ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, May 14, 2011

Z`bar yafungua ofisi za kutangaza utalii Dubai

Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (GNU) imeamua kufungua ofisi za kutangaza sekta ya utalii Zanzibar katika nchi za Sharja na Dubai, kwa kushirikiana na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), imefahamika.
Hayo yalielezwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Issa Ahmed Othman, alipokuwa akizungumza na NIPASHE kuhusu maonyesho ya utalii ya kimataifa yaliyofanyika Dubai na kuhudhuriwa na wajumbe kutoka Tanzania.
Alisema hatua ya kuwa na ofisi katika nchi hizo itasaidia kuhamasisha watalii kutoka Falme za Kiarabu na Mashariki ya mbali kutembelea vivutio vya utalii Tanzania ikiwemo Zanzibar.

Alisema maonyesho ya mwaka huu, yatasaidia kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea Zanzibar kutoka Ulaya na Mashariki ya Kati baada ya mashirika ya ndege kukubali kurejesha huduma ya moja kwa moja kati ya nchi hizo na Zanzibar.
Hata hivyo, alisema Shirika la Ndege la Oman Air tayari limekubali kurejesha huduma zake Zanzibar hatua ambayo itasaidia kuimarisha sekta ya biashara na utalii visiwani.
Alisema lengo la Zanzibar ni kuona sekta ya utalii inachangia asilimia 50 ya pato la taifa hadi ifikapo 2020 kutoka asilimia 25.
CHANZO: NIPASHE

No comments: