ANGALIA LIVE NEWS
Thursday, September 29, 2011
Dk Slaa amnusuru mbunge wa CCM
WaandishiWetu, Igunga
KATIBU Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa jana mchana alilazimika kukatisha mapumziko yake ili kumwokoa Mbunge wa Sumbawanga Mjini (CCM), Khalfan Aeshi ambaye aliwekwa chini ya ulinzi na vijana wa chama chake.Aeshi aliwekwa chini ya ulinzi akiwa pamoja na viongozi wengine vijana wa CCM waliokwenda katika Hoteli ya The Planet ambako viongozi wakuu wa Chadema wamefikia kukutana kujadili jinsi ya kuendesha siasa za kistaarabu katika kampeni zinazoendelea hapa.
Viongozi wengine ni pamoja na Katibu wa Mambo ya Nje wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM, January Makamba, Kaimu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Benno Malisa na Mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM, Hussein Bashe.
Tukio hilo lilitokea saa chache baada ya jingine la kutekwa kwa vijana wanne wanaodaiwa kuwa wanachama wa Chadema ambao walikuwa kwenye kampeni za CCM zilizofanyika kwenye Viwanja vya Sabasaba, kuzindua rasmi matumizi ya helikopta kwa mgombea wake, Dk Dalaly Kafumu.
Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na January zimesema kwamba viongozi hao walikuwa na majadiliano na wenzao wa Chadema walioongozwa na Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe kuhusu jinsi ya kumaliza siasa chafu zinazofanyika Igunga hivi sasa.
Zitto pia alithibitisha kutokea kwa vurugu zilizosababishwa na uhusiano mbaya baina ya vijana wa Chadema ambao wanamshutumu Aeshi kwamba amekuwa akipanga mbinu chafu za kuwachafua.
Miongoni mwa matukio hayo ni lile la usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita, ambalo liliwahusisha baadhi ya vijana wa Chadema na tuhuma za kumfukuza na kumrushia risasi Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Esther Bulaya.
Ilikuwaje?
Habari zinasema kuwa Aeshi alifika katika eneo hilo ngome ya Chadema akifuatana na January na mara baada ya kushuka kwenye gari, baadhi ya vijana wa Chadema walimfuata wakitaka kumweka chini ya ulinzi.“Ilizuka tafrani kubwa tu hapa, vijana wetu walichachamaa sana wakasema lazima wamdhibiti huyo kada wa CCM kutokana na mambo mabaya ambayo amekuwa akitufanyia,” alisema mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo ambaye ameomba jina lake lihifadhiwe.
Shuhuda huyo alisema tafrani hiyo ilidumu kwa dakika kadhaa huku viongozi hao wa vijana wakijitahidi kusuluhisha bila mafanikio hadi Dk Slaa alipotoka chumbani kwake alikokuwa amepumzika na kuwatuliza vijana wa Chadema waliokuwa wamemweka Aeshi chini ya ulinzi.Kwa mujibu wa habari hizo, Dk Slaa aliwasihi vijana kupunguza jazba na kuwaasa kwamba siasa siyo uadui. Kauli yake hiyo ilifanikisha usuluhishi uliohitimisha ugomvi baina ya pande husika.
Akizungumzia tukio hilo Aeshi alisema: “Si kweli kwamba mimi niliwekwa chini ya ulinzi, kilichotokea ni tafrani ndogo tu ambayo ilitokana na tofauti za kisiasa baina yetu na wenzetu.”
Lengo la kukutana
Kuhusu madhumuni ya kukutana January alisema: “Lengo la kwenda kwetu pale (Chadema) lilikuwa ni kufanya mazungumzo na vijana wenzetu na tayari tulishawasiliana na Zitto na tukakubaliana kwamba tukutane tujadili jinsi ya kuhitimisha kampeni hizi kwa amani.”
“Ujue hata kama tunatafuta kura, hatuwezi kutafuta katika sehemu ambayo inaonekana kugubikwa na matukio ya aina hii, mara risasi, mara nini hii siyo nzuri, kwa hiyo kumbe hata wenzetu wa Chadema waliliona hilo, hivyo tumekutana kwa ajili hiyo.”“Basi tulipofika pale, kukatokea hiyo tafrani ndogo, lakini tunashukuru kwamba Dk Slaa alipokuja tulikaa na tukawa na mazungumzo rasmi ambayo yalituwezesha kufikia hitimisho, hayo yamepita.”
Hata hivyo, Zitto alikosoa hatua ya January kufika katika eneo la Hoteli ya The Planet akiambatana na Aeshi hali akijua kwamba mbunge huyo ana ugomvi na vijana wa Chadema.“Sisi wote ni viongozi na sisi hawa kina Bashe, January na Benno hatuna ugomvi nao hata kidogo kwani mazungumzo yetu yalilenga kujenga mazingira mazuri ya ushindani wa kisiasa tofauti na ilivyo sasa, ila nadhani January alikosea kuja na Aeshi pale, maana tayari huyu alikuwa na ugomvi na vijana wa Chadema,” alisema Zitto.
Habari zilizopatikana zinasema kuwa kikao hicho pia kilijadili utekaji nyara wa vijana wanaosadikiwa kuwa wafuasi wa Chadema, ambao ulifanyika jana asubuhi kwenye mkutano wa kampeni wa CCM.
Utekaji mkutanoni CCM
Mapema katika mkutano wa kampeni uliofanyika jana asubuhi katika Viwanja vya Sabasaba Mjini Igunga, vijana waliovalia sare za CCM na wengine waliovaa kiraia waliwateka nyara watu wanne na kuwaingiza kwenye gari kisha kuwapeleka kusikojuliana.
Vijana hao walitekwa wakati viongozi wa juu wa kisiasa wa CCM walipokuwa wakihutubia muda mfupi baada ya kutua kwa helikopta ya chama hicho inayotarajia kutumiwa katika siku tatu za mwisho za kampeni.Mwandishi alishuhudia vijana hao wakikamatwa kwa nguvu kisha kuwapandisha kwenye gari lenye rangi nyeupe aina ya Land Cruiser, Hardtop na gari hilo kutokomea kusikojulikana.
Tukio hilo lilitokea siku moja tangu Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro kutoa madai ya kuwapo kwa vijana wa CCM walioletwa Igunga kwa lengo la kutisha wananchi na kufanya vurugu.Wakati wa tukio hilo la utekaji, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira alikuwa jukwaani akihutubia mkutano huo.
Wassira ambaye alijitambulisha mbele ya umati wa watu kuwa yeye ni maarufu kwa jina la Tyson, aliwataka walio wanachama wa CCM kunyoosha mikono kitendo ambacho kiliitikiwa na baadhi ya wananchi, wengi wakiwa ni waliokuwa wamevalia sare za rangi za chama hicho, kijani na njano.
Baadaye aliwataka wanachama wa Chadema waliokuwapo kunyoosha mikono, lakini hakuna aliyeitika wito huo.
Baada ya hapo Wassira alisema: “Mnaona hamna kitu hapa,” ndipo umati wa watu wengi wakiwa nyuma ya wale wenye sare waliponyoosha mikono yao juu, huku wakionyesha vidole viwili na wengine wakiimba “peoples power”, kisha Wassira akasema: “Kumbe wapo kule nyuma.”
Baada ya hapo, vijana wa CCM walisambaa kutoka katika maeneo mbalimbali ya uwanja huo na ndipo walipoonekana wakikamata vijana hao na kuwapakia kwa nguvu kwenye gari.Baada ya tukio hilo vijana hao walisikika wakilalamika: “Tunaonewa tunaonewa,” hawakusikilizwa na gari hilo liliondoka kwa kasi katika eneo hilo na kutokomea kusikojulikana.
Vijana walioshuhudia tukio hilo walisema wenzao walitekwa nyara baada ya kutekeleza agizo la Wassira na la kutaka wanachama wa Chadema wajitambulishe kwa kunyoosha mikono.
“Huo ndiyo uonevu wa CCM si mnaona?” alisikika mmoja wa vijana hao akipaza sauti na ndipo kundi hilo lilipotoka uwanjani hapo likiimba wimbo maarufu unaotumiwa na Chadema wa (peoples power).Vijana hao walitoka katika eneo hilo kwa maandamano kwa lengo la kwenda kujaribu kuwaokoa wenzao lakini gari hilo lilibadili njia na kuelekea kusikojulikana.
Msemaji wa Polisi katika kampeni za Igunga, Naibu Kamishna, Isaya Mngulu alipoulizwa kuhusu tukio hilo alisema hakuwa akifahamu chochote.“Gari hilo bado halijafika na sisi bado tunaendelea kulifuatilia tutawapatia taarifa,” alisema Mngulu alipozungumza kwa simu na Mwananchi.
Baadaye Mngulu alitoa taarifa kwamba kulikuwa na fujo kwenye mkutano wa CCM jana saa 5.00 asubuhi na kwamba vijana wawili, Joseph Kamanga na Adam Iddi walikamatwa kwa tuhuma za kuhusika na fujo hizo na kutoa matusi.“Matusi hayo yalitolewa wakati Steven Wassira alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara na kuwataka waliokuwapo kwenye kampeni kunyoosha mikono ikiwa ni ishara ya kuonyesha ni kina nani watamchagua mgombea wa CCM, Dk Dalaly Kafumu...,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo ya polisi iliyosainiwa na Mngulu na kuongeza:
“Kufuatia tukio hilo ndipo watuhumiwa walipoanza kutoa kauli za kejeli na matusi zilizosababisha fujo na hatimaye kukamatwa na walinzi wa chama cha CCM Green Guard, ambao hatimaye waliwakabidhi kwa askari polisi waliokuwa kwenye mkutano kwa shughuli za ulinzi na usalama.”
Helikopta zapasua anga
Ilipotimu saa 4:30 asubuhi jana, helikopta ya CCM iliwasili katika eneo la Igunga na kuanza kuzunguka kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kukusanya watu.Mara baada ya muda ilitua katika viwanja hivyo na kuzungukwa na mamia ya watu waliofika kuishangaa huku baadhi yao wakiwa wamevaa sare za chama.
Mapokezi hayo yalipambwa na kila aina ya burudani zikiwahusisha wasanii mbalimbali wakiwamo wa kundi la TOT Plus, likiongozwa na Kapteni John Komba.Awali, ilielezwa kwamba chama hicho kingeleta jimboni hapa, helikopta mbili lakini haikuelezwa kama hiyo nyingine itawasili au la kwa ajili ya kufanya mikutano 25 kwa siku kama kilivyoeleza.
Baada ya kutua, Januari aliyekuwamo katika helikopta hiyo aliteremka na moja kwa moja kuelekea katika jukwaa akiwa na viongozi wengine kuzungumza na wananchi.
Mratibu wa kampeni hizo, Mwigulu Nchemba aliutambulisha ugeni huo na kuwaasa wakazi wa Igunga kutochagua chama kingine kwa sababu Serikali iliyoko madarakani ni ya CCM na sera zinazotekelezwa ni za chama hicho.
Katika mkutano huo Januari alisema: “Dunia nzima inafuatilia uchaguzi huu, inajua kunawagombea wanane wa ubunge, wawekeni kwenye mizani na kuwapima kielimu, kimaadili na kimaarifa, bila shaka Dk Kafumu ana sifa hizo.”
Aliwataka wakazi hao kutopeleka mtu wa kuomba miongozo bungeni na badala yake wamchague mtu wa kuwasemea. Alitamba kwamba CCM kimekamata katika jeshi la ardhi na sasa limekuja angani na kusisitiza kuwa kazi ndiyo inaanza kuhakikisha CCM kinashinda.
CUF nayo ni anga kwa anga
Jana jioni helikopta ya CUF nayo iliwasili tayari kwa ajili ya kurahisisha kampeni za mgombea wake, Leopord Mahona. Ujio huo unavifanya vyama vikuu vitatu kila kimoja kuwa na usafiri huo. Cha kwanza kilikuwa Chadema ambacho helikopta yake iliwasili hapa juzi tayari kwa ajili ya kumnadi mgombea wake, Joseph Kashindye.Baada ya kutua, helikopta hiyo ya CUF ilivuta umati mkubwa wa wananchi.
Magufuli asalimu kwa lugha nane
Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, jana alikuwa kivutio kikubwa katika kampeni za CCM baada ya kuwasalimu wananchi waliokuwa kwenye Viwanja vya Sabasaba kwa kutumia lugha za makabila manane tofauti kwa ufasaha.
Pia alitumia mkutano huo kumpiga vijembe Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba kuwa alivunja sheria za nchi alipopanda punda na kumtembeza kwenye barabara ya lami katika uzinduzi wa kampeni za chama hicho wakati wa maandamano yaliyoishia Uwanja wa Sokoine.
Dk Magufuli ambaye hakumtaja kwa jina Profesa Lipumba alisema kitendo hicho kilikuwa ni kinyume cha Sheria namba 13 ya mwaka 2007 na Sheria namba 18 ya mwaka 2008 ya Mambo ya Ngozi.
“Hata sheria namba 19 ya mwaka 2008 ya Ustawi wa Wanyama huwezi ukampanda punda anavuja damu eti unakwenda kwenye kampeni… msichague watu ambao hawajui hata sheria,” alisema Dk Magufuli.
Akihutubia mkutano huo uliokuwa mahsusi kwa ajili ya kupokea helikopta ya CCM, Dk Magufuli alisema alipopitisha Bajeti ya Sh1.49 trilioni alifahamu kuwa wananchi wa Igunga wanayo kero za barabara na madaraja.
“Leo hii ninavyokuja tumeshatangaza tenda kwa ajili ya kujenga Daraja la Mbutu…. nilisikia kuna mmoja anasema mkimchagua atajenga daraja hilo kwa siku 60 hizo ni ndoto za mchana,” alisema Dk Magufuli.
Alisema daraja hilo lina eneo la kilometa tatu ambazo zinatakiwa kujengwa tuta huku daraja lenyewe likiwa ni meta 53 na pia yakihitajika madaraja mengine matano madogo.
Aliwasihi wananchi wa Igunga kumchagua mgombea wa CCM akisema huyo ndiye mwenye uwezo wa kuingia ofisi ya Waziri yeyote kufuatilia maendeleo ya Wananchi hao kwa kuwa sera inayotekelezwa sasa ni ya CCM.
Wakati akihutubia, Dk Magufuli aliuliza kama kulikuwa na wafuasi wa Chadema na ndipo kundi la vijana waliponyoosha vidole wakitumia ishara ya V. Baada ya kubaini hilo aliwaeleza kuwa kinachotakiwa ni maendeleo si uhasama.
Kwa upande wake, Dk Kafumu aliwaomba wananchi hao wamchague akisema kazi yake ya kwanza itakuwa ni kufuta ushuru wa Sh500 wanaotozwa wafanyabiashara wa mchicha katika Soko Kuu la Igunga.
Rage yamkuta
Katika hatua nyingine, Kamati ya Maadili ya Uchaguzi ya Jimbo la Igunga, imemtoza faini ya Sh100,000, Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Aden Rage kwa kosa la kupanda jukwaani na bastola.
Rage alitozwa faini hiyo jana katika kikao cha kamati hiyo kilichofanyika jana chini ya mwenyekiti wake, Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Igunga, Protace Magayane.Magayane alithibitisha kutolewa kwa adhabu hiyo akisema kikao hicho kilihudhuriwa na mwakilishi mmoja mmoja kutoka vyama vyote vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi huo.Hatua hiyo imekuja baada ya Chadema kuiandikia barua kamati hiyo ikilalamikia kitendo hicho cha Rage.
Habari hii imeandikwa na Neville Meena, Daniel Mjema na Geofrey Nyang’oro, Igunga
Mwananchi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment