ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, May 17, 2011

Zitto azuru kaburi la Amina Chifupa

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (aliyechuchumaa) akiwa na wabunge wa Viti Maalum, Raya Ibrahimu (kushoto) na Joyce Mukya wakiwa katika kaburi la Marehemu Amina Chifupa aliyekuwa mbunge wa CCM kupitia Vijana, walipotembelea katika kijiji cha Lupembe, mkoani Njombe jana. Picha na Edwin Mjwahuzi
Mwandishi Wetu
MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema jana alizuru kaburi la Mbunge wa zamani wa Viti Maalumu-Vijana wa CCM, marehemu Amina Chifupa, katika Kijiji cha Lupembe, Iyanjo, wilayani Njombe.
Zitto alizuru kaburi hilo akiwa katika ziara ya mikutano ya hadhara ya Oparesheni Sangara na maandamano ya chama chake, ambayo sasa ipo katika Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, ikiwa na lengo la kupinga ongezeko la gharama za maisha. Jana alikuwa akitembelea Jimbo la Njombe Kaskazini kufanya mikutano katika vijiji vya Lupembe, Kidegembye na Mtwango.
Kabla ya kuanza mkutano wa kwanza katika Kijiji cha Lupembe, Zitto aliyeambatana na wabunge wa Viti Maalumu wa Chadema, Raya Ibrahim Khamis na Joyce Mukya waliamua kwenda kuzuru kaburi la marehemu Amina kwa ajili ya kumwombea dua.

Amina alifariki dunia Juni 26, 2007 na kuzikwa Juni 28 mwaka huo kijijini hapo mkoani Njombe.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Lupembe, Zitto alisema: "Nashukuru sana kufika katika kijiji chenu kwani nimefarijika kufika mahali alipozikwa marehemu Amina Chifupa".
"Amina alikuwa rafiki yangu sana, tulikuwa tukipambana katika Bunge la 9 la Jamhuri ya Muungano katika kutetea haki za vijana wa nchini."
"Kwa bahati mbaya sikupata nafasi ya kushiriki katika mazishi yake, leo ndiyo mara yangu ya kwanza kufika kaburini kwake," alisema Zitto.
Wakati wakiomba dua kaburini hapo, Mukya alishindwa kujizuia na kuanza kutokwa na machozi huku akisema: "Kwa kweli sitamsahau Amina kwa mambo matatu. Alikuwa mjasiri, mwenye upendo na alijitolea kuisaidia jamii pale alipotakiwa kufanya hivyo au kwa ridhaa yake mwenyewe."
"Amina alikuwa mpambanaji bungeni japokuwa alikuwa na umri mdogo kuliko wabunge wote, aliweza kujitoa kupambana na wauzaji wakubwa wa dawa za kulevya bila woga."
Mbowe adai CCM janga la taifa
Chadema kimeendelea kukishambulia CCM kwa kuwaeleza wananchi kuwa chama hicho tawala ni janga la kitaifa kwa kuwa kimekuwapo madarakani kwa miaka mingi lakini kimeshindwa kuwasaidia wananchi kuondokana na umaskini.
Akiwahutubia wananchi wa Makambako katika Uwanja wa Polisi, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema "Tumesema ni lazima tuiwajibishe serikali kwa kufanya maandamano na kuwaamsha CCM na serikali yao ambayo imeweka pamba masikioni. Inabidi ilazimishwe kwa maandamano na nguvu ya umma ili iwapunguzie wananchi makali ya maisha."Alisema kama si maandamano ya Chadema, Serikali ilikuwa tayari kuilipa Dowans wakati hali ni mbaya kwa wananchi.
Nape ang'ang'ana na Dk Slaa
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, amemtaka Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, ajitokeze mwenyewe hadharani awaambie Watanzania kwa nini alikubali mshahara wa Sh7.5milioni wakati aliupinga ule wa Bunge wa Sh 7 milioni.Akizungumza katika Ofisi Ndogo za CCM Mtaa wa Lumumba, Dar es Salaam jana, Nape alisema Dk Slaa ni bingwa wa kujibu tuhuma zinazoelekezwa kwake hivyo ni vyema akijibu na hilo na kuacha kutumia wale aliowaita vibaraka.
"Dk Slaa analipwa mshahara huo Sh7.5milioni wa ukatibu mkuu wa Chadema, lakini mwaka mmoja kabla na wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa rais, alipita mikoani akipinga mshahara wa mbunge wa Sh 7milioni, akisema unaongeza pengo la kipato kwa watumishi," alisema Nnauye na kuongeza kuwa kupiga chenga kwa Dk Slaa kwa kushindwa kujibu hoja hiyo hakutamsaidia kwani Watanzania wa sasa wameamka.
"Hoja ya msingi ni msimamo wa Dk Slaa kuhusu pengo la mishahara kwa Watanzania... yeye alisema ana huruma sana lakini amekubali kupokea mshahara zaidi ya ule wa mbunge, halafu hajibu hoja. Kwa nini atumie vibaraka kusema maneno ya kutunga?"
"Nilisema ukiwa kwenye nyumba ya vioo usirushe mawe. Kuna watu wanadhani hawagusiki sasa tumewagusa. Ajitokeze sasa awaambie Watanzania kwa nini anapokea kiasi hicho wakati alikataa mwaka jana," alisisitiza Nape.

Msimamo wa Nec palepale
Akizungumzia msimamo wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec-CCM) katika kile kinachoitwa kujivua gamba, Nnauye alisema haujabadilika na wahusika lazima wawajibishwe.
Kwa mujibu wa msemaji huyo wa CCM, uamuzi wa Nec hauwezi kubadilishwa na mtu mmoja, bali chombo hicho chenyewe au mkutano mkuu.
Ajivunia mafanikio 
Akizungumzia ziara ya chama hicho mkoani Singida, Nnauye alisema sekretarieti iliridhika na utekelezaji wa Ilani ya CCM katika maeneo ya barabara, huduma za afya na maji.Alisema ujenzi wa hospitali kubwa ya rufaa umekuwa ukiendelea vizuri mkoani humo ambayo hadi kukamilika utagharimu jumla ya Sh80 bilioni.
Alisema CCM kimevuna wanachama 580 wa upinzani huku wapya waliokuwa hawana vyama wakiwa ni 188.
 Habari hii imeandikwa na Edwin Mjwahuzi, Njombe; Boniface Meena, Makambako na Ramadhan Semtawa, Dar.

CHANZO:MWANANCHI

No comments: