ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, May 19, 2011

Wajane wa wachungaji waanza kupata misaada

Na Rabia Bakari

WAJANE waliokuwa wake wa wachungaji zaidi ya 50 wameanza kunufaika na msaada kutoka kwa watumishi wa Mungu ambao pia ni wafanyabiashara wa madini kutoka
Lubumbashi, DRC, ambao walikuwa nchini kwa shughuli za kiroho ikiwa ni pamoja na kushiriki katika kongamano la maadili.

Wajane hao, wamefunguliwa akaunti ambayo itakuwa ikiingizwa fedha za kujikimu, huku wafanyabiashara hao wakiangalia utaratibu wa kuwaanzishia miradi itakayowasaidia maishani.

Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu ambaye anaratibu ugeni wa watumishi hao wa Kicongo, Askofu David Mwasota alisema kuwa wamefikiria kulisaidia kundi hilo, kwa kuwa ni kundi la kitumishi linaloathirika zaidi.


"Unajua wake wa wachungaji, waume zao hawana bima, hivyo wakifariki huwaacha katika hali ngumu na kanisa hushindwa kuwahudumia, ndio maana tumeamua kulipatia kundi hili umuhimu mkubwa," aliongeza Askofu Mwasota.

Aliongeza kuwa licha ya kusaidia kundi hilo, lakini pia kuna watoto kadhaa yatima wa wachungaji ambao walishindwa kuendelea na shule kwa kukosa ada, nao pia wameingizwa katika kundi la kusaidiwa.

Aidha kundi hilo la watumishi wa Mungu kutoka Congo ambalo lilikuja maalumu kwa ajili ya kongamano la maadili lilihutubiwa na Askofu Paulin Mwewa, mwenye utajiri mkubwa wa viwanda na mmiliki wa migodi Congo, lilikuwa na nia ya kuhubiri waafrika kumuamini Mungu bila kumsubiri mzungu kutoa mafundisho.

Askofu Mwasota alisema kuwa kongamano hilo ambalo limeisha juzi, lilikuwa na msisimko mkubwa, na ilikuwa ajabu ukumbi wa PTA Sabasaba kujaa watu tofauti na ilivyodhaniwa.

Kongamano hilo lililoandaliwa na watumishi hao kwa kushirikiana na Umoja wa Makanisa ya Kipentekosti nchini (CPT) lilikuwa na lengo la kutoa mafundisho ya kiroho ya kuacha kutegemea wazunguu pekee, ambapo mada mbalimbali zilitolewa ikiwa ni pamoja na mafundisho ya ndoa kwa maadili ya kiafrika na maandiko ya biblia na namna ya kujikwamua kiuchumi.


CHANZO:MAJIRA

No comments: