ANGALIA LIVE NEWS

Monday, August 1, 2011

Aliyeoa waume wawili atamani ndoa kanisani

MWANAMKE aliyeoa waume wawili, Veronica Saleh (50) au Mama Kaela, amesema anatamani kufunga ndoa ya kanisani na waume zake, lakini anaonewa na kwa sasa anafikiria kufunga ndoa serikalini.

Veronica alitoa kauli hiyo wiki iliyopita alipozungumza na gazeti hili kuhusu uhusiano wa familia yake na Kanisa Katoliki pamoja na ndugu wa waume zake.

“Nina hamu kubwa sana kufunga ndoa kanisani lakini wananionea kwa kuwa wamenikatalia, sasa sijui kama watanikubalia kufunga ndoa ya kimila au kiserikali. 


“Watoto wangu kila Jumapili tunaenda kusali ila huyu mtoto wetu mdogo (Willston, 7) bado mpaka sasa hajabatizwa wametukatalia,” alisema mama huyo bila kutoa ufafanuzi wa kauli hiyo.

Katekista wa Kigango cha Kanisa Katoliki cha Parokia ya Uruira, katika Jimbo la Mpanda, Mashaka Abel alithibitisha kuwa mama huyo pamoja na watoto wake wote hawajazuiliwa kuhudhuria ibada kanisani humo.

Hata hivyo, alisema Veronica na mumewe mdogo, Arcado Mlele (45) ambaye ni Mkatoliki pia wanakosa huduma muhimu za kiroho ikiwemo ya kushiriki chakula cha bwana. Mume mkubwa Paulo Sabun (60) au Baba Kaela ni muumini wa makanisa ya Pentekoste.

Ndoa ya Veronica pia si rahisi kufungwa kiserikali au kimila kwa kuwa tayari ndoa hiyo imesababisha utata katika Sheria ya Ndoa na ndugu wa Arcado wanasema ndugu yao kawadhalilisha kama familia.

Kwa mujibu wa baadhi ya wanasheria waliozungumza na gazeti hili wiki hii, wanasema Veronica anaweza kushitakiwa kisheria na wengine wanasema hakuna sheria inayombana kwa kuwa wakati Sheria ya Ndoa ikitungwa, hakukuwa na tukio la mwanamke kuoa, achilia mbali kuoa waume wawili.

Profesa mmoja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wa zamani, ambaye hakutaka kutajwa jina alisema, sheria ikisema wanaume wanaweza kuoa mke zaidi ya mmoja, haimaanishi kuwa mwanamke mmoja anakatazwa kuolewa na mume zaidi ya mmoja.

Msomi huyo alisema ndoa hiyo ni vyema ikachukuliwa kama changamoto kwa kuwa siku za nyuma haikuwepo.


Hata hivyo, Mwanasheria Maarufu, Majura Magafu alisema kisheria na kawaida mwanamume ndiye anayeruhusiwa kuoa wake zaidi ya mmoja na si kinyume chake. Ndani ya Kanisa Katoliki baadhi ya waumini wamekuwa wakiomba uongozi wa juu wa kanisa hilo kumtenga mama huyo.

Waumini hao wamekuwa wakidai analidhalilisha Kanisa mpaka pale atakapojirudi na kufunga ndoa na mume mmoja kanisani hapo.

Familia ya mume mdogo nayo imekuwa ikipinga ndoa hiyo ambapo baadhi ya ndugu wa karibu wa Arcado wamelaani kitendo cha ndugu yao kuolewa na Veronica, wakidai kuwa ameidhalilisha familia yao.

Arcado ni mkazi wa kijiji cha Ikondamoyo kilicho umbali wa takribani kilometa 30 kutoka mjini Sumbawanga katika Jimbo la Katavi linalowakilishwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Wanandugu hao walioomba kutoandikwa majina yao gazetini walieleza kuwa wanakerwa na uamuzi mgumu wa ndugu yao Arcado, wa kuachana na mkewe anayefahamika kijijini hapo kama Mama Pere na kuamua kuolewa na Veronica.

Kwa mujibu wa ndugu hao, walishamshauri Arcado na kumuahidi kuwa endapo ataachana na Veronica, watamwozesha mwanamke mwingine, lakini yeye akadai kuwa yuko tayari kufa, lakini si kuachana na Veronica kwani ndiye ubavu wake wa maisha.

“Sasa tumebaki tunamwangalia tu huyu ndugu yetu Arcado, tumemshauri, lakini mkaidi, hatusikilizi. Basi nasi hatuna la kufanya zaidi ya kumwangalia,“ alisema mmoja wa ndugu hao. Hata hivyo ukiacha changamoto hizo, ndoa hiyo imedumu kwa miaka saba sasa huku wanandoa hao wakipendana jambo linalosababisha uhusiano huo kutokuwa na mgogoro wa mara kwa mara.

Veronica alipoulizwa alisema ana watoto wanne, Alfred (20), binti mwenye miaka 16 (ambaye ameolewa) na wengine wawili wa kiume, mmoja akisoma darasa la sita na mdogo, Willston ana miaka saba na amesisitiza hana shida na waume wake. Changamoto kubwa iliyowahi kutokea ni wakati wa ubatizo wa Willston ambapo waume wa mama huyo kila mmoja alidai ni mtoto wake.

Katekista Abel alisema familia hiyo ilishindwa kumbatiza mtoto huyo baada ya wazazi wa kiume kumgombania mtoto huyo kanisani.

“Mtoto huyo (Willston) akiwa na umri wa mwaka mmoja, alifanyiwa utaratibu wa ubatizo, lakini ilishindikana, kutokana na wanaume hao, kila mmoja kudai ndiye baba mzazi wa mtoto.

“Familia ilifanya maandalizi yote ya sherehe ya ubatizo wa mtoto huyo, lakini siku hiyo kanisani wakati huo ilikuwa ni Kigango cha Katumba ambacho sasa ni Uruira, sakata likaanzia mbele ya Padri.

“Padri alimwuliza mama wa mtoto huyo ubini wa mtoto naye akasema ni Mlele (jina la mume mdogo Arcado, 45) lakini mume mkubwa, Paulo Sabuni (60) au Baba Kaela ambaye ni muumini wa makanisa ya Pentekoste, alisimama na kupinga kwa kudai kuwa mtoto yule si wa Arcado bali wake na yeye ndiye baba halali,” alisema Abel.

Kwa mujibu wa maelezo ya Katekista huyo, ambaye katika Kanisa Katoliki ni mwalimu wa dini, Padri huyo hakuamini, akauliza tena na tena na majibu yakawa ni yale yale; “ndipo ubatizo ukashindikana.”

Mwananchi

No comments: