Mabasi yaua abiria 16
Yajeruhi wengine 58
Yaligongana uso kwa uso
Yajeruhi wengine 58
Yaligongana uso kwa uso.jpg)
Watu 16 wamekufa na wengine 58 kujeruhiwa vibaya, wilayani Geita mkoani Mwanza, baada ya mabasi mawili kugongana uso kwa uso katika kijiji cha Chibingo. Ajali hiyo ilitokea jana saa 3.30 asubuhi na mabasi yaliyohusika na ajali hiyo ni Sheraton lenye namba za usajili T 268 AJC mali ya Talib K. Abdallia, lililokuwa likiendeshwa na dereva Enos na basi la Bunda lenye namba T 810 BDW lilolokuwa likiendeshwa na Karamdin.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ajali hiyo, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Nonosius Komba, alisema kati ya waliokufa, 12 walikufa papo hapo eneo la ajali.
Alisema wengine watatu walifariki wakiwa katika hospitali ya wilaya ya Geita na mwingine amefia wilayani Sengerema alasiri jana wakati akipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando akiwa miongoni mwa majeruhi tisa waliohamishiwa huko.
Kamanda Komba alisema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe na kuwa madereva wa mabasi yote mawili wanashikiliwa kwa mahojiano kwa ajili ya hatua za kisheria.
“Basi la Sheraton lilitaka kulipita lori lililokuwa mbele yake wakati basi la Bunda nalo likija kwa mwendo wa kasi na ndipo yakakutana uso kwa uso. Abiria waliofariki wametoka katika mabasi yote mawili,” alisema Komba na kusisitiza kuwa chanzo ni uzembe wa madereva hao.
Basi la Sheraton na Mitsubishi Fuso yalikuwa yakitokea Ushirombo kuelekea jijini Mwanza wakati lile la Bunda likitokea Mwanza kwenda wilayani Karagwe, mkoani Kagera.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Geita, Dk. Omari Dihega, alithibitisha kupokea maiti ya watu 16 kati yao mmoja alifariki alasiri wakati akipelekwa hospitali ya Rufaa Bugando, pamoja na majeruhi 58 waliotokana na ajali hiyo.
Alisema hali za majeruhi ambao wamelazwa hospitalini hapo ni mbaya na kwamba majeruhi tisa wamepelekwa katika hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza kwa matibabu zaidi.
Alisema miongoni mwa majeruhi waliofikishwa hospitalini hapo, yumo mtoto mchanga, Amina Abdallah mwenye umri wa wiki tatu ambaye alinusurika na hakupata jeraha.
Alisema kuwa miili 11 ya marehemu tayari imetambuliwa na ndugu zao, ambao ni pamoja na Danny Zabron aliyefariki njiani wakati akimbikizwa katika hospitali ya Rufaa ya Bugando, Maneno Ngassa, Amani Deogratius; Samson Sanga na wengine waliotambuliwa kwa jina moja moja, ambao ni Msemakweli na Mwarabu.
Wengine waliofariki katika ajali hiyo ni Jonson Nyonyi, Klalfan Chinga, Sumbuko Paulo, Samson na Deogratius Makunga.
Majeruhi katika ajali hiyo ni Venance Nestory, Masoud Athuman, Abel Shimbo, Ibrahim Kihungwe, Mudashiri Joseph, Mabula Lusegwa, Jumanne Katoto, Zanzibar Kitangila, Enock Paulo, Mussa Kashiriri, Sele Elius, Deogratius Mathias, Fikiri Leonard, Claud Mashimba, Mchungaji Jonasi, Tupatupa na Isaya Ally.
Wengine waliojeruhiwa katika ajali hiyo ni Samuel Lukanye, Charles Maige, Libu Kahadi, Kimbi Bahati, Nathaniel Bernard, Masai Magembe, Emmanuel Mabala, Boniface Kitagalo (amepelekwa Bugando), Joseph Mabwanga (Bugando), Tereza Tondane (Bugando), na Juma Fanuel (Bugando).
Aliwataja wengine waliojeruhiwa kuwa ni Christina Joseph, Imaculata Mgula, Emilian Joseph, Godness Joseph, Veronica Lwagalo, Marietha Kalokola, Dadia Bernard, Edith Charles, Agnes Moris, Thereza Ondope, Salome Alon, Agripina Nathaniel, Gretuda Hoston, Edna Jackson, Lulu Kishabakaki (Bugando), Forestina Magige (Bugando), Christina Joseph, Mawazo Nicolaus (Bugando) na wengine waliotambulika kwa jina moja moja la Leon na Chiza.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment