ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, July 13, 2011

Zitto aijia juu serikali kuhusu umeme

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, (Chadema), Zitto Kabwe, ameibana serikali kwa kutosema ukweli kuhusiana na mashine za kufulia (process) gesi zinazomilikiwa na Kampuni ya Pan Africa ambazo amedai kuwa zina kutu.
Zitto alisema kuwa suala la umeme nchini limekuwa kizungumkutu ambapo wabunge na wananchi wamekuwa wakilalamikia kuhusiana na tatizo hilo.
Alisema taifa limepoteza fedha nyingi na kwamba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imesema imepoteza mapato ya Sh. bilioni 840 hadi kufika Mei.

Alisema kuna tatizo kubwa la serikali kutosema ukweli na kutoa mfano wa wakati wa Songas serikali ilisema kuwa kuna ukarabati na kwamba baadaye iligundulika kuwa zile mashine za kufulia umeme Songas zina kutu.
Hata hivyo, alisema serikali haikusema na hadi sasa haijasema ukweli kuhusiana na jambo hilo na kuhoji kwanini serikali imewaficha Watanzania haijasema ukweli.
Zitto alihoji pia kwanini Waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja, na Naibu wake Adam Malima, bado wanaendelea kuwepo katika wizara hiyo.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Malima, alisema Januari mwaka huu alikwenda eneo hilo na kugundua tatizo si mashine za kufulia gesi bali ni visima.
Alisema visima hivyo viwili SS 5 na SS 8 viliwekwa mwaka 2004 na kwamba matarajio yake ni kuwa visima hivyo vingekuwa na uhai hadi miaka 12, lakini kuna chemical component Songosongo ambayo ilifanya vikapata kutu.
Alisema visima hivyo vilifungwa na kufunguliwa kwa kisima kingine kipya cha SS 10 ambacho kina uwezo wa kufua gesi nyingi kuliko vile vya awali.
CHANZO: NIPASHE

No comments: