ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, September 29, 2011

Igunga: Bastola yamlipukia Rage


  Tume yampiga faini kali
  Chadema wapewa karipio
  Chopa za CCM, CUF zatua
Mbunge wa Tabora Mjini (CCM), Aden Rage
Kamati ya Maadili ya Jimbo la Igunga, mkoani Tabora, imemhukumu Mbunge wa Tabora Mjini (CCM), Aden Rage, kulipa faini ya Sh. 100,000 kwa kosa la kupanda jukwaani na bastola katika mkutano wa hadhara wa kampeni katika eneo la Igurubi wilayani hapa.
Aidha, kamati hiyo imekipa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) karipio kali baada ya CCM kukilalamikia kuwa kiliifanyia vurugu.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya jimbo hilo, ambaye pia ni Msimamizi wa Uchaguzi wa Tume ya Uchaguzi, Protace Magayane, alisema jana kuwa walipokea malalamiko ya Rage kupanda na bastola jukwaani Septemba 24, mwaka huu.

Alisema baada ya kupokea maelezo kutoka CCM, aliitisha kikao cha maadili jana asubuhi ambacho kilipitia malalamiko na maelezo ya upande unaolalamikiwa na kumhukumu Rage kulipa faini hiyo.
“Baada ya kuyapitia tumetoa adhabu kufuatana na maadili. Tuliona alivunja kifungu cha maadili 2:2 (c ) ambacho kinasema mtu yeyote haruhusiwi kubeba silaha ya aina yoyote ikiwa ni pamoja na silaha za kijadi ama silaha yoyote inayoweza kudhuru mtu katika mkutano wa kampeni ama mkusanyiko wowote wa kisiasa,” alisema Magayane.
Alifafanua kuwa faini hiyo inatakiwa kulipwa kabla ya kampeni za uchaguzi huo kumalizika keshokutwa.
“Endapo mhusika ataendelea kukiuka maadili au kutolipa faini anaweza kusimamishwa kampeni za uchaguzi kwa idhini ya kamati ya taifa…faini italipwa kwa msimamizi wa uchaguzi au Tume ya Taifa ya Uchaguzi,” alisema.
CHADEMA YAPEWA KARIPIO
Kuhusu karipio kali, Magayane alisema Chadema wamepewa karipio kali kwa kutakiwa kutofanya tena vitendo vya vurugu.
Magayane alisema alipokea malalamiko ya CCM wakituhumu Chadema kuwarushia mawe na risasi wabunge wake. Katika tukio hilo la utata lilitokea Ijumaa iliyopita, CCM walidai kuwa Mratibu wa Kampeni wa Chadema katika uchaguzi huo, Mwita Waitara, aliwafyatulia risasi wabunge CCM Esther Bulaya (Viti Maalum) na Mbunge wa Sumbawanga Mjini (CCM), Hilary Aesh.
Aidha, CCM waliilalamikia Chadema kuwa wafuasi wake walirusha mawe katika tukio hilo.
Polisi walisema tukio hilo lilitokea katika hoteli waliyofikia wabunge wa Chadema wakati CCM wanadai kuwa ni katika barabara kuu ya Igunga-Nzega.
MATOKEO KUTANGAZWA MAPEMA
Katika hatua nyingine, Magayane alisema wamejiandaa vizuri kuhakikisha kuwa matokeo ya uchaguzi utakaofanyika Jumapili yanatolewa mapema.
“Tuna kitu kinaitwa result management system (mfumo wa kusimamia matokeo ya uchaguzi), hapa nina vijana wanne wanawafundisha vijana watatu baadaye watakuwa saba kwa ajili ya kutoa matokeo kwa hiyo tunategemea matokeo yatatoka mapema,” alisema.
Alisema kuwa katika Uchaguzi Mkuu uliopita matokeo yalichelewa kutangazwa kwa kuwa kulikuwa na gari moja katika kila kata kwa ajili ya kukusanya kura kutoka kata mbalimbali, lakini katika uchaguzi huu wameweka magari mawili kila kata.
“Kutakuwa na magari matano yatakayokuwa yaki-supervise (kusimamia) kwa hiyo tunatarajia matokeo yatangazwa mapema,” alisema na kuongeza kuwa kutakuwa na magari 52 katika kata zote 26 zilizopo katika Jimbo la Igunga.
VYAMA SABA KUWEKA MAWAKALA
Kuhusu mawakala, Magayane alisema vyama saba kati ya vinane vimeweka mawakala katika uchaguzi huo utakaofanyika Jumapili ijayo.
Alivitaja vyama hivyo kuwa ni AFP, CCM, Sau, DP, CUF, Chadema na UPDP na kwamba chama ambacho kimeshindwa kuwasilisha orodha ya mawakala ni Chausta. “Chausta wamekuja hapa wakaniomba niwaongezee muda wa siku mbili wa kutafuta mawakala, lakini sikuwapa muda kwa sababu ulikuwa umeisha na tuliwaapisha jana (juzi),” alisema.
HELIKOPTA YA CCM YAWASILI
Vumbi la kusaka kura jana lilizidi kutimka baada ya helikopta ya CCM kuwasili saa 4:30 asubuhi ikiwa na Mbunge wa Bumbuli ambaye pia ni Katibu wa Kamati Kuu ya CCM wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, January Makamba, kwa ajili ya kuongeza nguvu katika kampeni za chama hicho.
Baada ya kuwasili, helikopta hiyo ilizunguka katika anga ya Igunga kwa zaidi ya dakika 10 kabla ya kutua na kupokewa na Mratibu wa Kampeni za CCM katika uchaguzi huo, Lameck Nchemba Mwigulu, wabunge na makada wengine wa CCM.
WASSIRA ACHAFUA HALI YA HEWA
Katika tukio jingine vurugu zilizuka katika mapokezi ya helikopta ya CCM mara baada Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uratibu na Uhusiano) Stephen Wassira, kuuliza kama kwenye mkutano huo kulikuwa na wanachama wa Chadema.
Wassira aliwataka wanachama wa Chadema waliokuwepo katika mkutano huo kunyoosha mikono juu, jambo ambalo liliwafanya mashabiki wote wa chama hicho ambao walikuwa sehemu kubwa ya mkutano huo, kunyoosha mikoni juu huku wakionyesha alama ya 'V' ambayo hutumiwa na chama hicho.
Hali hiyo ilisababisha walinzi wa CCM waliokuwepo katika eneo kuwakamata baadhi yao na kuwaweka katika gari aina ya Land Cruiser Hardtop lenye namba za usajili T 479 ABT, na kuondoka.
Hali hiyo iliwafanya baadhi ya waandishi wa habari kupiga simu polisi ambao walifika na kulifuatilia gari hilo. Mkuu wa Kitengo cha Tathimini na Ufuatiliaji wa Jeshi la Polisi, Issaya Mngulu, alisema wanawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kufanya fujo na kutoa lugha ya matusi wakati Wassira alipokuwa anahutubia mkutano wa kampeni za CCM.
Alisema watu hao walikamatwa katika uwanja wa Sabasaba, mjini Igunga, jana asubuhi na kuwataja kuwa ni Joseph Kamanga na Adam Idd.
Alisema tukio hilo lilitokea wakati akihutubia katika mkutano na kuwataka waliokuwepo katika uwanja huo kunyoosha mikono kuonyesha kuwa watamchagua mgombea wa CCM, Dk. Peter Kafumu.
Alisema watu hao walikamatwa na kikundi cha walinzi wa CCM (Green Guard) kufuatia matusi na vurugu. Hata hivyo, alisema miongoni mwa watuhumiwa hao wanaendelea kutafutwa na polisi.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willbroad Slaa, alishangazwa na hatua ya CCM kuwakamata watu wanaokwenda kusikiliza mikutano hiyo.
Alisema inafika wakati Tanzania watu wanapewa masharti ya nani afike kusikiliza sera na kwamba wamekuwa wakisisitiza katika mikutano mbalimbali ya kampeni kuwa ni vyema wanachama wakaenda kusikiliza mikutano ya vyama vingine ili waweze kupambanua pumba na mchele.
VIJANA CCM, CHADEMA WATAFUTA MWAFAKA
Wakati huo huo, viongozi vijana wa CCM na Chadema wamefikia mwafaka wa kusuluhisha migongano kati ya mashabiki wa vyama hivyo ili kuepuka kuacha madonda ya uchaguzi mara baada ya kumalizika kwa zoezi la upigaji kura Jumapili.
Mjumbe wa Baraza Kuu la Vijana Taifa (Bavicha), Husein Bashe, alisema mazungumzo hayo yalianza Jumamosi iliyopita kwa simu kati yake na Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema, na kwamba walikubaliana yafanyikie jimboni Igunga.
“Tumefanya mazungumzo ya kirafiki tu ya kutuliza munkari (hasira) wa vijana wetu,” alisema Bashe na kuongeza kuwa
mazungumzo hayo yaliwafikisha hatua ya kukutana jana mara baada ya helikopta ya CCM kutua katika viwanja vya Sabasaba.
Kwa mujibu wa Bashe, yeye na Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Beno Malisa, walikwenda katika hoteli waliyofikia Chadema na baadae walifuatwa na Makamba pamoja na Mbunge wa Sumbawanga Mjini (CCM), Aeshi Hilary.
Alisema baada ya akina Makamba kufika, vijana wa Chadema waliungana kushiriki mazungumzo hayo akiwemo Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe, Lema na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), John Heche. Alitaja wengine waliohudhuria kikao hicho kuwa ni pamoja na Mbunge wa Singida Magharibi (Chadema), Tundu Lissu, wabunge wa Viti Maalumu Chadema, Suzan Lyimo na Grace Kiwelu na Slaa.
Makamba alisema wamekubaliana kuendelea kuzungumza kila panapotokea kutoelewana kati ya mashabiki wao na kila upande ujitahidi kuzuia jazba za vijana wao.
“Mimi nilisikitishwa sana na hali ya vurugu zinazoendelea Igunga na katika kikao chetu tumezungumza vizuri na kukubaliana kuwa ili tufanikishe kampeni na uchaguzi, tuondoe vurugu. Tumekubaliana tusiache makovu baada ya uchaguzi,” alisema Makamba.
HELIKOPTA YA CUF YAWASILI
Nayo CUF jana ilianza kutumia helikopta yenye namba za usajili 5-BTW ambayo ilitua katika uwanja wa Barafu viliopo mjini hapa huku umati wa watu ukishuhudia Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Ismail Jussa, akishuka katika helikopta hiyo.
Akizungumuza na waandishi wa habari baada ya kutua helikopta hiyo Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Julius Mtatiro, alisema helikopta hiyo inatarajiwa kufanya mikutano 12 kwa siku kwa siku tatu zilizosalia.
MAGUFULI ANGURUMA, AMVAA LIPUMBA
Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, alianza rasmi kumpigia kampeni mgombea wa CCM, Dk. Peter Kafumu katika tarafa ya Igurubi.
Akiwasalimia wananchi waliokuja kuipokea helikopta hiyo, Dk. Magufuli alisema zabuni kwa ajili ya ujenzi wa daraja la Mbutu ambalo ni shida ya wakazi wa jimbo hilo kwa muda mrefu imeshatangazwa.
“Nilisikia kuna mmoja (mgombea wa CUF, Leopard Mahona), ambaye alisema mkimchagua ana uwezo wa kutengeza daraja kwa siku 60 hizo ni ndoto, inawezekana hajawahi kufika pale, daraja la Mbutu lina eneo la kilometa tatu ambazo zinatakiwa kujenga tuta pamoja na madaraja mengine yanahitajika matano,” alisema na kuongeza:
“Naapa mbele ya Mungu daraja hili nitalitengeneza na leo nikitoka hapa nakwenda kulitembelea, lakini Dk. Kafumu amezungumza mengi hapa kuna daraja la Manongana barabara zake nataka kukueleza kuwa nitatoa bajeti maalum kwa Igunga.”
Alisema kuwa aliona kwenye TV chama cha siasa kinaandamana kwenda katika mkutano huku wakiwa wamepanda punda.
CUF ndiwo walizindua kampeni zao rasmi kwa staili ya kutumia punda ambapo mgombea wake, Mahona na viongozi wengine wa chama hicho akiwemo Mwenyekiti wa Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba, walipanda katika mikokoteni unaokokotwa na wanyama hao.
“Kwa mujibu wa sheria namba 13 ya mwaka 2007, wale watu walikuwa wanapitisha punda kwenye barabara, walikuwa wanavunja sheria, lakini kwa mujibu wa sheria namba 18 ya mwaka 2008 ya mambo ya ngozi pamoja na sheria namba 19 ya mwaka 2008 ya ustawi wa wanyama huwezi ukampanda punda anavuja damu eti unaenda kwenye kampeni. Usidhanie watu hawajui sheria,” alisema Dk. Magufuli ambaye alikuwa akichanganya Kiswahili na Kisukuma.
MBOWE AKEMEA UDINI
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, amekemea mtindo unaodaiwa kufanywa na baadhi ya watu kwa kuvigawa vyama vya siasa katika misingi ya udini. Aliyasema wakati akihutubia mkutano wa kampeni katika uwanja wa Sokoni katika Kata ya Nkinga kumnadi mgombea wa chama chake, Joseph Kashindye.
Alisema ni wajibu wa viongozi wa vyama vyote vya siasa nchini kujenga mshikamano wa taifa na kuwaeleza Watanzania kuwa dini moja inatumiwa na chama fulani kujenga ufa ambao ni hatari kwa taifa.
Alisema CCM imeandaa mbinu chafu ili kuligawa taifa katika misingi ya imani.
“Ukiligawa taifa katika misingi ya dini unaleta hatari kubwa, awe CCM, awe wa Chadema, awe wa dhehebu la dini ipi,” alisema na kuongeza: “Tujenge mshikamano.”
CHANZO: NIPASHE

No comments: