ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, July 13, 2011

Maelezo ya Mbunge Lema hayatatolewa

Ofisi ya Bunge imesema ushahidi uliotolewa na Mbunge wa Arusha Mjini, (Chadema), Godbless Lema, kuwa Waziri Mkuu amelidanganya Bunge kuhusiana na mauaji ya Arusha, hauwezi kutolewa uamuzi kwa sababu suala hilo bado liko mahakamani.
Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel, ameliambia NIPASHE mjini hapa kuwa kesi ya msingi bado iko mahakamani, kufanya maamuzi yoyote juu ya suala la Lema ni kuingilia uhuru wa Mahakama.

Hivi karibuni Lema alilalamikia kuchelewa kutolewa uamuzi utetezi wake na kuongeza kwamba Spika wa Bunge, Anne Makinda, hamtendei haki.
Alisema yuko radhi kuchagua kupigwa risasi kuliko kufuta kauli yake aliyotoa bungeni kuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alilidanganya Bunge kwa kuwa ana ushahidi kwa asilimia 100 na ana uhakika nao.
Lema aliingia matatani Februari 10, mwaka huu alipoomba mwongozo wa Spika baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu, siku ya Alhamisi ambayo Waziri Mkuu alikuwa amejibu maswali ya papo kwa papo akitaka kujua mbunge anaweza kuchukua hatua gani iwapo atagungua kuwa kiongozi mkubwa kama Waziri Mkuu amelidanganya Bunge.
Spika Mkinda alikuwa mkali na kumtamka kuwa inaelekea bunge linataka kukosa adabu. Alimwambia Lema kuwa kwa kauli yake ya kuomba mwongozo wa Spika alikuwa anamaanisha kuwa Waziri Mkuu alikuwa anasema uongo.
Makinda alimtaka Lema kuthibitisha kauli hiyo na kumpa siku tano hadi Februari 15 awe amewasilisha ushahidi wake kwamba Waziri Mkuu alisema uongo bungeni, jambo ambalo alilifanya.
Hata hivyo, pamoja na kuwasilisha utetezi huo, Makinda hakuutolea uamuzi wakati wa Mkutano huo wa Pili Februari mwaka huu hadi leo bila kueleza sababu za kutokufanya hivyo.
MAKINDA BADO KUJADILIWA
Katika hatua nyingine, Ofisi ya Bunge imesema Kamati ya Kudumu ya Kanuni za Bunge imechelewa kukutana kusikiliza malalamiko dhidi ya Spika Makinda, kutokana na wajumbe wengi kutokuwepo bungeni.
Joel alisema huenda kamati hiyo ikaketi wiki hii baada ya wajumbe wengi kurejea.
“Naona wabunge wameanza kurejea bungeni natarajia wiki hii huenda tukakaa,” alisema bila kueleza walikuwa wamekwenda wapi. Hivi karibuni, Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, aliwasilisha kwa Katibu wa Bunge malalamiko dhidi ya uamuzi wa Spika wa kumkataza Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kujibu bungeni swali lake kuhusu mauaji yaliyofanywa na askari wa Jeshi la Polisi dhidi ya wananchi katika maeneo ya Mgodi wa dhahabu wa North Mara, Nyamongo, katika Wilaya ya Tarime, mkoani Mara.
Spika Makinda alimkataza Pinda kujibu swali hilo kwa hoja kwamba suala hilo liko mahakamani.
Spika Makinda alichukua uamuzi huo wakati wa kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu, bungeni, Juni 26, mwaka huu.
Lissu, ambaye pia ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alisema waraka wa malalamiko hayo umezingatia kanuni ya 5 (4) ya kanuni za kudumu za Bunge ya mwaka 2007.
Kanuni hiyo inatamka kwamba: “Mbunge yeyote ambaye hataridhika na uamuzi wa Spika anaweza kuwasilisha sababu za kutoridhika kwake kwa Katibu wa Bunge ambaye atawasilisha malalamiko hayo kwa Spika.”
Kwa mujibu wa kanuni ya 5 (5) na (6), baada ya malalamiko hayo kuwasilishwa kwa Katibu wa Bunge, kitakachofuatia ni Spika kuwajibika kuitisha kikao cha Kamati ya Kanuni za Bunge na kulijulisha Bunge kuhusu uamuzi utakaotolewa na kamati hiyo.
Tayari Spika Makinda alikwishaweka wazi msimamo wake kwamba yuko tayari kuhojiwa na kamati hiyo iwapo ataitwa.
Lissu alitoa sababu kuu mbili. Ya kwanza ni kwamba, swali alilomuuliza Waziri Mkuu siku hiyo halikuhusu jambo lolote, ambalo linasubiri uamuzi wa mahakama yoyote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Sababu ya pili, alisema kesi namba 210 ya mwaka 2011 inayomhusu yeye pamoja na washtakiwa wengine saba katika Mahakama ya Wilaya ya Tarime, haina uhusiano wowote na masuala ya Nyamongo.
Lissu alisema katika malalamiko yake kuwa hoja ya kuhusisha kesi yake na masuala ya Nyamongo, iliibuliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, bungeni siku hiyo, wakati haikuwa sahihi.
Pia alisema yeye pamoja na Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Esther Matiko, hawakabiliwi na kesi yoyote ya jinai inayohusu jambo lolote lililotokea mahali popote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Vilevile, alisema kesi dhidi yake na wenzake, haina uhusiano na eneo la Nyamongo yalikotokea mauaji Juni 16, mwaka huu na hata siku ya nyuma.
Anasema nakala ya hati ya mashtaka, inaeleza bayana kuwa yeye na wenzake wameshtakiwa kwa makosa matatu.
Makosa hayo ni pamoja na kuingia kwa kijinai katika eneo la kuhifadhia maiti la Hospitali ya Serikali ya Tarime saa 4 usiku, Mei 23, mwaka huu; kufanya mkusanyiko usiokuwa halali katika eneo hilo hilo na kwa muda huo huo.
Lingine ni kumzuia mganga na askari na polisi kutimiza wajibu wao kwa kuwazuia kufanya uchunguzi wa maiti za watu wanne.
CHANZO: NIPASHE

No comments: