Fredy Azzah, Morogoro
MFUMO wa sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika Agosti 31, mwakani, itajumuisha Watanzania wanaoishi nje ya nchi na wale wenye ulemavu wa aina mbalimbali.
Utaratibu huo wa kuorodhesha Watanzania waliopo nje unakuja kipindi ambacho tayari Serikali imekuwa ikichua maoni kutoka kwa wadau mbalimbali kuhusu kuanzishwa kwa uraia wa nchi mbili. Akizungumza kwenye mafunzo ya wakufunzi wa sensa ya majaribio jana, Mkurugenzi Mkuu Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dk Albina Chuwa, sensa hiyo itakuwa ya tano kufanyika tangu nchi ipate uhuru.
“Itakuwa na maswali ambayo hayajawahi kuulizwa kwa zile zilizotangulia, mojawapo ni kutaka kujua Watanzania waliopo nje ya nchi na mengine yanayohusu walemavu, ambayo yataulizwa kwa undani zaidi,” alisema Dk Chuwa.
Sensa ya majaribio inatarajiwa kufanyika Septemba mwaka huu kwenye mikoa 11 nchini.
Kwa mujibu wa Dk Chuwa, sensa ya majaribio inayotarajia kuanza Septemba 4, itafanyika kwa siku saba, ndiyo itakayobainisha ni maswali yatakayojumuishwa au kutolewa kwenye sensa mwakani.
Pia, Dk Chuwa alisema sensa hiyo licha ya kujua idadi ya Watanzania, italenga kujua umaskini wa kipato cha mtu mmoja na idadi ya vifo vitokanavyo na uzazi.
Kwa Mujibu wa Dk Chuwa, sensa hiyo itasaidia Serikali kwenye mipango yake mbalimbali, ikiwamo kutathmini Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania (Mkukuta) na Mkuza kwa upande wa Zanzibar.
Dk Chuwa alisema sensa hiyo ya majaribio itafanyika Mikoa ya Dar es Salaam, Kilimanjaro, Arusha, Kigoma, Mara, Njombe, Manyara, Pwani, Mtwara, Mjini Magharibi na Kaskazini Pemba.
Akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Luteni Kanali mstaafu Issa Machibya, aliwataka wakufunzi hao kuwa makini katika utekelezaji shughuli iliyopo mbele yao, ili kuepuka kuletea taifa hasara kwa kukusanya takwimu zisizo sahihi.
“Mzingatie mafunzo mnayopewa hapa leo, kutofanya hivyo mnaweza kulipa taifa hasara kubwa, tunataka tupate takwimu sahihi ili malengo ya Serikali yafikiwe,” alisema Machibya.
Alisema kutokuwa na takwimu muhimu kama za watu wenye ulemavu wa ngozi, inaiwia vigumu Serikali na taasisi nyingine kutekeleza majumu yao.“Wakati nikiwa RC Mara, tulipata shida sana kupata takwimu sahihi za walemavu wa ngozi wakati ule kulikuwa na mauaji makubwa ya ndugu zetu hawa, ilibidi tutume watu wakawahesabu lakini bado kulikuwa na changamoto kubwa,” alisema Machibya.
Pia, Machibya alisema shughuli hiyo itatoa mchango mkubwa wa kuboresha maisha ya Watanzania kwa ujumla na kuipa Serikali nafasi ya kujitathmini.Aliwataka wananchi wote kuhakikisha wanatoa ushirikiano wa kila aina kwa maofisa wanaoendesha shughuli hiyo, ili zoezi hilo lifanikiwe.
Alisema baadhi ya wananchi wanaogopa maofisa wa Serikali na wakati mwingine kuwakimbia wanapokuwa kwenye utekelezaji wa shughuli zao.“Hivi karibuni nilikuwa Malinyi, nikapita katika shamba la mpunga la mama mmoja, nikataka kumwita ili nizungumze naye, lakini badala ya kuja akakimbia, hii ni mbaya sana, hakujua hata nilikuwa nataka nimwambie nini,” alisema Machibya.
No comments:
Post a Comment