Tuesday, September 6, 2011

Igunga: Uwanja wa Mkapa, Slaa


Slaa kurusha karata keshokutwa
  Mkapa kunguruma Jumamosi
Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa
Moto wa uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Igunga, mkoani Tabora unatarajiwa kuwashwa keshokutwa wakati Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, atakapozindua kampeni za chama chake na Jumamosi Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa, atakapozindua kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mkapa atazindua rasmi kampeni za kumnadi mgombea wa CCM, Dk. Peter Kafumu mjini hapa katika uchaguzi huo wa kujaza nafasi iliyoachwa na Rostam Aziz, aliyejiuzulu Julai 13, mwaka huu kwa maelezo kuwa amechoshwa na siasa uchwara, fitina na kuandamwa ndani ya CCM.


Mbali na kujiuzulu ubunge, Rostam pia alijiuzulu nafasi ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kupitia Mkoa wa Tabora.

Akizungumza na NIPASHE, Katibu wa CCM wa Wilaya ya Igunga, Neema Adam, alisema kuwa Mkapa atazindua kampeni hizo katika kiwanja cha Sokoine kilichopo mjini Igunga.

“Mheshimiwa Mkapa atazindua rasmi kampeni Septemba 10 (Jumamosi wiki hii ) katika kiwanja cha Sokoine mjini hapa,” alisema Adam.

Kwa upande wake, Mratibu wa kampeni za uchaguzi wa Chadema, Waitara Mwikabe, alisema kuwa kampeni hizo zitazinduliwa na Dk.  Slaa katika uwanja huo huo wa Sokoine keshokutwa.

“Mheshimiwa Katibu Mkuu ndiye atakayezindua kampeni zetu rasmi Septema 8,” alisema Waitara.

Chama cha Wananchi (CUF), kilishatangaza kuwa kampeni zake zitazinduliwa rasmi Septemba 13, mwaka huu.
Kampeni hizo zitazinduliwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba.

Vyama vyote vitatu vya CCM, Chadema na CUF vimetangaza kutumia helikopta katika mikutano yao ya kampeni zitakazoanza kutimua vumbi keshokutwa.

IGUNGA YAFURIKA WAGENI
Hali ya upatikanaji wa huduma muhimu ya malazi katika mji wa Igunga imeanza kuwa ngumu kutokana na nyumba za kulala wageni kujaa watu wanaotarajiwa kuwasili leo kwa ajili ya kampeni zinazotarajiwa kuanza kutimua vumbi keshokutwa.

Wateja waliokuwa wakifika katika nyumba hizo walikuwa wakijibiwa kuwa hakuna nafasi hadi Oktoba na kwamba wameshapokea malipo.

VYAMA VYAFIKIA NANE
Wakati huo huo, wagombea wa vyama viwili vya Chausta na UPDP wamejitokeza kuchukua fomu na kuongeza idadi ya wagombea kutoka sita hadi wanane.

Wagombea hao walichukua fomu za kuwania nafasi hiyo jana mchana katika ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga ambaye ndiye Msimamizi wa uchaguzi huo, Protace Magayane.

Aliyekuwa wa kwanza kuwasili katika ofisi za Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kuchukua fomu hizo ni mgombea wa UPDP, Hemed Ramadhan Dedi. Dedi aliyekuwa ameongozana na wanachama wenzake wawili, walitumia usafiri wa bajaji moja kati ya tatu zilifungwa bendera ya chama chake.

Mgombea huyo alifuatiwa na mgombea wa Chausta, Hassan Ramadhan Lutegana. 

Akizungumza baada ya kuwakabidhi fomu hizo, Magayane alisema kuwa leo saa 10:00 jioni itakuwa mwisho wa kurejesha fomu hizo baada ya wagombea kuzijaza.  Wagombea wengine ni na vyama vyao katika mabano ni  Dk. Peter Kafumu (CCM), Joseph Mwandu Kashindye (Chadema), Leopard Mahona (CUF), Lazaro Ndegaya (UMD), Said Makeni (DP) na John Maguma (Sau). 

Awali, TLP kilisimamisha John Maguma ambaye hata hivyo, alijitoa baadaye kwa madai ya kutelekezwa na chama hicho.
Katika hatua nyingine, maofisa uchaguzi wa Jimbo la Igunga jana walikuwa na kazi ya kuhakiki fomu za wagombea ambao walizipeleka kwao kabla ya kuzirejesha rasmi leo.

NIPASHE ilishuhudia vyama vya Chadema, CUF na CCM vikipeleleka fomu zao kwa maofisa uchaguzi kwa ajili ya kuhakikiwa kabla ya kuzirejesha leo. Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika Oktoba 2, mwaka huu baada ya kampeni kusitishwa siku moja kabla.

VIJANA 200 CCM KUPIGA KAMBI
Naye Lucas Macha anaripoti kutoka Tabora kuwa, CCM Mkoa wa Tabora, kimeamua kupeleka zaidi ya vijana 200 kuweka kambi kuhakikisha kinaibuka kidedea katika uchaguzi mdogo wa ubunge wa Igunga unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2, mwaka huu. Vijana hao watapelekwa katika kambi hiyo wilayani Iramba, Mkoa wa Singida.

Katibu wa UVCCM Mkoa wa Tabora, Julius Peter, alisema vijana hao watakwenda kuweka kambi itakayosaidia ushindi wa CCM kwenye uchaguzi mdogo Igunga na ni kawaida kwao kuwa na kambi hizo kila chaguzi.
CHANZO: NIPASHE

No comments: