.jpg)
Nadir Haroub `Cannavaro`
Kocha wa timu ya taifa ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, Jan Poulsen, amemshauri beki wa kati wa mabingwa wa soka wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Yanga, Nadir Haroub 'Cannavaro' asijiunge na klabu ya Simba ambayo inasemekana kuanza mipango ya kumsajili.
Habari ambazo NIPASHE imezipata kutoka katika kambi ya Taifa Stars, ni kwamba beki huyo alifuatwa na Poulsen juzi asubuhi na kuulizwa na kocha huyo kama ni kweli amesaini mkataba wa kujiunga na Simba kama ilivyoripotiwa katika vyombo vya habari nchini.
Chanzo kilisema kwamba baada ya kocha huyo kumuuliza Cannavaro, beki huyo alikana kujiunga na Simba na Poulsen alimtaka asiihame Yanga.
Alimweleza Cannavaro kwamba tabia ya kuhama-hama klabu sio nzuri na endapo anataka kuheshimika kwa uwezo wake kuonekana ni vyema akaendelea kuichezea Yanga.
"Baada ya magazeti kuandika kuwa amesaini mkataba wa kujiunga na Simba, babu (Poulsen) alimfuata na kutaka afahamu ukweli kutoka kwa Cannavaro mwenyewe, baada ya kujibiwa alimshauri asipende tabia ya kuhama hama," kilisema chanzo chetu.
Cannavaro aliliambia gazeti hili jana mchana kwamba muda wa usajili haujafika na yeye bado anaheshimu mkataba wake na Yanga ambao unamalizika mwezi Desemba mwaka huu.
Alisema kuwa muda wa usajili ukifika yeye hatakuwa mzungumzaji na kama Simba wanamuhitaji watatakiwa kwenda kuzungumza na Yanga kama taratibu zinavyoeleza.
Alisema kuwa yeye anachoangalia ni kuona maslahi yake yanalindwa na hapo atacheza kwa juhudi na kuisaidia timu ifanye vizuri kwenye ligi na mashindano ya kimataifa.
"Sina tatizo kama Simba watakuwa tayari kulipa gharama zangu na kuvunja mkataba nilionao Yanga, niko tayari kukipiga Msimbazi msimu ujao," Cannavaro ambaye pia ni tegemeo katika ukuta wa timu ya Zanzibar, Zanzibar Heroes aliongeza.
Alisema pia ushauri wa wazazi wake ni sehemu ya maisha yake na kwamba katika kufanya maamuzi yake daima huwashirikisha wote wawili pale inapohitajika na anaamini kwamba nao hawatakuwa radhi kuacha fedha endapo atapata klabu nyingine ya Tanzania au nje ya Tanzania.
"Najua mama yangu anataka niendelee kucheza Yanga kwa sababu ndio timu anayoishabikia, lakini baba yangu naye ni shabiki mkubwa wa Simba atafurahi nikihamia upande wake," aliongeza Cannavaro.
Beki huyo msimu uliopita aliisaidia Yanga isifungwe magoli mengi na kuipa ubingwa wa ligi kutokana na kuwa na tofauti nzuri ya magoli ya kufunga na kufungwa.
Habari ambazo Simba na mchezaji huyo hawajathibitisha ni kwamba amesaini mkataba wa miaka mitatu na dirisha la usajili utakapofika Wekundu hao watawasilisha maombi yao rasmi kwa Yanga.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake