Katibu Mkuu Nishati na Madini, David Jairo ofisini kwake Agosti 24. (Picha na Evance Ng’ingo). |
Makinda ameiagiza kamati hiyo ifanye kazi kwa muda usiozidi wiki nane na anatarajia kwamba itafanya kazi kwa kuzingatia Katiba ya nchi, sheria na taratibu, na itatoa haki kwa watu wote.
Amewataja wajumbe wa kamati hiyo kuwa ni Mbunge wa Tunduru Kaskazini, Ramo Makani (CCM), Mbunge wa Karagwe, Gosbert Blandes (CCM), Mbunge wa Karatu, Mchungaji Israel Natse (Chadema), Mbunge wa Gando, Khalifa Suleiman Khalifa(CUF), na Mbunge wa Viti Maalum, Martha Umbula (CCM).
Makinda amewaeleza wabunge kuwa, kamati hiyo inapaswa kuchunguza utaratibu uliotumika kukusanya fedha kwa ajili ya kufanikishwa kupitishwa bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, sanjari na uhalali wa utaratibu huo kisheria na kikanuni.
Kamati hiyo inapaswa pia kuchunguza kama fedha zilizokusanywa zinakasimiwa katika bajeti husika, na ichunguze matumizi halisi ya fedha zilizokusanywa.
Makinda ameiagiza kamati hiyo ichunguze taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu uchunguzi kuhusiana na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini kukusanya fedha katika idara zilizo chini ya Wizara hiyo kwa ajili ya kufanikisha kuwasilisha bajeti ya Wizara hiyo.
Kamati hiyo pia inapaswa kuchunguza mfumo wa Serikali kujibu hoja zinazowasilishwa bungeni, na kubaini kama utaratibu huo unaathiri dhana ya madaraka ya Bunge.
Makinda kaagiza pia kwamba, kamati iangalie nafasi ya mamlaka ya uteuzi kwa ngazi ya makatibu wakuu katika kushughulikia masuala ya kinidhamu kwa anaowateua na pia kuangalia mambo mengine yoyote yanayohusiana na mambo hayo.
Amewasifu wabunge kwa kufanya kazi nzuri katika mkutano wa Bunge uliokwisha leo mjini Dodoma, na kwamba walivumiliana, walisikilizana na kufanya kazi pamoja.
Am esema, Bunge hilo lilipoanza lilianza kama Ze Comedy, lakini linaelekea kuwa imara, na litafanya kazi ipasavyo kuisimamia Serikali.
Amewataka wabunge wasiwe na chuki au uadui na wanaoongoza vikao vya Bunge, kwa kuwa hakuna aliye na chuki na yeyote.
“Chuki na hila mziache hapa, na ziozee humu…mkiwa hapa mwenzio akisema usijenge uadui.. kwa waliokwazwa naomba tusameheane” amesema Makinda kabla ya kusitisha shughuli za Bunge hadi Novemba 8 mwaka huu.
Habari Leo
No comments:
Post a Comment