
NAAM, kama ilivyo ada tumekutana tena kwenye kona yetu ya Uhusiano na Mapenzi, ili kujazana machache kuhusiana na maisha yetu ya kila siku ambayo yametawaliwa na mapenzi kwa asilimia kubwa.
Kumekuwa na kasumba kubwa katika mapenzi ya kileo kwa mtu kumburuza mpenzi wake, kisa amejua anapendwa. Hii imefanya watu wengi kuteswa na mapenzi kutokana na wapenzi wao kutoonyesha ushirikiano.
Kumekuwa na kasumba kubwa katika mapenzi ya kileo kwa mtu kumburuza mpenzi wake, kisa amejua anapendwa. Hii imefanya watu wengi kuteswa na mapenzi kutokana na wapenzi wao kutoonyesha ushirikiano.
Kutokana na mizunguko yangu ya kila siku, nimekutana na maneno mengi ya majisifu kutoka kwa wanawake, mfano unakuta mmoja anajiona mzuri kupindukia kwa mwanamume aliyenaye ambaye ameonyesha anampenda.
Utamsikia mtu akisema; kwangu hapindui chochote nikitakacho hunipatia, hata ninapofanya makosa akiniuliza humjia juu na yeye anafunga mdomo au yeye kuniomba msamaha.
Lazima hili mlifahamu kuwa mapenzi ni kikohozi siku zote ‘limkamatalo kulificha hawezi’. Mwenye mapenzi ya kweli anapopenda lazima atakuonyesha wazi na kukupatia kile ukitakacho, lengo likiwa ni kukuridhisha mpenzi wake.
Sisemi asiye na kitu hawezi kuonyesha mapenzi, bali wewe ndiye unayetakiwa kujua uwezo wa mpenzi wako na kuomba kilicho ndani ya uwezo wake. Siyo utumie upendo wake kwako kulazimisha mambo.
Tatizo linakuja kwa yule anayependwa kwa kuamini ule ndiyo muda wa kumburuza ukifikiri hakuna chochote kilicho kizuri mbele yake zaidi yako.
Ni wazi wengi huwa hawajui kuwa mapenzi ni kitu kilicho wazi kama glasi, kupata mpenzi ni sawa na ndege aliyechagua mti ili apumzike na akiona mti ule si mapumziko mema basi ndege yule huruka na kutafuta mti mwingine.
Ndege mwenye mapenzi hujenga kiota na kuhamishia makazi yake pale na kuwa ya kudumu, ila ndege mpitaji akiisha pumzika huanzisha safari nyingine hata katika mapenzi.
Kumbuka unapopata mpenzi na kuwa tayari kukupa kila ukitakacho hata kikiwa nje ya uwezo wake, lazima ujione ni mtu mwenye bahati kwani dunia ya leo kupata penzi la kweli ni adimu kama maji jangwani.
Kuutumia upendo wa mpenzi kama fimbo ya kumpigia ni kosa kubwa kwa kiumbe chenye moyo wa nyama ambacho nacho huumia pale kinaponyimwa haki yake ya msingi.
Pia ni kosa kubwa upendo wa mwenzako kuugeuza kama kitega uchumi au ni sehemu ya kumburuza mwenzio, ni makosa sawa na kumshika mkono kipofu wakati wa kula.
Siku akipata mwenye mapenzi ya kweli, anayehitaji mapenzi yasiyo na gharama wala mateso ataondoka bila kuaga.
Siku zote mbegu ya mapenzi haiwezi kuota kwenye moyo usio na rutuba ya mapenzi.
Kwa kipindi ulichokuwa naye hukuona thamani yake lakini akiondoka ndipo utakapojuta, sijui kama atakuwa tayari kurudiana na wewe.
Akukumbuke kwa lipi, kwa mateso na penzi la gharama? Natumia kalamu yangu kuwaomba wote wenye wapenzi wa kweli wawatumie vizuri wapenzi wao kwa penzi lenye kuonyesha unathamini kile ulichonacho.
Jiepushe na penzi la kukutana bar na kuachana nyumba ya wageni. Tumia upendo wa mwenzako kujijenga kimaisha na si kutumia uzuri wako. Utakuja kukumbuka shuka kumekucha.
KWA HAYO MACHACHE TUKUTANE WIKI IJAYO.
No comments:
Post a Comment