ANGALIA LIVE NEWS

Monday, July 18, 2011

Shibuda, umeya wa Arusha ngoma nzito

Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda
Kamati Kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) imeukataa mwafaka wa umeya wa Jiji la Arusha uliofikiwa na madiwani wa vyama vya CCM, Chadema na TLP.
Chadema kiliupinga ushindi wa Gaudence Lyimo wa CCM kwa madai kuwa uchaguzi huo ulikiuka kanuni.

Januari 5, mwaka huu, chama hicho kilifanya maandamano jijini Arusha kupinga uchaguzi huo, lakini Jeshi la polisi liliingilia kati na kuyavunja maandamamo hayo, hatua iliyosababisha vurugu na kuuawa kwa watu watatu.
Hata hivyo, Juni 20, mwaka huu, madiwani hao walitangaza kufikia mwafaka wa umeya kwa kumtambua Lyimo.
Pamoja na kukubaliana kugawana kamati mbalimbali za Halmashauri ya Jiji, pia ilikubaliwa kuwa Diwani wa Chadema, Estomiah Mallah, ashike unaibu umeya hadi mwaka 2014 na baadaye diwani wa TLP ashike unaibu meya hadi Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Siku chache baadaye, Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema, alitangaza kutoutambua mwafaka huo kwa maelezo kuwa taratibu na kanuni vilikiukwa na kuwa chama hakikuhusishwa.
Juni 29, mwaka huu, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, alitangaza kuunda kamati ya watu watatu ikiongozwa na Mjumbe wa Kamati Kuu, Mabere Marando, kuwachunguza madiwani wa chama hicho waliohusika katika mazungumzo ya mwafaka na kuipa siku sita. Alisema watakaobainika kuhusika watachukuliwa hatua.
Habari ambazo NIPASHE ilizipata jana usiku kutoka ndani ya kikao cha kamati kuu kilichokuwa kikifanyika jijini Dar es Salaam, zilieleza kuwa Kamati Kuu imeukataa mwafaka huo rasmi.
Hata hivyo, hakuna kiongozi yeyote aliyethibitisha taarifa hizo rasmi. Hakuna aliyepatikana kuzungumza kwa kuwa kikao kilikuwa kikiendelea.

SHIBUDA SI RIZIKI
Wakati huo huo, habari kutoka ndani ya kikao hicho, zinaeleza kuwa hatima ya Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda, ndani ya chama hicho iko katika wakati mgumu.
Ugumu wake unatokana na Shibuda hadi jana kutoandika barua ya kumuomba radhi Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani, Tundu Lissu, ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki. Aidha, Shibuda ameenedelea kutoa kauli za utovu wa nidhamu nje ya chama.
Shibuda anatuhumiwa kwenda kinyume na azimio lililotolewa na chama hicho la kuwakataza wabunge wake kupokea posho za vikao vya Bunge.
Kwa mujinu wa chanzo chetu ndani ya kikao hicho zinaeleza kuwa wajumbe hawaoni sababu za kutomchukulia hatua Shibuda kwa kuogopa kupoteza jimbo.
Katika kikao cha Kamati Kuu jana, moja ya ajenda ilikuwa ni kumjadili kwa kina Shibuda na kutoa maamuzi ya hatua za kumchukulia kwa kwenda kinyume na taratibu za chama.
Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya ufunguzi wa kikao hicho, Mwenyekitiki wa Chadema, Freeman Mbowe, alithibitisha kuwa kikao hicho kingemjadili Shibuda na kutoa maamuzi.
Alisema Chadema hakina nia ya kumkandamiza mtu wala mwanachama wake yoyote, bali kinachowaongoza ni katiba yao na kanuni mbalimbali walizojiwekea.
Mbowe alisema mtu yoyote anayekwenda kinyume na misingi ya chama hicho lazima wajibishwe kikamilifu bila uoga wala uonevu.
“Lazima chama kiwe na nidhamu na mtu yoyote anayekwenda kinyume cha hapo chama kitamchukulia hatua haraka iwezekanvyo,” alisema Mbowe.
Shibuda alianza kwenda kinyume na msimamo wa Chadema baada ya kutangaza hadharani bungeni kwamba ataendelea kupokea posho za vikao kama wabunge wa Chadema wakizikataa na kukejeli msimamo wa chama na kusema anatamani kiasi kiongezwe kutoka Sh. 70,000 hadi Sh. 500,000 kwa siku.
Hivi karibuni, Lissu, alimwandikia Shibuda barua ya kumtaka ajieleze kuhusiana na kauli yake inayokwenda kinyume na msimamo wa chama hicho kuhusu posho.
Hata hivyo, Lissu alisema kuwa barua hiyo ilikuwa ikimsubiri Shibuda ili akabidhiwe kwa kuwa alikuwa nje ya Bunge kwa siku kadhaa.
Kabla ya kujiunga na Chadema, Shibuda alikuwa mbunge wa jimbo hilo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na aliondoka baada kushindwa kwenye kura za maoni ndani ya chama hicho.
Hadi tunakwenda mitamboni kikao hicho kilikuwa kinaendelea. Hata hivyo, Mbowe alisema chama kitatoa taarifa wakati wowote baada ya kikao kumalizika.
CHANZO: NIPASHE

No comments: