.jpg)
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, John Mwankenja
Rais Jakaya Kikwete ameiagiza serikali mkoani Mbeya kuwasaka, kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria watuhumiwa wote wa mauaji ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, John Mwankenja aliyeuawa juzi kwa kupigwa risasi akiwa nyumbani kwake.
Ametoa agizo hilo kupitia Waziri wa Maji, Profesa Mark Mwandosya ambaye aliueleza umati wa maelfu ya wananchi waliojitokeza kwenye mazishi ya Mwankenja yaliyofanyika jana katika kijiji cha Mpandapanda kilichopo kata ya Kiwira wilayani Rungwe.
“Baada ya kutokea tukio hili la mauaji ya kinyama, Rais Kikwete alinitafuta kwa simu na kuniuliza kulikoni mauaji haya na amesema wale wote waliohusika katika mauaji haya watafutwe na watiwe mbaroni,” alisema Profesa Mwandosya wakati akiwasilisha salama hizo za rais.
Alisema wanasiasa vijana waache siasa za chuki na badala yake waendeleze umoja,upendo na amani kwa lengo la kuitakia mema wilaya ya Rungwe ambayo imeanza kupoteza sifa kutokana na mfululizo wa matukio mabaya.
Alisema heshima ya wilaya ya Rungwe imeanza kupungua ambapo kulianza kutokea mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi na baadaye matukio ya ubakaji wa watoto na kuuawa na sasa wanaanza kuuwa viongozi kama ilivyotokea kwa Mwenyekiti wa Halmashauri.
Akitoa salamu za rambirambi, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa, Deo Sanga ‘Jar People’ ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mazishi hayo ,alisema matukio ya mauaji haya ni matokeo ya baadhi ya watu wanaoendelea kuchochea vurugu nchini.
Kwaupande wake Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, John Mwakipesile, alisema hivi sasa nchi inapita katika kipindi kigumu cha siasa ambapo vimekuja vyama vingi hivyo akashauri wanasiasa wasichanganye siasa na uadui na kuanza kuuwana.
“Siku hizi nasikia maandamano , matusi na kejeli kwa viongozi, hizi siyo siasa bali siasa ni urafiki na kujenga zinazokubalika kwa wananchi ambao watakuchagua,”alisema Mwakipesile.
Akizungumzia agizo la Rais Kikwete, Mwakipesile ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoa wa Mbeya, alisema amesikia agizo hilo na amesoma mabango yaliyoandikwa na wananchi wakitaka hatua zichukuliwe dhidi ya wahalifu hao.
Naye Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia elimu, Kassimu Majaliwa, alisema matukio kama haya yanatokana na baadhi ya watu kulewa amani na utulivu uliopo nchini kwa kipindi kirefu.
Aliwataka wananchi kuwafichua watu hao ili serikali yao wanayoiamini iweze kuwachukulia hatua ili wananchi wengine waendelee kuishi kwa amani.
Shughuli za mazishi ya marehemu Mwankenja,zilianza kwa ibada takatifu iliyoongozwa na Askofu wa Kanisa la Moraviani Jimbo la Kusini, Lusekelo Mwakafwila, iliyofanyika katika kanisa la Moraviani Usharika wa Kiwira.
Akitoa tamko la kanisa Mwenyekiti wa Kanisa la Moraviani Jimbo la Kusini, Mchungaji Clement Mwaitebele, alisema serikali iwasake na kuwakamata wauaji kisha kutoa taarifa kwa wananchi ili waendelee kuiamini serikali yao.
Marehemu John Mwankenja aliuawa Mei 19, mwaka huu kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana wakati akiegesha gari nyumbani kwake baada ya kurejea kutoka Mbeya Mjini alikokwenda kumsalimia mkewe ambaye alikuwa amelazwa hospitalini akisubiri kufanyiwa upasuaji.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake