ANGALIA LIVE NEWS

Monday, July 18, 2011

Kikwete afanya ziara ya kihistoria Afrika Kusini

RAIS Jakaya Kikwete leo ameanza ziara ya kihistoria ya Kidola nchini Afrika Kusini, ikiwa ni ziara ya kwanza ya aina yake kufanywa na Rais wa Tanzania katika nchi hiyo.

Rais Kikwete anafanya ziara hiyo kwa mwaliko wa Rais Jacob Zuma ambaye utawala wake umekuwa karibu na kuwa na uhusiano mzuri na Tanzania tangu aliposhika madaraka ya kuongoza taifa hilo kubwa kiuchumi kuliko mengine yote katika Afrika. 


Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, Rais Kikwete na ujumbe wake ambao ni pamoja na Mama Salma Kikwete, uliondoka nchini leo mchana kwenda mjini Pretoria tayari kuanza ziara hiyo ya siku nne.

Pamoja na kwamba marais wa Tanzania waliomtangulia Rais Kikwete wametembelea Afrika Kusini mara nyingi kwa shughuli mbalimbali, lakini hakuna Rais wa Tanzania aliyewahi kualikwa kufanya ziara rasmi, ya Kiserikali ama ya Kidola, tangu nchi hiyo kuingia katika mfumo wa demokrasia mwaka 1994.

Kwa mujibu wa ratiba ya ziara hiyo, Rais Kikwete, Mama Salma Kikwete na ujumbe wa Tanzania watapokewa rasmi kesho asubuhi kwenye Jumba la Serikali mjini Pretoria na Rais Zuma na mkewe tayari kwa sherehe ya makaribisho ambazo zitafuatiwa na mazungumzo rasmi ya Kiserikali kati ya Tanzania na Afrika Kusini.

Baada ya mazungumzo rasmi yatakayofuatiwa na utiaji saini wa mikataba na makubaliano katika nyanja mbalimbali kati ya nchi hizo, viongozi hao wawili watahutubia mkutano wa waandishi wa habari. Baadaye, Rais Kikwete atatembelea Uwanja wa Uhuru akiandamana na Rais Zuma.

Kesho mchana, watakula chakula cha mchana cha wafanyabiashara wa Tanzania na Afrika Kusini ambako watazungumza kuelezea umuhimu wa kuimarisha uhusiano wa kibiashara na kiuchumi kati ya nchi hizo.

Kesho jioni, Rais Zuma ataandaa dhifa ya kitaifa kwa ajili ya Rais Kikwete na ujumbe wake kwenye Nyumba ya Wageni ya Rais wa Afrika Kusini ambako Rais Kikwete atafikia wakati wa ziara hiyo.

Keshokutwa, Rais Kikwete na ujumbe wake watakwenda Cape Town ambako miongoni mwa mambo mengine ujumbe huo utatembelea Kisiwa cha Robben ambako wapigania uhuru maarufu wa Afrika Kusini, akiwemo Rais mstaafu Nelson Mandela, walifungwa kwa miaka mingi na makaburu.

Habari Leo

No comments: