ANGALIA LIVE NEWS

Friday, May 13, 2011

Siri 10 za kumjua mpenzi aliyekusaliti muda mfupi uliopita!-2(GPL)

NINA furaha sana, maana ile siku muhimu ya kukutana nyingi rafiki zangu imefika. Wakati ambao tunautumia kwa ajili ya kuwekana sawa na kutengeneza maisha yetu ya kimapenzi. Karibuni sana tujifunze.

Mada ni kama inavyoonekana hapo juu ikiwa ni mwendelezo kutoka wiki iliyopita. Yes...nazungumzia juu ya mambo ambayo wengi hawapendi yajulikane. Siri 10 za kumjua mpenzi ambaye amekusaliti muda mfupi uliopita.


Kwa bahati mbaya kuna baadhi ya watu wanadhani kwamba kwa kufahamu siri hizi itakuwa rahisi kwa mpenzi aliyesaliti kuigiza ili asioneshe dalili hizi; aaaah! Hao wanajidanganya sana.

Ngoja niwape siri moja, hili ni suala la kisaikolojia zaidi, ambalo hata ukiwa na wadhifa gani, ujanja kiasi gani utanasa tu. Kwa maneno hayo, nawapa habari njema rafiki zangu kuwa kama umesalitiwa utagundua kwa kuzingatia siri hizi ninazoziandika katika ukurasa huu.

Labda niwakumbushe kidogo, wiki iliyopita nilianza kwa kueleza vipengele vitano vya mwanzo ambavyo ni ratiba ya ghafla, kukwepa kuwasiliana, uchangamfu kupitiliza, upole kupitiliza na ugonjwa wa ghafla. Sasa tuendelee katika vipengele vingine.

MAJIBU TATA
Mpenzi ambaye ametoka kukusaliti huwa hapendi kuulizwa maswali mengi, ukimwuliza majibu yake huwa tatanishi sana. Mathalani ameshasingizia kwamba anaumwa, hivyo atafika na kulala moja kwa moja.

Ukitaka kujua zaidi kuhusu kuugua kwake au dharura aliyoipata iliyosababisha achelewe kurudi nyumbani, hukosa majibu yanayoeleweka. Wakati mwingine anaweza kujisahau na kukupa jibu ambalo linakinzana na maelezo yake ya awali. Ukiona hivyo ujue kuna namna.

HATAKI FARAGHA
Kwa kuwa tayari ameshatoka kwa mtu mwingine, huhofia sana kukutana na wewe faragha. Kama tulivyoona katika vipengele vilivyopita, hutengeneza mazingira ya kukufanya msikutane kimwili, hofu yake ikiwa ni kukuficha usigundue mchezo wake mchafu.

Kisingizio cha kuumwa, bila shaka ni kikubwa na kitakufanya ushindwe kuwa na mhemko wa kimahaba, lakini kurudi nyumbani akiwa amekunja ndita au mpole kupitiliza, tafsiri yake ni wewe kuogopa au kuhamisha hisia zako kutoka kwenye mapenzi na kuanza kumfikiria yeye kama yeye! Nasomeka marafiki?

Kwa vyovyote vile, kama ni mwenzi wako wa muda mrefu, zipo alama nyingi zitakazoweza kukufanya ujue kuwa ametoka nje, kwanza ni vyema kumkazania kukutana naye faragha. Hata kama atasingizia anaumwa, ng’ang’ania kukutana naye, maana hapa ndipo penye ukweli mkubwa zaidi.

Mchunguze anavyokupokea, halafu pima uwajibikaji wake. Huwa mvivu na asiyetaka kutoa ushirikiano. Anaweza kuishia kulalamika kuwa hajisikii vizuri na kusisitiza mhairishe zoezi hilo.

Rafiki zangu, njia unayopita kila siku unaijua...sehemu yenye makorongo unaifahamu, yenye matuta pia utatambua, hata yenye makorongo yenye maji yaliyosimama pia unaijua vyema, sasa ukikutana na tofauti yoyote katika barabara unayoitumia siku zote, maana yake tingatinga limepita! 

ANAKWEPA KUSOGELEWA
Akifika tu nyumbani, atahakikisha hupati nafasi ya kuwa naye karibu. Hataki kabisa kusogelewa. Hapo anakimbia vitu vitatu; mosi, inawezekana huko alipotoka alitumia manukato tofauti na aliyotoka nayo nyumbani asubuhi.

Pili, manukato ya sabuni mpya aliyotumia, anaogopa usiyasikie, tatu, kila mtu ana harufu yake, unapokaa na mtu kwa ukaribu hasa faragha kwa saa mbili au zaidi, kila mmoja huhama na harufu ya mwenzake.

Kwa kuwa wewe unaitambua vyema harufu ya mpenzi wako, atahofia kukusogelea maana utashtukia. Mwisho kabisa, hata kama atakuwa amekwepa yote hayo, labda hajaoga, hajatumia manukato mengine, bado utaweza kumkamata kwa harufu ya manukato, sabuni au mafuta aliyotumia mtu aliyekuwa naye.

Kukwepa kukusogelea, tafsiri yake ni kwamba hataki usikie harufu ya tofauti kutoka kwake, maana anajua alichokifanya. Jiulize, kama kila siku huwa mnapokeana kwa mabusu na kukumbatiana, kwanini safari hii anakukwepa? Akili kichwani mwako.
  
ANAKIMBILIA BAFUNI
Akifanikiwa kukuzuga katika kipengele kilichopita, basi safari yake huishia bafuni. Ataenda haraka na hatataka kwenda na wewe maana kuna kitu anajaribu kukuficha. Wengi wanaamini (kuna ukweli kwa asilimia chache) baada ya kuoga wanaweza kupoteza ushahidi wa kutoka nje ya ndoa/wapenzi wao.

Utakapomruhusu aoge, kwanza atatumia sabuni ya siku zote, ambayo anaweza kuitumia kwa wingi awezavyo ili kuficha ushahidi. Atajisafisha zaidi nyeti zake ili usijue kilichotokea muda mfupi.

Akitoka bafuni lazima atakimbilia kwenye meza ya kujipambia kisha hapo atajimiminia manukato ili kuzima kabisa ushahidi ambao ungeweza kumuumbua. Jiulize, kama kila siku huwa mnaoga pamoja, kwanini amekuja ghafla na kukimbilia bafuni bila wewe? Umeona eh!

WASIWASI MWINGI
Atakuwa mwenye wasiwasi mwingi sana, hata kama akikubali kukutana na wewe faragha, ushirikiano huwa hafifu. Mwoga kupitiliza na muda wote huwa anahisi kwamba hatakufikisha salama safari yako.

Wasiwasi wake hauishii hapo, hata kupeana mikono tu na kukutanisha macho, kutakuonesha jinsi alivyo na wasiwasi. Si kama anapenda hali hiyo, ila anazidiwa na hisia za usaliti kwa kuwa anajua alichokifanya muda mfupi uliopita.

Nimesomeka?
Vipengele hivyo, kama utavifuatilia kwa makini, ni rahisi sana kumkamata mwizi wako. Acha papara, chunguza taratibu, ukiona angalau kuna dalili nusu ya hizi nili zokupa hapo juu, ujue wazi kuwa HAPO HUNA MTU, UNAIBIWA TU!
Ahsante sana kwa kunisoma. Naweka kituo kikubwa.

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vya True Love na Let’s Talk About Love. Unaweza kumtembelea kwenye mtandao wake; www.shaluwanew.blogspot.comau jiunge naye kwenye facebook.

No comments: