilikuwa ni “Miaka 47 tuwaenzi waasisi wetu, tudumishe Muungano, matunda ya miaka 47 ya Mapinduzi na miaka 50 ya uhuru, amani, utulivu na maendeleo ni matokeo ya Muungano wetu."
Sherehe hizo zimefanyika huku kukiwa na kauli mbalimbali kutoka kwa wananchi na hata baadhi ya viongozi wa Zanzibar wakitaka Muungano huo ufanyiwe tathimini upya.
Viongozi wengine waliokuwapo katika sherehe hizo ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk Gharib Bilal, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Dk Ali Mohammed Shein na Makamu wake wa Pili, Balozi Seif Idd.
Wengine ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Anne Makinda; Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Pandu Ameir Kificho; Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange; Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Ali Hassan Mwinyi, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Sita wa SMZ, Dk Salim Amour.
Pia walikuwapo viongozi wa vyama vya siasa, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM, Philip Mangula, Mwenyekiti wa NCCR -Mageuzi, James Mbatia na wanadiplomasia wanaoziwakilisha nchi zao nchini.
Viongozi wengine wa kitaifa akiwamo Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, mawaziri wakuu wastaafu, Cleopa Msuya, Dk Salim Ahmed Salim na Frederick Sumaye hawakuwapo katika sherehe hizo.
Jumuiya, taasisi za Kiislamu zatoa tamko
Katika hatua nyingine, Umoja wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar zimetoa tamko kuhusu hali ya Muungano zikisema umekosa kukubalika kwa Wazanzibari tangu siku yake ya kwanza hadi leo.
Huku wakitoa ushahidi wa tume kadhaa zilizoundwa ili kutafuta maoni ya wananchi kama vile Tume ya Jaji Nyalali na ile ya Jaji Kissanga, jumuiya hizo zimekilaumu CCM kwa kile walichokiita kuhodhi Muungano. Katika tamko hilo la pamoja, zimesema kuwa nguvu za Zanzibar ikiwa mshirika kamili wa Muungano huo hazipo.
“Kwa karibu miaka yote 47, Muungano huu umekuwa ni miliki ya chama kimoja cha siasa cha CCM, ukitoa miaka michache ya 1964-1977”.Jumuiya hizo zimetaka kuwapo kwa majadiliano ya Muungano zikitaka pia nafasi ya Rais wa Zanzibar katika Muungano ya kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais, irejeshwe.
“Mjadala wowote wa Muungano ule urudishe nafasi ya Rais wa Zanzibar katika Muungano na siyo ilivyo hivi sasa... Rais wa Zanzibar hana maana wala amri yoyote ile katika Muungano,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

CHANZO:MWANANCHI

No comments: