
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, amelipa meno Shirika la Nyumba la Taifa, kuzibana taasisi za serikali zinazokwepa kulipa kodi, kwa kulitaka likate kodi hizo kwenye bajeti za taasisi hizo kutoka Hazina.
Akifungua mkutano wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa NHC jana, Waziri Tibaijuka alisema "naelewa kuwa sasa hivi mnakusanya kodi na malimbikizo kutoka kwa watu binafsi na taasisi za serikali.Endeleeni na moto huo huo kwani kodi hizo ndizo zinazowawezesha kutoa huduma bora na kutekeleza mipango yenu mingine."
Hata hivyo Profesa Tibaijuka alizitaka taasisi za serikali zisizo na nidhamu katika kulipa kodi, zikatwe katika bajeti zake Hazina."NHC pia ni asasi ya serikali hivyo, mkono wa kulia wa serikali usihujumu mkono wa kushoto."
Taarifa za hivi karibuni za NHC zinaonyesha kuwa wadaiwa wake wakuu kwa sasa ni taasisi za serikali na wizara zake ambazo zinadaiwa wastani wa Sh1.6 bilioni.
"Lakini fanyeni hili kwa ustaarabu na kufuata sheria. Wapo wasioweza kulipa na wasiotaka kulipa, hatuwezi kuwavumilia walio wabinafsi, wadanganyifu msiwavumilie na sisi wa serikali mtubane tulipe, viongozi wa nchi wanaunga mkono hili kwani kila taasisi na wizara ina bajeti za kodi,"alisema.
Mkurugenzi wa NHC, Nehemia Mchechu, alisema shirika hilo limekuwa na mafanikio makubwa lakini, lina changamoto ya kutimiza matazamio ya Watanzania.Msechu alitaja moja ya changamoto hizo kuwa ni kulazimika kuomba kibali kutoka kwa Waziri wa Fedha linapotaka kukopa fedha benki kwa ajili ya kutekeleza miradi yake.
Mchechu alisema katika mwaka ujao wa fedha,HC imejipanga kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya ujenziya nyumba ikiwa na bajeti ya Sh300 bilioni.
Hata hivyo Profesa Tibaijuka alisema ingawa shirika hilo linapaswa kujiendesha kibiashara, lazima lihudumie wananchi kwa kujenga na kuwauzia nyumba nafuu.Alisema kikwazo cha NHC kulazimika kuomba kibali cha kukopa benki kutoka Hazina kinazorotesha utoaji huduma kwa shirika hilo.
CHANZO:MWANANCHI
No comments:
Post a Comment