ANGALIA LIVE NEWS

Monday, September 19, 2011

Azam yainyuka Yanga, Simba yashikwa Kagera


Mshambuliaji wa Yanga,Keneth Asamoah(kushoto), akiwania mpira na beki wa Azam, Agrey Moris, wakati wa mechi ya Ligi kuu ya Vodacom jana,Azam ilishinda 1-0.Picha na Michael Mtemanga
Sweetbert Lukonge, Wiliam Paul, Kagera
AZAM imefuta uteja wake kwa Yanga baada ya kuichapa kwa bao 1-0 kwenye Uwanja Taifa, huku Simba wakiendelea kubaki kileleni baada ya kupata sare 1-1 na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Mshambuliaji John Boko alilizamisha jahazi la Yanga dakika ya 20 na kupoteza matumaini ya mabingwa hao kurudi katika mstari wao wa ushindi, nao vinara wa Ligi Kuu Simba walishindwa kuvunja mwiko mkoani Kagera baada ya kulazimisha sare 1-1kwa  goli yaliyofungwa na  Patrick Mafisango na Hussein Sued kwa wenyeji.

Baada ya michezo hiyo Simba inaongoza kwa kufikisha pointi 14 wakifutiwa na Azam na Mtibwa Sugar zenye pointi 11wakati Yanga imebaki na pointi zake sita na Kagera Sugar imefikisha pointi tano baada ya michezo sita kila moja.
Azam walianza mchezo kwa kasi na dakika ya kwanza mshambuliaji  Boko alifika langoni kwa Yanga, lakini kipa Yaw Berko alikuwa makini kuokoa hatari hiyo.


Mrisho Ngassa alikosa bao la wazi dakika 16 kwa kushindwa kumalizia mpira wa kona iliyopigwa na Ibrahimu Mwaipopo. Yanga ilijibu mapigo kupitia Hamis Kiiza aliyekosa bao dakika 18, pamoja na kushindwa kumalizia kazi nzuri ya Nurdin Bakari. Kabla ya Haruna Niyonzima kupiga shuti kali lililotoka nje kidogo ya goli la Azam.

Mshambuliaji Boko alitumia vizuri udhaifu wa ngome ya Yanga kuipatia Azam bao la kuongeza dakika 20 akimalizia kwa umakini kazi ya Waziri Salum aliyempokonya mpira Shamte Ally na kupitisha pasi kwa mfungaji.

Katika mchezo huo Azam ilikuwa ikishangiliwa kwa nguvu na mashabiki wachache waliojitokeza kutazama mchezo huo.
Kocha Stewart Hall aliwasifu wachezaji wake kwa kucheza kwa nguvu na kujiamini hasa sehemu ya ulinzi.
Kukosa umakini kwa safu ya ushambuliaji wa Yanga kulimfanya kocha Sam Timbe kumtoa Davies Mwape na kumwingiza Keneth Asamoah katika dakika 38, mabadiliko hayakuwasidia kwani hadi mapumziko mabingwa hao walikuwa nyuma kwa bao 1-0.
Ukata wa Yanga ulioruhusu mabao saba tu msimu mzima uliopita hali imekuwa tofauti kabisa sasa kwani katika mechi sita ilizocheza imesharuhusu mabao matano.
Beki Chacha Marwa na Maneno Mbegu wameshindwa kuziba vizuri pengo la majeruhi Nadir Haroub kwani mara kadhaa walionekana wakijichanganya.
Rashid Gumbo mfungaji wa bao la ushindi dhidi ya African Lyon aliingia kipindi cha Pili kuchukua nafasi ya Pius Kisambale na kuifanya Yanga kuwa na viungo wanne ambao ni Niyonzima, Nurdin na Godfrei Taita aliyechukua nafasi Shamte.
Kocha Hall alimtoa Hamis Mcha na kumwingiza kiungo Abdubakari Salum ili kuendelea kukitawala kiungo.
Mshambuliaji Kiiza alikosa bao dakika 64 baada ya kipa wa Azam, Mwadini Ally kutema mpira kufutia shuti la Niyonzima.
Mwamuzi Oden Mbaga alimpa kadi ya njano Chacha kwa kupiga mpira nje kwa makusudi dakika ya 80.
Kocha Timbe alisema wachezaji wake wamekosa nafasi nyingi za kufunga jambo lililochangia kupoteza mchezo huo.
Mjini Bukoba, mwenyeji Kagera Sugar wameendeleza rekodi ya kutokufungwa kwenye Uwanja wa Kaitaba baada ya kuwalazimisha sare 1-1na vinara wa ligi Simba huku mwamuzi Alex Maagi kutoka Mwanza akitoa penalti kwa kila timu.

Mshambuliaji Felix Sunzu alikosa penalti baada ya beki wa Kagera Sugar, Malegesi Mwangwa kunawa mpira kwenye eneo la hatari, lakini nyota huyo wa zamani Al Hilal alipaisha.

Beki ya Kagera Sugar Sugar iliyokuwa ikicheza kwa umakini zaidi muda wote lipotea mabayo na kumwacha Patrick Mafisango akiunganisha krosi Shomari Kapombe dakika 65 na kuipatia Simba bao la kuongoza.

Wenyeji Kagera waliamka na kufanikiwa kupata bao la kusawazisha kupitia mkwaju wa penalti Hussein Sued aliyeingia akitokea benchi baada ya beki Victor Costa kumchezea vibaya Juma Mpola kwenye eneo la hatari dakika 75.
Simba walimtoa Geirvas Kago na kumwingiza Haruna Moshi wakati Kagera walimtoa Sunday Frank na kumwingiza Hussen Sued.

Mwananchi

No comments: