Maduka matatu yametekezwa kwa moto usiku wa kuamkia mjini juzi Zanzibar na kusababisha hasara ya mamilioni ya fedha.
Bidhaa aina mbalimbali zikiwemo nguo, vipodozi na vitu vya urembo, ni miongoni mwa mali zilizoteketea katika maduka hayo ambayo pia ni makazi ya wamiliki wa maduka hayo usiku wa kumkia juzi.
Abdulkarim Yakub, mmoja wa wamiliki wa maduka hayo alisema maduka hayo yalikuwa ndani ya jengo la ghorofa moja katika eneo la Kiponda karibu na mtaa maarufu wa biashara mjini Zanzibar wa Darajani.
Alisema yeye alikuwa anamiliki duka kubwa la sonara lililokuwa na vitu vya urembo vyenye thamani ya mamilioni ya fedha.
“Tumepata hasara kubwa, kila kitu kimeungua,” alisema," Abdukarim.
Alisema mali nyingine za dukani zilikuwa ghorofani katika nyumba ya kuishi pamoja na mali nyingine za matumizi ya nyumbani.
Msemaji wa duka lingine lililoungua la Warda Saleh, alisema lilikuwa limejaa vipodozi vya aina mbali mbali na kwamba moto huo ulianza usiku wa kuamkia juzi saa 4:30 usiku.
Hata hivyo, msemaji huyo hakuweza kukadiria hasara iliyosababishwa na moto huo kwa duka lake, lakini alisema imemgharimu mamilioni ya fedha kupata mali zilizokuwa ndani ya duka hilo.
Mmiliki wa duka la nguo, Ismail Daud, alisema mali zilizokuwa dukani na katika vyumba vya kuishi ghorofani juu ya duka hilo zote zimeteketea.
Wamiliki wa maduka yote walisema chanzo cha moto huo ni hitilafu ya umeme.
Walisema hitilafu hiyo ilifuatiwa na mlipuko wa compresa ya chombo cha kuhifadhia gesi kilichokuwa kimewekwa nyuma ya jengo la duka la vipodozi.
Juhudi za kuzima moto zilianza dakika 30 baada ya maduka hayo kushika moto saa 4:30. Zaidi ya magari matano ya Kikosi cha Zimamoto yalifika katika eneo la tukio.
Idadi ya watu waliokuwa wanaishi kwenye ghorofa za maduka hayo haikuweza kufahamika mara moja, lakini wote kwa sasa hawana makazi.
Jumuiya ya Wazekezaji kwenye Utalii (Zati) imekipongeza kikosi cha zimamoto kwa kuwasili kwa wakati katika tukio hilo.
Mwenyekiti wa Zati, Abdul Samad, alisema utendaji wa kikosi hicho umeokoa maisha ya watu na mali zao, lakini kikubwa zaidi hatua hiyo imeweza kuunusuru Mkongwe kwani bila moto huo kuzimwa kwa wakati umepata madhara makubwa.
Abdul alisema mji huo ni kivutio kikubwa kwa shughuli za kitalii visiwani Zanzibar, hivyo utendaji wa kikosi hichoi umelinda hazina ya utalii wa Zanzibar.
Miongoni mwa waliowatembelea waathirika wa tukio hilo ni pamoja na Mwakilishi wa Mjimkongwe, Islmail Jussa Ladhu na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohammed Aboud Mohammed.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment