ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, August 24, 2011

Wageni wasio na vibali wapewa wiki mbili




Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha, amewapa wiki mbili raia wote wa kigeni wanaofanya kazi nchini bila ya kuwa na vibali vya ukaazi, kujisalimisha Idara ya Uhamiaji, ili kusaidiwa kuondoka nchini au kuelekezwa namna ya kupata vibali hivyo.
Pia amewataka waajiri wote kuhakikisha wageni wanaowaajiri wana kibali hicho, vinginevyo nao pia watachukuliwa hatua, ikiwa ni pamoja na kukamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.
Waziri Nahodha alisema hayo alipokutana na viongozi wa Idara ya Uhamiaji, jijini Dar es Salaam jana.
Katika mkutano huo, Waziri Nahodha aliwaagiza viongozi hao kusimamia kikamilifu zoezi hilo, ambalo litaendeshwa nchini kote.

Alisema katika siku za hivi karibuni, kumekuwa na taarifa mbalimbali zinazotolewa katika vyombo vya habari na nyingine kufika ofisini kwake kuhusu wageni wanaofanya kazi katika maeneo mbalimbali bila kuwa na vibali vya ukaazi na pia waajiri wanaotoa ajira kwa wageni hao.
Waziri Nahodha alisema wizara yake inazifanyia kazi taarifa hizo.“Jambo hili ni kinyume cha sheria na nawaagiza kufuatilia kwa karibu suala hili ili kubaini ukweli wake na kuwa watakaokamatwa wachukuliwe hatua za kisheria,” alisema Waziri Nahodha.
Aliongeza: “Ni vyema hapa nikawakumbusha tena waajiri na wageni wanaoingia nchini kwa lengo la kuomba ajira kuwa kufuatana na sheria za nchi yetu mgeni yeyote haruhusiwi kuomba ajira kama hana kibali cha ukaazi kinachotolewa na Idara ya Uhamiaji.”
Alisema vibali vya muda wanavyopewa wageni wanaotembelea ndugu au jamaa nchini, haviruhusiwi kuombea ajira.
Waziri Nahodha alisema baada ya muda wa wiki mbili kuisha, wageni wote wanaofanya kazi bila ya kibali cha ukaazi na waajiri watakaokamatwa watatangazwa majina yao.
CHANZO: NIPASHE

No comments: