
Mashabiki wa klabu ya Yanga wakiwa wamezingira gari ndogo lililombeba kocha mkuu wa timu hiyo, Sam Timbe huku wakimlalamikia kushindwa kumtoa Nurdin Bakari kwa madai ya kucheza chini ya kiwango hali iliyoababisha timu hiyo kupoteza mechi dhidi ya JKT Ruvu juzi. Picha na Juma Mtanda.
BAADA ya mashabiki wa Yanga mkoani Morogoro kumfanyia vurugu kocha wao Mganda Sam Timbe kwenye Uwanja wa Jamhuri kutokana na kufungwa bao 1-0 na JKT Ruvu juzi, uongozi wa mabingwa hao umedai utawachukulia hatua kali wote waliohusika na kitendo hicho.
Katika mchezo huo wa ufunguzi wa Ligi Kuu uliofanyika Mkoani Morogoro Yanga ilifungwa, ambapo kitendo kiliwauzi mashabiki hao na kuamua kumzunguka Timbe na kumtupia maneno makali huku wakidai ameshindwa kuipanga timu hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Ofisa habari wa klabu hiyo Louis Sendeu alisema mashabiki waliofanya fujo wanatambulika na watachukuliwa hatua za kinidhamu na uongozi wa juu ambao unatarajia kukutana leo.
Akifafanua Sendeu alisema pia wameweka mikakati ya kukomesha mashabiki wenye nia mbaya na timu yao na kuanzia sasa watakuwa wakitumia kamera za video itakayokuwa ikirekodi vitendo vyote vya mashabiki wao ili kuwabaini kwa haraka.
"Kwanza kabisa tunapenda kulaani kitendo cha mashabiki kutaka kumfanyia fujo kocha na hili tunalipa uzito kwani wanachama hao tumewabaini na wataadhibiwa ipasavyo, tumepanga kila mchezo utakuwa ukichukuliwa video ili tuweze kubaini wanaotaka kuiharibu klabu yetu,"aliongeza Sendeu.
Aidha alisema kwa mujibu wa Kocha kufungwa kwao pia kunachangiwa na uwanja wa Jamhuri kutokuwa katika hadhi nzuri pamoja na kutawaliwa na majeruhi wengi katika kikosi hicho.
Aliwataja majeruhi katika kikosi hicho ni pamoja na Golikipa wao Yaw Berko, Davies Mwape, Kenneth Asamoah, Kigi Makasy na Idrisa Rashid ambao kwa kiasi kikubwa wameacha pengo kubwa.
Kwa upande wa kocha Timbe amewataka wachezaji wake kujituma zaidi ili kuweza kutetea ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom baada ya kuanza vibaya.
Timbe alisema kuwa kupoteza kwa mchezo huo kumetokana na wachezaji kushindwa kujituma na kudai kuwa safu ya ushambuliaji nayo imeshindwa kutekeleza majukumu yao kwa kushindwa kutumia vema nafasi walizopata wakiwa katika nafasi nzuri ya kufunga ambapo hali hiyo imewanufaisha wapinzani wao katika mchezo huo kwa kuibuka na pointi tatu.
“Safu ya ushambuliaji imeniangusha kutokana na kushindwa kupachika mabao kwani katika mchezo ule sisi tulicheza kipindi cha pili na hawa wapinzani wetu walicheza vizuri kipindi cha kwanza na tumeshindwa kutumia vema nafasi tulizopata,” alisema Timbe.
Timbe alisema kwa sasa anaifanyia kazi hasa safu ya ushambuliaji kwa kuongeza mbinu mbalimbali za ufungaji katika mazoezi na hatarajii kuoana tena washambuliaji wake wakikosa mabao, Yanga ilifanya jana mazoezi kwenye uwanja wa Jamhuri ikiwa ni maandalizi kwa mchezo na Moro United hapo kesho.
Akizungumzia juu ya yeye kugoma kuzungumza na Wanahabari mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo,Timbe alisema waandishi wa habari za michezo amewaomba waandae utaratibu nzuri wa kutafuta namna ya kuongea na makocha mara baada ya kumalizika kwa mchezo kwa sababu za kiusalama.
“Mimi sikugoma kuongea na waandishi wa habari nilichotaka ni kuwapo kwa chumba cha mikutano sasa ninyi waandishi mkishindwa kufanya hilo basi mshirikiane na jeshi la polisi kuwapo na ulinzi, lakini ni mara baada ya kuondoka kwa mashabiki kwani mashabiki wamekuwa na tabia ya jazba mara baada ya timu zao kupoteza mchezo kwani kiusalama suala hilo sio sahihi,” alisema Timbe.
Timbe alisema kuwa mashabiki wanapaswa kufahamu hakuna kiongozi anayependa timu ipoteze mchezo kwani wamekuwa na jazba hasa timu yao inapofanya vibaya hivyo hiyo inakuwa ni hatari kwao makocha kuzungumza wakati bado mashabiki wapo ndani ya uwanja huku wakiwa na jazba ari inayotia hofu kuwa wanaweza kufanya jambo lolote baya kutokana na timu yao kupoteza mchezo.
Naye kocha msaidizi wa Yanga, Fred Minziro alisema wamefungwa bahati mbaya, lakini amesisitiza kuwa wanajipanga upya kuganga yajayo na wao bado ni mabingwa.Minziro alisema kupoteza pointi tatu imewauma, lakini hawana cha kufanya kwa vile ligi ndio imeanza na bado wana mechi 25 ambazo lolote linaweza kutokea.
Alisisitiza; "Yanga ina timu imara ambayo ina uwezo wa kuchukua tena ubingwa, kupoteza mchezo kwenye mashindano kama haya ni kitu ambacho kinatokea, tutajipanga wala hatukucheza vibaya wao walipata nafasi moja tu wakaitumia wakatudhuru."
Mwanachi
No comments:
Post a Comment