ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, August 4, 2011

Wauza mafuta wakubali kuuza

Kaimu Katimu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini,Eliakim Maswi akiwa katika kikao faragha na wamiliki vituo vya mafuta kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Wizara hiyo Jijini Dar Es Salaam(picha kwa hisani ya MICHUZI BLOG)
MKURUGENZI Mtendaji wa Chama cha Waagizaji Wakubwa wa Mafuta ya Petroli nchini (TAOMAC), Salum Bisarara, amesema wamekubali kuendelea kutoa huduma kwa bei elekezi.

Alitoa msimamo huo katika mkutano wa waagizaji wa mafuta hao na Serikali jana katika
Wizara ya Nishati na Madini, Dar es Salaam, uliozungumzia mgomo wa wafanyabiashara hao uliofanyika juzi na jana maeneo mengi nchini.


Mkutano huo ulikutanisha kampuni zinazoagiza mafuta nchini za Total Tanzania, NSK Oil, Nat Oil, Lake Oil, Oryx, Camel Oil Ltd, Oil Com, BP, Gapco, Engen, MGS International Ltd, Moil na TPDC.

Pamoja na makubaliano hayo, chama hicho kiliteua kamati maalumu itakayokaa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), kupitia upungufu uliosababisha wamiliki hao kusitisha kutoa huduma juzi.

Bisarara alisema kulikuwa na tatizo, kwa sababu bei iliyotangazwa na Ewura iliwashitua kwa madai kuwa haikuwa imekubaliwa katika vikao vyao vya awali vya kukokotoa bei.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Engen, Seelan Naidoo, aliipa Serikali saa 24 kufanyia kazi upungufu uliomo katika fomula ya ukokotoaji bei mpya, la sivyo, atasitisha huduma.
Naidoo alidai ni vibaya kwa nchi kuendelea kuuza mafuta kwa bei hiyo elekezi na kuitaka Serikali itambue kuwa wao wanafanya biashara kwa ajili ya faida.

“Ni vema tukaruhusiwa kufanya biashara kwa njia endelevu, kwa bei hizo tutakuwa tunakusanya hasara badala ya faida na inaweza kushusha uchumi wa nchi,” alidai Naidoo.

Alisema pamoja na kufikia makubaliano kati ya waagizaji wenzake na Serikali, ya kuendelea kutoa huduma kwa bei elekezi wakati wakisubiri upungufu uliojitokeza kurekebishwa, endapo hautafanyiwa kazi kwa saa 24 kuanzia sasa, kampuni hiyo haitaendelea kutoa huduma.

Engen ni kampuni ya Afrika Kusini ambayo inamiliki asilimia kati ya nne na tano ya soko la mafuta nchini.

Mwakilishi wa Oilcom, Ameir Nahdi, aliyekuwa wa kwanza kutoa msimamo wake, alisema wamekubali kuendelea na biashara baada ya kuelezea upungufu wa upatikanaji wa bei hiyo na kuahidiwa kufanyiwa kazi.

Akijibu hoja ya Serikali kupewa saa 24, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi aliyeitisha mkutano huo, aliwaambia waagizaji hao kuwa hawana mamlaka ya kutoa masharti kwa Serikali.

Alifafanua kuwa Serikali haipewi masharti ya aina hiyo na kuwataka waagizaji hao wafanye kazi kwa ushirikiano na kuonya kwamba kama masharti ya aina hiyo yatatolewa, Serikali pia itatoa ya kwake.

Maswi aliwataka waendelee kuuza mafuta kwa bei elekezi kama ilivyotangazwa na Ewura.

Kuhusu dalili za kuwapo baadhi ya wafanyabiashara wasiotii agizo hilo, Maswi alisema sheria ziko wazi, kwamba mwagizaji anaweza kunyang’anywa leseni ingawa anaamini hawawezi kufika huko kwa kuwa tayari wamekubaliana.

Alifafanua, kuwa juzi mara baada ya mgomo, Serikali ilikutana na waagizaji na kuwataka wauze mafuta kwa kuzingatia bei elekezi kabla ya mkutano wa jana wa kuzungumzia yaliyowatatiza.

Alisema baada ya kukutana na wagizaji hao jana saa 5 asubuhi, ni kweli walikiri kufanya kazi kwa hasara, lakini wakakubaliana kuendelea na biashara kama ilivyo kwa bei elekezi na palipo na matatizo, Ewura iangalie na kutoa maelekezo.

“Tumekubaliana bila masharti na tumechagua Kamati ambayo itakaa na kufuatilia hayo yote ili suluhu ipatikane.

“Tumewaelekeza wawaambie pia wauzaji wao wa mikoani kuuza mafuta kwa bei hiyo na hata magari yaliyokuwa yakisafiri yaendelee na safari ya kwenda yalikokusudiwa,” alisema Maswi.

Kaimu Katibu Mkuu huyo alisema atakagua katika maghala yao kuona kama wametekeleza agizo la Serikali la kuendelea kutoa huduma kama inavyotakiwa.

Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Haruna Masebu, alisema masuala ya waagizaji yana sura ya kisera, usalama wa Taifa na udhibiti ambayo waliyazingatia zaidi.

Hata hivyo wachambuzi wa masuala ya kisheria, wanasema wafanyabiashara hao wamekiuka sheria ya ushindani wa kibiashara ambayo hairuhusu wao kukutana na kupanga mgomo wa kuuza mafuta.

Pia wanasema hawaoni sababu ya wao kusita kuuza mafuta kutokana na bei kushushwa, huku wakiuza mafuta ya taa mwezi uliopita, kwa bei ya juu wakati wakiwa wameyaagiza kwa kodi ya asilimia 52 kwa lita kabla haijapanda hadi asilimia 400.30 zilizokusudia kukabiliana na uchakachuaji.

Habari Leo

No comments: