ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, August 3, 2011

Petroli bei chini

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Maji (Ewura), Harun Masebu (kushoto), akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana juu ya kushuka kwa bei za mafuta.

  Yapungua kwa Shilingi 201.37 kuanzia leo
  Tozo za Ewura, TRA, Tiper Sumatra zakatwa
Serikali imeshusha bei ya mafuta na petroli, dizeli na mafuta ya taa kuanzia leo nchi nzima. Bei ya petroli imepungua kwa Sh. 202.37 (sawa na asilimia 9.17) kwa lita moja wakati dizeli imeshushwa kwa Sh. 173.49 (sawa na asilimia 8.31).
Aidha, bei ya mafuta ya taa imepungua kwa Sh. 181.37 sawa na (asilimia 8.70). Uamuzi huo
ulitangazwa jana na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), Haruna Masebu, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma.
Alisema kushuka kwa bei hizo kumetokana na marekebisho yaliyofanywa kwenye tozo zilizokuwa zikitozwa na taasisi mbalimbali za serikali kulingana na majukumu waliyonayo kwenye mfumo wa biashara ya mafuta.
Masebu alisema tozo za taasisi mbalimbali zimerekebishwa kwa ujumla wake ambapo tozo katika petroli imepungua kutoka Sh. 54.03 kwa lita hadi 27.27 (sawa na asilimia 49.53) na dizeli kutoka Sh. 55.00 hadi Sh. 28.15 kwa lita (asilimia 48.80).
“Mafuta ya taa yamepungua kutoka Sh. 55.66 kwa lita hadi Sh. 24.50 (asilimia 55.98) kwa lita. Kwa wastani tozo za taasisi zimepungua kwa asilimia 51.44,” alisema Masebu.
Kwa mujibu wa Masebu, bei ya kikomo kwa mafuta ya petroli kuanzia Julai Mosi hadi sasa ilikuwa Sh. 2,206.16 na kwamba bei ya kikomo mara baada ya mchakato wa marekebisho hayo sasa ni Sh. 2,003.79.
Kwa upande wa dizeli, Masebu alisema bei ya kikomo ilikuwa ni Sh. 2,084.33 wakati bei ya sasa ya kikomo itakuwa ni Sh. 1,910.84.
Masebu alisema bei ya awali ya kikomo kwa mafuta ya taa ilikuwa ni Sh. 2,085.90 wakati bei ya sasa ni Sh. 1,904.53.
Kwa mujibu wa bei mpya, bei ya kikomo katika jiji la Dar es Salaam sasa itakuwa Sh. 2,004 kwa petroli, dizeli Sh. 1,911 na mafuta ya taa ni Sh. 1,905.
Bei kwa mikoa mingine Arusha ni Sh. 2,004; Kihaba Sh. 2,008; Dodoma Sh. 2,062; Iringa Sh. 2,068, Bukoba Sh. 2,219; Kigoma Sh. 2,235; Moshi Sh. 2,072; Lindi Sh. 2,063; Musoma Sh. 2,182; Mbeya Sh. 2,111; Morogoro Sh. 2,029; Mwanza Sh. 2,154; Singida 2,094; Shinyanga Sh. 2,132; Tanga Sh. 2,050; na Tabora Sh. 2,158.
Masebu alisema kuwa bei hiyo mpya itaanza kutumika kuanzia leo na yeyote atakayebainika kuuza mafuta kwa bei ya zaidi ya maelekezo atachukuliwa hatua ikiwa ni kutozwa faini ya Sh. milioni tatu. Kwa mujibu wa Masebu, wahusika na biashara ya mafuta walipatiwa taarifa jana kwa lengo la kuwapa muda wa kutekeleza agizo hilo leo.
Masebu aliwataka wananchi kudai risiti kila mara wanaponunua mafuta katika vituo vya mafuta ambayo itakuwa na tarehe na aina ya mafuta waliyonunua na bei kwa lita.
Alisema kithibiti hicho kitatumika kama kidhibiti cha mnunuzi kama kutajitokeza malalamiko ya ama kuuziwa mafuta kwa bei ya juu kuliko bei elekezi ya kikomo ama ameuziwa mafuta yenye chini ya kiwango cha ubora.
Kupungua kwa bei ya mafuta kulitangazwa bungeni wakati Waziri wa Fedha, Mustafa Mkullo, Juni 8, mwaka huu aliposoma bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha wa 2011/2012.
Kwa mujibu wa vyanzo huru vya NIPASHE, mabadiko ya tozo yataathiri Sumatra ambayo sasa itakuwa inapata Sh.0.29 kwa lita ya petroli; Sh.0.33 lita ya dizeli na Sh. 0.31 kwa lita ya mafuta taa.
Pia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) itapungukiwa kwa kupata tozo ya Sh. 7.05 kwa lita ya petroli; Sh. 7.18 kwa lita ya dizeli na Sh. 7.27 kwa lita ya mafuta ya taa. Nayo Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) pia itapungukiwa kwa kupata Sh. 18.07 kwa lita ya petroli; Sh.18.58 kwa lita ya dizeli na Sh. 18.72 kwa lita ya mafuta ya taa.
Wengine ni Tiper (Sh. 20 kwa petroli; Sh. 0.23 kwa dizeli na Sh. 0.22 kwa mafuta ya taa); TBS (Sh. 1.25 kwa petroli; Sh. 1.24 kwa dizeli na Sh. 125 kwa mafuta ya taa); Ewura (Sh. 6.10 kwa petroli; Sh. 6.80 kwa dizeli na Sh. 3.50 kwa mafuta taa); na Malaka ya Vipimo (Sh. moja).
Serikali itaendea kupata kodi ya bidhaa ya Sh. 539 kwa kila lita ya mafuta kati yake Sh. 200 ni kwa ajili ya ushuru wa barabara (road toll).
CHANZO: NIPASHE

No comments: