ANGALIA LIVE NEWS

Friday, May 20, 2011

Maelfu ya waandamanaji wa mji wa Iringa na viunga vyake wakiwa katika maandamano ya amani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), yalioanzia Kihesa hadi Uwanja wa Shule ya Msingi 
Mji wa Iringa na vitongoji vyake, jana ulirindima kwa kila aina ya mbwembwe, baada ya maelfu ya wakazi wake wakiongozwa na wafuasi wa Chadema, kujitokeza katika maandamano ya amani yaliyoongozwa na viongozi wakuu ngazi ya taifa, wabunge na makada waandamizi wa chama hicho.
Maandamano hayo yaliyoanzia katika eneo la Kihesa karibu kilomita nane kufika katika uwanjani hapo, yalisindikizwa na msururu mrefu wa baiskeli, pikipiki na bajaj, ambazo idadi yake haikufahamika mara moja kwa jinsi zilivyokuwa nyingi.

Pia yalisindikizwa na watembea kwa miguu waliobeba mabango yenye ujumbe mbalimbali, huku wengine wakiimba nyimbo za kukijeli Chama Cha Mapinduzi (CCM), baadhi ya viongozi wake, viongozi wa serikali na watuhumiwa wa ufisadi.
Pia barabara kuu ya Dodoma na ile ya Mlandege, zilifungwa kwa muda ili kuruhusu waandamanaji kuzitumia.
Maelfu ya watu walijipanga kando kando mwa barabara hizo, kuanzia saa 6.00 mchana hadi saa 9.00 alasiri, kushuhudia maandamano hayo ya aina yake, yaliyohitimishwa katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mlandege.
Viongozi hao walioongozwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Makamu wake Zanzibar, Said Issa Mohamed, Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa na Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara, Zitto Kabwe, ni pamoja na Mbunge wa Viti Maalum (Zanzibar), Mariam Salum Msabaha, Joyce Mukya (Viti Maalum-Arusha), Raya Ibrahim Khamisi (Viti Maalum-Pemba) na makada waandamizi wa chama, Thomas Nyimbo na Fred Mpendazoe.
Wengine ni Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama, Wilfred Lwakatare, Naomi Kaihula (Viti Maalum-Mbeya), Joseph Mbilinyi, maarufu kama “Mr. Sugu” (Mbeya Mjini), Grace Kiwelu (Viti Maalum-Kilimanjaro), Suzan Kiwanga (Viti Maalum-Morogoro), Mkurugenzi wa Sera na Utafiti, Mwita Mwikabe Waitara, Mkurugenzi wa Organaizesheni na Mafunzo, Benson Kigaila, Chiku Abwao (Viti Maalum-Iringa) na Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini).
Operesheni hiyo ya chama hicho ilihitimishwa jana katika mikoa sita ya Nyanda za Juu Kusini; inayohusisha mikoa ya Mbeya, Rukwa, Katavi, Ruvuma, Njombe na kuhitimishwa na mkoa wa Iringa.
Kwa mujibu wa Mratibu wa Operesheni hiyo, Kigaila, timu hizo kati ya sita hadi nane za operesheni hiyo, zilifanikiwa kutembelea majimbo yote 37 yaliyoko katika mikoa hiyo.
Pia zilitembelea kata 224, kufanya mikutano ya hadhara katika vijiji 457 na kugawa kadi 46,000 za chama na kufanikiwa kutatua migogoro mbalimbali ya uongozi na wanachama katika maeneo hayo.
SLAA AMSHANGAA MEMBE
Naye Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibroad Slaa alisema anasikitishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe kwa kauli yake kwamba, Serikali Uingereza imeisikitisha Tanzania kwa kupeleka fedha za chenji ya rada kwa mashirika wahisani, badala ya serikalini.
“Ni halali fedha zile zipelekwe kwenye NGO (shirika lisiyo la kiserikali) wanayoiona ilimradi inaaminika kuliko kuipeleka serikalini kulikojaa ufisadi,” alisema Dk. Slaa.
Aliitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuhakikisha inashughulikia ufisadi wote, ukiwamo unaohusisha kampuni ya Kagoda Agriculture Limited, vinginevyo itapoteza uhalali wa kuwapo kwake licha ya viongozi wake kupokea mishahara mikubwa.
MBOWE: LISSU, MARANDO WAPO TARIME
Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, alisema wananchi waliouawa Tarime, ambao ndugu zao wamekataa kuwazika, Chadema itawasaidia.
Alisema tayari wameshatuma timu ya watu kwenda Tarime, akiwamo Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Mabere Marando na kwamba, viongozi wakuu wa chama watafuata baadaye.
ZITTO AMVAA NGELEJA
Katika hatua nyingine Zitto jana alimtaka Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, kujiuzulu wadhifa wake serikalini, kwa madai ya kushindwa kuwa ‘waziri wa umeme’ na badala yake amekuwa waziri wa mgawo wa nishati hiyo.
Zitto alisema hayo alipohutubia mkutano wa hadhara, uliofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mlandege, baada ya kuhitimishwa kwa maandamano yao.
Zitto, ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini na Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi, alitoa kauli hiyo kuzungumzia uamuzi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kutangaza mgawo wa umeme, ulioanza jana katika mikoa inayotumia nishati hiyo kwa gridi ya taifa.
Alisema tayari wamekwisha kumuagiza Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, ambaye ni Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, kuhakikisha anasimamia kwa dhati na makini hoja ya chama ya kutaka Ngeleja ajiuzulu kutokana na sababu hizo.
“Huyu ni waziri wa umeme au mgawo wa umeme?” alihoji Zitto, ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni.
Zitto alisema mgawo wa umeme umekuwa ukiwaathiri wananchi, hususan wale wadogo, wakiwamo wanaojiajiri katika saluni za kunyoa nywele na mashine za kusagisha nafaka.
Alisema wananchi hao wamekuwa wakishindwa kufanya shughuli zao, badala yake wanahangaika kwa sababu ya kukosa umeme.
“Kwa nini tuendelee kuwa na mikataba ya kifisadi inayosababisha tuwe na mgawo wa umeme, huku wananchi katika mikoa mingi tuliyotembelea wakiendelea kuishi maisha magumu?” alisema Zitto.
Alisema timu ya Chadema inayoundwa na Mbowe, Dk. Slaa na Zitto, ndiyo pekee itakayowakomboa Watanzania na kwamba, maadui kamwe hawawezi kuwagombanisha kwa vile Chadema bado ni chama imara.
Zitto, alisema hatua ya Wizara ya Fedha na Uchumi kutoa waraka unaowaagiza makatibu wakuu pamoja na wakurugenzi wake wote kwamba, kila ifikapo tarehe 25 kila mwezi, watumishi wake wote wawe wamelipwa mishahara, ni miongoni mwa mafanikio makubwa ya kazi ya Chadema.
CHANZO: NIPASHE

No comments: