MWANAFUNZI wa Darasa la Kwanza katika Shule ya Msingi Ambureni, wilayani Arumeru, Mkoa wa Arusha, Prince Elisaria (7), amekutwa ameuawa na kuwekwa ndani ya mfuko maarufu kama kiroba.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Akili Mpwapwa, alisema tukio hilo ni la Mei 3, mwaka huu saa 8.00 mchana. Lilitokea katika Kitongoji cha Nguambia, kijijini Nkoandua.
Alisema mtoto huyo aliondoka nyumbani kwa wazazi wake Aprili 29, mwaka huu saa 1.00 asubuhi akienda shuleni, lakini hakurejea.
“Lakini cha kushangaza wazazi walisubiri muda ulipofika wa kurudi nyumbani hawakumwona na walipojaribu kuulizia shuleni hakuonekana, ndipo jitihada za kumtafuta zikaanza na wakatupa sisi polisi taarifa,” alisema Mpwapwa.
Kaimu Kamanda huyo alisema baada ya Polisi kupewa taarifa, waliendesha msako kwa kushirikiana na wananchi ndipo wakaukuta mwili huo ukiwa umefungwa katika mfuko.
“Tuliufungua mfuko huo, tukashangaa kuona mwili wa mtoto huyo huku akiwa tayari amefariki na tayari ameanza kuharibika, tukachunguza na kubaini aliuawa na watu, hivyo tukaamuru uzikwe,” alisema.
Polisi wanaendelea na uchunguzi, ili kubaini wahusika wa mauaji hayo. Mpwapwa amewaomba watu wanaowafahamu waliohusika watoe taarifa za siri Polisi.
“Mnajua ndugu zangu lazima tushirikiane katika kuwafichua watu kama hawa, haiwezekani watu wauawe kama wanyama na tusiwafichue, leo ameuawa mtoto wa mwenzako na kesho atauawa wa kwako,” alisema Kaimu Kamanda wa Polisi.
CHANZO:HABARI LEO
No comments:
Post a Comment